Kazi ya kuhesabu kura kwenye uchaguzi wa bunge la Pakistan iliyofanyika tarehe 19 inaonesha kuwa, Chama cha Umma cha Pakistan kimepata kura nyingi zaidi, lakini kutokana na kuwa kura hizo hazikuzidi nusu ya kura zote, chama hicho hakiwezi kuunda serikali peke yake. Tarehe 19 vyombo vya habari vya Pakistani viliripoti kuwa kwa mujibu wa hesabu za mwanzo za kura, chama hicho kimepata viti 87, na chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan N kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani Bw. Nawaz Sharif kimepata viti 66, na chama kilichokuwa tawala yaani chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan Q kimepata viti 38 tu. Kwa mujibu wa katiba ya uchaguzi nchini Pakistan, kutokana na kuwa hakuna chama kilichopata zaidi ya nusu ya kura, Chama cha Umma kitashirikiana na vyama vingine kuunda serikali ya muungano.
Chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan N tarehe 19 kilitangaza kuridhika na uchaguzi huo, na mwenyekiti wa chama cha chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan Q Bw. Choudhry Shujaat na viongozi wengine pia wamekubali kupokea matokeo ya uchaguzi huo, na kukubali kushindwa katika uchaguzi huo. Bw. Shujaat alisema chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan Q kinakubali matokeo hayo na kushirikiana na vyama vingine kwenye nafasi ya vyama vya upinzani. Rais wa Pakistan Pervez Musharraf siku hiyo alisema yeyote atakayekuwa waziri mkuu na chama chochote kitakachounda baraza la mawaziri, yeye mwenyewe atashirikiana naye kikazi kwa "mapatano". Imefahamika kuwa tarehe 20 matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yatatangazwa rasmi, na serikali mpya itaundwa kabla ya tarehe mosi Machi, na bunge hilo litachagua spika, naibu spika na waziri mkuu.
Bunge la Pakistan linaundwa kwa baraza la chini na la juu, baraza la chini linaundwa kwa uchaguzi wa raia na baraza la juu linaundwa kwa idadi sawa ya wajumbe waliochaguliwa kutoka mabaraza ya chini na ya juu ya mikoa. Baraza la chini lina viti 342, na kati ya viti hivyo viti 70 ni vya ziada kwa ajili ya wanawake na watu wasio waislam. Katika uchaguzi huo watu 7000 watagombea viti 272 vya bunge la taifa na watu 577 watagombea viti vya bunge la mikoa. Kutokana na kuwa baadhi ya sehemu bado hazijakuwa salama, uchaguzi umeahirishwa katika sehemu hizo, katika uchaguzi wa bunge la taifa na uchaguzi wa bunge la mikoa watu waliogombea walipungua hadi kuwa 269 na 570.
Hivi sasa vyama vitatu ambavyo ni Chama cha Umma cha Pakistan, Chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan N na Chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan Q vinaongoza katika nafasi tatu za mwanzo kwa wingi wa kura. Lakini chama gani kitachaguliwa na Chama cha Umma cha Pakistan kushirikiana kuunda serikali litakuwa ni suala la kufuatiliwa zaidi. Kabla ya hapo vyombo vya habari viliona kuwa chama kilichokuwa tawala yaani Chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan Q kilikuwa na uwezekano zaidi kushirikiana na Chama cha Umma cha Pakistan. Lakini tarehe 19 mwenyekiti wa Chama cha Umma cha Pakistani Bw. Asif Ali Zardari kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, chama chake hakishirikiana na Chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan Q, kwa hiyo uwezekano huo haupo tena. Hivi sasa vyombo vingi vya habari vinaona kuwa Chama cha Umma cha Pakistan kitaungana na Chama cha Shirikisho la kiislamu la Pakistan N kuunda serikali mpya. Hali ilivyo ni kwamba Asif Ali Zardari tarehe 19 alidokeza kuwa Chama cha Umma cha Pakistan kimeshawasiliana kwa simu na kiongozi wa Chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan N Bw. Nawaz Sharif kuhusu kuunda serikali mpya, na tarehe 20 watakutana tena. Bw. Asif Ali Zardari alisema, kuzungumza na vyama vingine kunasaidia kuimarisha demokrasia ya taifa. Kwa sababu Chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan N kinatetea kumwondoa madarakani Rais Pervez Musharraf, tarehe 19 Nawaz Sharif kwenye mkutano na waandishi wa habari alimtaka Rais Pervez Musharraf ajiuzulu. Kwa hiyo vyombo vya habari vinaona wasiwasi kuwa, kama Chama cha Shirikisho la Kiislamu la Pakistan N kikishikilia msimamo wake mkali kwa Rais Pervez Musharraf, huenda italeta hali ya wasiwasi nchini Pakistan.
|