Mjumbe maalumu wa serikali ya China anayeshughulikia suala la Darfur Bw. Liu Guijin, tarehe 21 kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mjini London, alifahamisha hali ilivyo ya mgogoro wa Darfur na msimamo wa serikali ya China kuhusu suala hilo. Bw. Liu Guijin alieleza jitihada zilizofanywa na serikali ya China ili kutatua mgogoro wa Darfur. Alisema kutokana na jitihada za pamoja za China na jumuiya ya kimataifa, serikali ya Sudan ilikubali operesheni ya kulinda amani kwa jeshi la mseto, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 1769, na utatuzi wa suala la Darfur ukaanza kufuata njia sahihi. Bw. Liu alisema
"Utatuzi wa suala la Darfur unahusu mambo mengi, na unahitaji juhudi za pande zisizopungua tano. Upande mmoja ni serikali ya Sudan, wa pili ni makundi ya upinzani, ni matumaini yangu kuwa makundi hayo yatarudi kwenye meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo, kwani bila maendeleo ya mchakato wa kisiasa na bila kuwa na makubaliano kati ya serikali na makundi hayo, ni vigumu kukomesha mapambano, kuboresha hali ya usalama na kufanya operesheni za kulinda amani kwa jeshi la mseto huko Darfur. Upande wa tatu ni jitihada za jumuiya ya kimataifa, kwani hivi sasa bado kuna matatizo ya kiufundi katika kuweka walinzi wa amani wa jeshi la mseto. Upande wa nne ni jitihada za nchi mbalimbali katika kanda hiyo na majirani wa Sudan. Na upande wa tano ni jitihada za Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, ambazo zinatakiwa kutumia ipasavyo mfumo wa mazungumzo kati ya pande tatu za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Sudan, kuharakisha mchakato na kutatua masuala yaliyosababishwa na kutokuelewana na masuala ya kiufundi."
Kuhusu kanuni ya serikali ya China juu ya mgogoro wa Darfur, Bw. Liu Guijin alieleza kuwa China ilitoa ushawishi wenye manufaa, lakini haikubali njia ya kutatua migogoro ya kikanda kwa kuweka shinikizo au kwa njia ya kuwalazimisha watu wakubali maoni ya upande mmoja. Alisema
"Sisi tunafuata kanuni moja ya kimsingi, nayo ni kuheshimu mamlaka ya Sudan na ukamilifu wa ardhi yake, hii ni kanuni ya kutafuta utatuzi wa mgogoro wa Darfur, suala la Sudan na mapambano ya kikanda yanayohusika. Nafurahia kuona kuwa nchi nyingi zikiwemo Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya, zinakubali njia hiyo. Natoa mfano wa shughuli za ulinzi wa amani, China iliposhika nafasi ya mwenyekiti wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, azimio namba 1769 lilipitishwa tarehe 31 Julai mwaka jana. Lakini kwa upande mwingine, China inaona ni lazima azimio hilo likubaliwe na serikali ya Sudan, ama sivyo halitaweza kutekelezwa bila uungaji mkono na ushiriki wa serikali ya Sudan. Kutokana na mchakato wa utatuzi wa suala la Darfur, China itatoa mchango zaidi na kubeba wajibu mkubwa zaidi katika utatuzi wa mapambano mengine yanayotokea katika nchi zinazoendelea. Vile vile China imetambua kuwa, inapaswa kuzingatia ufuatiliaji wa pande mbalimbali, na kwa kufanya hivyo ndipo masuala yatakapotatuliwa hatua kwa hatua."
Kuhusu suala la baadhi ya watu kujaribu kususia michezo ya Olimpiki ya Beijing kwa kutumia suala la Darfur, Bw. Liu Guijin alisema, (sauti 3) "Narudia mara kwa mara kuwa, Darfur haipo nchini China, wala suala la Darfur si suala la China, kwa hiyo haina maana yoyote kuhusisha masuala hayo mawili yasiyo na uhusiano wowote. Pia napenda kusema hivi sasa kwenye jumuiya ya kimataifa zimejitokeza sauti za haki ambazo pia zimetambua jambo hilo, kwamba iwapo jumuiya ya kimataifa inahamasisha maoni na vitendo vya kuifanya michezo kama michezo ya Olimpiki iwe ya kisiasa, hii ni hatari sana kwa upeo wa mbali. Kwa mfano, London utakuwa mji mwenyeji wa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012, ambapo kama kutakuwa na watu watakaotoa suala lisilo na uhusiano wowote na michezo ya Olimpiki, basi litakuwa ni jambo la kuibana nchi hiyo."
|