Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-25 16:19:38    
Mwimbaji mlemavu Liang Fuping

cri

Katika mji wa mlimani Chongqing, kusini magharibi mwa China, yupo mwimbaji mmoja anayejulikana kote mjini humo, ambaye si mmahiri wa kuimba tu bali pia ni mtungaji nyimbo. Kutokana na ulemavu wa mguu wa kulia, inampasa abebe gitaa mgogoni na kutembea kwa bakora. Mwimbaji huyo licha ya kushiriki kwenye mashindano ya kuimba, pia ametoa albamu. Ingawa maisha yake ni ya shida sana, lakini anakabiliana nayo kwa tabasamu. Mwimbaji huyo anaitwa Liang Fuping.

Bw. Liang Fuping anaishi katika nyumba ya zamani mjini Chongqing. Kutokana na shida ya kutembea, aliyetoka kutukaribisha alikuwa mke wake Bibi A Jiao.

Tulipoingia tu ndani mara tulimwona mwimbaji huyo aliyekuwa amekaa kwenye kochi. Ana nywele fupi na uso wa mraba ulionawiri, anaonekana mwenye sura nzuri zaidi kuliko picha tuliyokuwa nayo kabla ya kumwona. Siku hiyo nyumbani kwake kulikuwa na wageni wengi, chakula na bia zilitapakaa mezani.

Mazungumzo yalipoanza kuhusu Bw. Liang, watu walifurahi kutueleza.

Binti yake alisema,

"Namheshimu sana baba yangu toka nilipokuwa mtoto, yeye ni mjasiri na siku zote hatarudi nyuma akikumbwa na matatizo."

Mdogo wake alisema,

"Anaweza kupiga kinanda cha mdomo, kodiani, fidla, na ala nyingine zote. Kaka yangu ni kiongozi wa roho yangu."

Rafiki yake pia alimsifu sana akisema,

"Bw. Liang Fuping ana kipaji cha muziki toka alipokuwa mtoto, ni mtu mwenye juhudi na mwenye msamaha kwa wengine."

Mke wake alisema,

"Napenda sana nyimbo zake, anapoimba ananifanya nitake kucheza."

Bw. Liang Fuping alipozungumza nafsi yake alisema kwa msisimko,

"Tumaini langu ni kuufanya muziki wangu usikike kwa wote."

Bw. Liang Fuping alizaliwa mwaka 1963 katika familia ya kawaida mjini Chongqing, mama yake alikuwa mfanyakazi wa kiwanda cha nguo, na sasa ni mgonjwa, baba yake alikuwa mfanyakazi katika idara ya reli na kutokana na shughuli nyingi hakuwa na nafasi ya kushughulika na kazi za nyumbani. Liang Fuping alipokuwa na umri wa miaka miwili alipata ugonjwa wa polio, mguu wake wa kulia umelemaa. Alipokumbuka hali ya zamani alisema alikuwa hawezi kucheza na watoto wenzake, muziki ulikuwa rafiki yake mkubwa wa kila siku.

"Ninapenda sana muziki toka nilipokuwa mtoto na hasa kuimba. Niliposikiliza nyimbo nilikuwa najiuliza ni kwa nini wimbo niliosikiliza ulitungwa hivi na kwa nini muziki unaendelea vile, masuali ambayo ni ajabu kwa wengine kujiuliza."

Liang Fuping alitumia muda mwingi kujifunza muziki, alipata elimu ya kimsingi ya muziki katika shule ya sekondari na kujizoesha kuimba nyumbani, baadaye alikuwa akiimba kando ya mto Jialing ulio karibu na nyumbani kwake, kila siku alifanya mazoezi kwa muda wa saa mbili bila kujali hali ya hewa ikiwa mbaya namna gani. Mdogo wake alisema,

"Nilikuwa pamoja na kaka yangu kila siku, katika majira ya joto niliogelea mtoni na kaka yangu alikuwa anaimba kando ya mto, mvua ikinyesha nilimkinga kwa mwavuli na nilimbeba mgongoni mpaka sasa."

Bw. Zhang Chaoming aliyekuwa pamoja na Liang Fuping walipokuwa watoto alisema, ingawa muda wao wa kuwa pamoja ulikuwa mfupi, lakini urafiki wao ni mkubwa. Alisema,

"Urafiki wetu ulianza tulipokuwa watoto, wakati huo tuliishi karibu na ukingo wa mto Jialing. Jioni alikuwa anapiga gitaa kando ya mto na mimi niliogelea, tulicheza na kuongea, maisha hayo nayakumbuka sana."

