Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-21 16:51:17    
Kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa ni kazi ya pamoja duniani

cri

Kongamano la Tano la watungaji sheria la kundi la nchi 8 na nyingine tano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani lilifunguliwa tarehe 20 mjini Brasilia, mji mkuu wa Brazil. Mjumbe wa China aliyehudhuria kongmanano hilo alisema, ni lazima suala hili litekelezwe kwa busara. Wajumbe zaidi ya mia moja kutoka kundi la nchi kubwa nane na nchi tano zinazoendelea za China, Brazil, India, Mexico na Afrika Kusini walihudhuria kongamano hilo. Mkuu wa ujumbe wa China Bw. Cao Buochun kwenye ufunguzi wa kongamano hilo alisema, China itajitahidi kuinua uwezo wake wa kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa mujibu wa hali yake, na hatua zinazochukuliwa ni thabiti na za kudumu. Alisema,

"Mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa si ya leo wala kesho bali ni ya muda mrefu, ni lazima jumuyia ya kimataifa iheshimu kanuni za 'Makubaliano ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa' na 'Mkataba wa Kyoto' na hasa 'kufuata kanuni kwa mujibu wa hali ilivyo' ".

Kuhusu suala la ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme ambalo linalofuatiliwa sana, Bw. Cao Buochun baada ya hotuba yake alionesha video ikionesha jinsi China inavyojitahidi kufunga vituo vidogo vya kuzalisha umeme. Baada ya kutizama video hiyo wajumbe wengi waliona kuwa China imefanya juhudi nyingi katika kudhibiti utoaji wa hewa chafu. Mbunge wa Ghana anayeshughulikia suala la mabadiliko ya hali ya hewa Bw. Joseph Boahen Aidoo alisema,

"Kwa mujibu wa video iliyooneshwa, kweli China imetoa mchango katika kupunguza hewa chafu kutokana na kufunga vituo vidogo vya kuzalisha umeme, kwa sababu vituo hivyo vinatumia nishati ya visukuku".

Kamati ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani, IPCC, hivi karibuni ilitoa ripoti ikisema, mabadiliko ya hali ya hewa hivi leo yanahusiana na matumizi ya nishati ya visukuku tokea miaka 200 iliyopita, uamuzi huo umeonesha wazi ni nani wanawajibika na mabadiliko hayo. Kaimu waziri wa mambo ya nje wa Brazil Bw. Samuel Guimaraes alisema,

"Kutokana na sababu za kihistoria, nchi zilizoendelea zimesababisha kuwepo kwa hewa chafu nyingi, hata kama nchi zinazoendelea zinapunguza namna gani, tatizo hilo bado ni kubwa."

Mabadiliko ya hali ya hewa ni suala linalozikabili nchi zote, na nchi zilizoendelea zinawajibika zaidi. Waziri mkuu wa nchi mwenyeji wa kongamano hilo, Japan, alitoa hotuba kwa njia ya video iliyoletwa kwenye kongamano hilo akisema, Japan itatoa msaada wa dola za Marekani bilioni 10 kwa ajili ya kuzisaidia nchi zinazoendelea kupunguza hewa chafu, licha ya nchi hiyo kujitahidi kupunguza utoaji wa hewa chafu. Wajumbe wengi wanaona kuwa inafaa nchi zinazoendelea ziungane ili kupambana kwa pamoja na suala hilo la mabadiliko ya hali ya hewa. Mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Brazil Bw. Alex anakubaliana kabisa msimamo wa jumbe wa China, alisema,

"Naona hotua ya mjumbe wa China ni ishara kwa nchi zilizoendelea kwamba kigezo cha utoaji wa hewa ya caborn dioxide hakifai kuwekwa na nchi zilizoendelea na kutekelezwa na nchi zinazoendelea. Hadi sasa nchi zinazotoa hewa chafu zinaendelea kuwa ni nchi zilizoendelea."

Nchi za magharibi zinapotaja suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani huzinyooneshea kidole China na India badala ya nchi zinazotoa hewa hiyo kwa wingi. Hali hiyo inaikera jumuyia ya "SOS" ya kuhifadhi mazingira nchini Brazil, mjumbe wa jumuyia hiyo alisema,

"Marekani haifanyi chochote ila tu kuzishutumu China, India na nchi nyingine ambazo zinatoa 17% tu ya hewa chafu duniani. Idadi ya watu wa Marekani ni milioni 300 tu ambayo ni 4% ya dunia nzima, lakini hewa chafu inayotolewa na nchi hiyo inachukua 25% ya dunia nzima, huu ni uhalifu kwa binadamu. Lakini China na India, nchi zenye watu bilioni mbili zinatoa 17% tu ya hewa chafu".

Suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani ni lazima lishughulikiwe na nchi zote duniani, na wala sio nchi moja na serikali moja.