Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-20 20:23:18    
Maisha bora ya watu wa kabila la Washe wanaoishi kwenye mkoa wa Jiangxi

cri

Kabila la Washe lina lugha yake, lakini linatumia maandishi ya kabila la Wahan. Kabila hilo pia halina sikukuu maalumu ya kikabila, kwa hiyo watu wa kabila hilo wanasherehekea sikukuu za kabila la Wahan hasa sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China. Leo tutawaletea maelezo kuhusu watu wa kabila la Washe wanaoishi kwenye tarafa ya Zhangping ya mji wa Guixi mkoani Jiangxi.

Tarafa ya kabila la Washe ya Zhangping ina eneo la kilomita za mraba 122 na idadi ya watu 1,090, na mandhari na hali ya hewa kwenye tarafa hiyo ni nzuri sana. Watu wakiingia kwenye tarafa hiyo, wanavutiwa kwanza na uwanja wa sanamu za mizimu zinazowakilisha historia ndefu na utamaduni mkubwa wa kabila la Washe. Kwenye sehemu ya katikati ya uwanja huo wenye eneo la mita za mraba elfu moja, kuna ukuta na nguzo 4 kubwa za mizimu ambazo zina kipenyo cha mita moja na urefu wa mita tano, na picha nzuri za watu na wanyama zilichorwa kwenye ukuta na nguzo hizo. Naibu mchunguzi wa jumba la makumbusho la mji wa Guixi Bw. Xie Jiangeng alisema,

"Picha kwenye ukuta wa mizimu zinahusu hadithi ya mfalme wa mbwa, na zinaonesha kuzaliwa, kuhamia, kubadilika na kushiriki kwenye vita kwa mfalme wa mbwa, hasa kuhusu maisha ya uwindaji ya watu wa kale wa kabila la Washe pamoja na mbwa. Wanyama waliochorwa kwenye nguzo za mizimu ni kirin ambaye ni mnyama kwenye hadithi za kiasili za China, lakini kwa kweli wanyama hao ni mbwa, kwa kuwa watu wa kabila la Washe wanaona mbwa ni kama wahenga wao."

Bw. Xie Jiangeng alijulisha kuwa zamani watu wa kabila la Washe waliabudu mungu wa mbwa, kwa kuwa mbwa ni rafiki yao mkubwa katika maisha yao ya uwindaji, lakini sasa wasanii wanaona mnyama aliyeabudiwa ni kirin. Kuna hadithi moja nzuri inayomhusu mnyama huo kirin. Miaka mingi iliyopita, watu wa makabila tofauti walikuwa wanapambana mara kwa mara. Mfalme mmoja aliahidi kuwa mtu yeyote akiweza kumshinda adui yake, atamwoza binti yake mrembo. Kirin alibadilika kuwa binadamu na kupambana na adui wa mfalme, hatimaye alimwua adui huyo na kumwoa binti wa mfalme. Lakini Kirin hakupenda kuwa ofisa wa mfalme yule, alihamia kwenye mlima wa Fenghuang mkoani Guangdong pamoja na mke wake.

Licha ya utamaduni wa mizimu, desturi za jadi za kabila la Washe pia zinawavutia watu sana. Vijana wa kabila hilo wanachagua wachumba kwa kuimba nyimbo, mvulana akimpenda msichana mmoja, atamtuma mshenga kwenda nyumbani kwa msichana huyo, na msichana akimpenda mvulana, atafungua mlango ili kumkaribisha. Bw. Xie Jiangeng alisema,

"Harusi ya kabila la Washe ina umaalumu sana. Bwana harusi anapokwenda nyumbani kwa bibi harusi ili kumpokea, ni lazima ajibu maswali ya bibi harusi kwa kuimba nyimbo, akishindwa hataweza kumwoa."

Lakini kutokana na athari ya watu wa kabila la Wahan, sasa harusi ya kabila la Washe imebadilika na kufanana na kabila la Wahan, desturi ya zamani ya harusi inaonekana katika maonesho ya utamaduni.

Watu wa kabila la Washe pia ni hodari katika kuimba nyimbo na kucheza ngoma. Kuna ngoma za aina nyingi za kabila hilo, na kati ya ngoma hizo, ngoma ya taa zenye umbo la farasi imehifadhiwa vizuri zaidi. Ngoma hiyo ni ya kusherehekea mavuno, na huchezwa na watu zaidi ya 20. Wachezaji wanacheza ngoma hiyo huku wakiimba. Taa nyingine zinazotumiwa kwenye ngoma hiyo ni pamoja na samaki, vipepeo na ndege. Bw. Lei Manguo wa kabila la Washe ni shabiki wa ngoma hiyo alisema,

"Taa zinazotumika kwenye ngoma hiyo zina maana tofauti, Taa ya farasi inamaanisha mafanikio, ya samaki inamaanisha mapato mazuri, na ya vipepeo ni ishara ya mapenzi. Ni matumaini yetu kuleta furaha na baraka kwa sehemu zote za kabila la Washe."

Baada ya kucheza ngoma hiyo, sanamu zilizotumiwa zitachomwa moto ili kutoa sadaka kwa wahenga. Kutokana na maendeleo ya jamii, ngoma hiyo ya kabila la Washe imepata maendeleo mapya. Bw. Xie Jiangeng alisema,

"Sasa ngoma ya taa za farasi imekuwa na vitu vipya na imekuwa na mabadiliko makubwa zaidi. Zamani ilichezwa kuanzia tarehe 28 mwezi Desemba hadi tarehe 15 mwezi Januari kwa kalenda ya kilimo ya China, lakini sasa pia inachezwa wakati wa kuwakaribisha wageni."

Sasa kila wakati wa sikukuu au kutokea kwa mambo mazuri, watu wa kabila la Washe wanacheza ngoma ya sanamu ya farasi ili kufanya sherehe. Ngoma hiyo sasa inajulikana kote nchini China. Tangu mwaka 1996 ngoma hiyo imechezwa katika michezo minne ya makabila madogo madogo nchini China, na mwaka 1999 ilichezwa katika tamasha la kusherehekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu China, na watazamaji waliipenda sana.

Kabila la Washe pia lina nyimbo nyingi za kikabila, kwa sasa zilizoenea ni zaidi ya elfu moja. Nyimbo hizo zina aina tatu, yaani zinazohusu kuchuma majani ya michai, za mapenzi na za maswali na majibu.

Utamaduni mkubwa unawafanya watu wa kabila la Washe waone fahari kubwa, na maisha bora yanawaletea furaha. Zamani kutokana hali duni ya mawasiliano, watu wa kabila hilo walioishi kwenye tarafa ya Zhangping walikuwa maskini sana, lakini sasa kutokana na misaada ya serikali, maisha ya watu hao yameboreshwa sana. Mkazi wa tarafa hiyo Bw. Lei Xianggui alisema,

"Zamani kwenye tarafa yetu hakukuwa na barabara na umeme, mapato ya kila mtu yalikuwa karibu Yuan mia tano kwa mwaka, lakini sasa tunaishi maisha bora."