Mto Jialing ulishuhudia jinsi Bw. Liang Fuping alivyopenda muziki, na mto huo pia ulimpatia msukumo wa muziki wake, alitunga wimbo wake wa kwanza wa "Mto Mzuri Jialing" kando ya mto huo. Kwa hiyo kila anaposimama kwenye mto huo huwa ana hisia nyingi.

Mwaka 1982 Liang Fuping kwa mara ya kwanza alipata ajira katika kiwanda kimoja, mishahara yake ilimwezesha kununua ala zake anazopenda, na alipata nafasi nyingi za kufanya maonesho.

"Nilinunua gitaa moja kwa kulimbikiza mishahara ya mwaka mmoja mzima, katika siku nilipopata gitaa hiyo nilipiga siku nzima, nilifurahi hata sikutaka kula. Kwa sababu ya uhodari wa kuimba mara nyingi nilikuwa napata tuzo kwa niaba ya kiwanda changu baada ya kuwashinda waimbaji waliotumwa na viwanda vingine, wakati huo nilijivunia sana."

Wakati huo mara kwa mara alikuwa anakiwakilisha kiwanda chake kushiriki kwenye mashindano, na alipata tuzo nyingi. Lakini kutokana na ndoa na kupata mtoto, maisha yakawa magumu, mshahara wake mdogo haukuweza kukidhi mahitaji ya maisha ya familia yake yenye watu watatu. Alisema,

"Binti yangu alizaliwa mwaka 1989, mke wangu alikuwa hana ajira, mshahara wangu ulikuwa mdogo, wakati huo kwa ujasiri niliamua kuacha kazi ya kiwandani na kuwa mwimbaji njiani."

Bw. Liang Fuping alianza kuchuma pesa kwa kuimba kutoka kwenye mkahawa mmoja hadi mwingine. Mwanzoni alikuwa anazunguka mjini Chongqing, baadaye alikwenda kwenye sehemu ya kusini ya China, aliimba nyimbo zilizokuwa zinachaguliwa kutoka kwenye orodha ya nyimbo zake.

"Nililazimika kuimba kwa kuzungukazunguka, kama maisha yangu yangekuwa kama watu wa kawaida kamwe nisingekubali kufnya hivyo."

Chaguo lake la kuimba kwa kuzunguka halikusaidia kuboresha maisha yake, kinyume chake, ndoa yake ilivunjika. Mwaka 2002 aliachana na mke wake wa kwanza. Hata hivyo, ni muziki ulimwokoa kutoka hali mbaya. Mwaka 2005 Bw. Liang Fuping alishiriki kwenye mashindano ya kitaifa ya waimbaji walemavu na alipata tuzo ya kwanza. Pamoja na tuzo hiyo pia alivuna mapenzi yake. Siku moja kwenye tafrija alifahamiana na mke wake wa sasa Bi. A Jio. Mke wake aliona ulemavu wa mguu wake wa kulia sio kikwazo kwa mapenzi yao, anapenda nyimbo za mumewe na anapenda zaidi kipaji chake cha muziki na kuheshimu nia yake thabiti ya kupambana na shida za maisha. Alisema,

"Kwanza nyimbo zake zilivutia hisia zangu, pili kipaji chake cha muziki kilinifanya nijivunie yeye. Mume wangu ni mtu anayewajibika kwangu na familia yetu, kila ninapofikiri hayo machozi yananilengalenga."

Binti yake pia anafurahi kwa kuwa na familia kamili. Alisema,

"Mama yangu ananipenda sana ingawa si mama yangu mzazi, ni mtu mwenye roho nzuri. Sisi watatu kila siku tunaishi kwa furaha."

Baada ya juhudi za miaka mingi mwezi Desemba mwaka 2007 albamu ya Bw. Liang Fuping ilitolewa na kuuzwa kote nchini.

Bw. Liang Fuping alisema, albamu hiyo ni sauti kutoka rohoni mwake na ni masimulizi ya maisha yake. Alisema,

"Njia yangu niliyopita ilitoka kutoka kujidhalilisha hadi kujiamini na kujiimarisha. Mungu amenifungia mlango lakini amenifungulia dirisha kupitisha mwangaza wa jua chumbani, nauthamini na kuufurahia mwangaza huo, ingawa mimi ni mlemavu lakini si kitu."

Idhaa ya kiswahili 2008-02-25