Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-25 16:08:17    
Picha za kuchorwa na za kukatwa katika Mwaka Mpya wa jadi wa China

cri

Kuna aina nyingi za sanaa za jadi za Kichina ambazo ni sehemu muhimu ya utamaduni wa China.

Tumewahi kueleza kwamba sikukuu ya Spring, yaani sikukuu ya Mwaka Mpya wa jadi wa China ni sikukuu muhimu zaidi kati ya sikukuu zote nchini China. katika siku za kukaribia sikukuu hiyo, kila familia hubandika mlangoni karatasi ndefu na nyekundu zenye maneno ya kuomba mema na kubandika picha za mwaka mpya madirishani, picha hizo ni za kuchorwa na za kukatwa kwa karatasi nyekundu.

Picha za kuchorwa na za kukatwa kwa katarasi ni picha maalum kwa ajili ya sikukuu ya Spring. Hapo awali picha hizo za kusherehekea Mwaka Mpya zilianza kuchorwa zama za kale, ambapo watu walichora mungu fulani aliyeelezwa katika hadithi kwenye karatasi na kubandika mlangoni ili kuzuia mashetani na kuepusha majanga. Kutokana na jamii inavyoendelea, picha hizo za kuchorwa kwa mikono zimekuwa picha za kuchapwa kwa mbao iliyochongwa, na mambo ya picha hayakuwa tena ya miungu, bali ni ya aina mbalimbali zikionesha matumaini ya watu kwa mwaka mpya.

Picha za Mwaka Mpya huwa na rangi nyekundu, kijani na nyeusi, na kuonesha watu ndani ya hadithi, wanyama na mandhari ya vijijini kwa kutia chumvi kwa ajili ya kuchangia furaha ya sikukuu. Kwa mfano picha ya "Mzee Mwenye Maisha Marefu", mzee huyo anachorwa kwa mujibu wa mzee mwenye maisha marefu anayesimuliwa kwenye kadithi simulizi, mzee huyo ana kipaji cha kujitokeza mbele, ana mvi na ndevu nyeupe na bakora mkononi, anatabasamu wakati wote anapokea salaamu za watu wanaomwamkia.

Picha za Mwaka Mpya zilizo maarufu zaidi ni picha kutoka sehemu ya Yangliuqing mjini Tianjin, Weifang mkoani Shandong, Taohuawu mjini Suzhou na Jinzhu mkoani Sichuan. Kutokana na mabadiliko ya jamii familia zinazobandika picha hizo zinapungua lakini sanaa yake ina thamani kubwa katika utamaduni wa jadi wa China.

Baada ya kueleza picha za Mwaka Mpya wa jadi wa China, sasa tueleze picha za kukatwa.

Picha za kukatwa ni aina nyingine ya sanaa ya jadi, ni picha za kukatwa kwa mkasi. Nchini China sanaa hiyo inajulikana sana hata watoto wa shule za msingi wanafundishwa sanaa hiyo. Sanaa hiyo ya sehemu tofauti nchini China ina mitindo tofauti na mambo yanayooneshwa katika picha hizo pia ni tofauti. Kwa ujumla picha za kukatwa katika sehemu ya kaskazini ya China zinakatwa kirahisi na kuonesha mambo kwa kutia chumvi zaidi, na ukataji wa picha wa sehemu ya kusini ya China una kazi nyingi na unaonesha mambo kwa makini zaidi.

Mambo ya kuoneshwa katika picha za kukatwa ni mengi zaidi ikilinganishwa na mambo yanayooneshwa katika picha za Mwaka Mpya zinazochapwa kwenye mbao, picha kama za watu mashuhuri ndani ya hadithi, wanyama, maua, ndege, michezo na hadithi za kale, zote zinaweza kuoneshwa. Picha za kukatwa ziko tofauti kwa ukubwa, picha iliyo ndogo inaweza kuwa kama kucha ya kidole cha mtu na picha kubwa inaweza kuwa na mita mia moja za mraba. Hivi karibuni, Bw. Hao Xianyi wa mkoa wa Xinjiang kwa nusu ya mwaka alikata picha kubwa yenye ukubwa wa urefu wa mita 50 na upana wa mita 1.3, ni picha inayoonesha mandhari ya sehemu mbalimbali za mkoani Xinjiang. Bw. Hao Xianyi alisema, anataka kusherehekea michezo ya Olimpiki ya Beijing kwa picha yake.

Kutokana na mila na desturi, katika siku ya mwisho ya mwaka Wachina hubandika sebuleni, chumbani na madirishani picha za Mwaka Mpya za kuchorwa na picha za kukatwa, ili kupamba nyumba zao kwa mazingira ya sikukuu ya mwaka mpya.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-28