Waziri wa mambo ya nje wa Sudan, Bw. Deng Alor tarehe 24 huko Khartoum alikuwa na mazungumzo na mjumbe maalumu wa serikali ya China anayeshughulikia suala la Darfur Bw. Liu Guijin, aliyekwenda ziarani nchini Sudan. Baada ya mazungumzo yao, waziri Deng Alor alihojiwa na waandishi wa habari wa China. Alipozungumzia uhusiano kati ya nchi hizi mbili waziri Alor alieleza kuwa, China si rafiki wa serikali ya Sudan tu, bali pia ni rafiki wa watu wa Sudan, akisema,
"barani Afrika, hususan nchini Sudan, China ni nchi inayokaribishwa sana, kwani China ni rafiki yetu. China ipo Sudan kwa ajili ya kuusaidia ujenzi wa Sudan, China siyo tu inashughulikia utoaji wa mafuta ya petroli, bali pia inashughulikia kazi za sekta nyingine. Zaidi ya hayo, China ikitumia uhusiano mzuri na Sudan, inajitahidi kutatua suala la Darfur."
Kuhusu baadhi ya jumuiya zisizo za kiserikali na watu wa nchi za magharibi wanaohusisha suala la Darfur na michezo ya Olimpiki ya Beijing waziri Alor alisema, Sudan inapinga kuhusisha masuala hayo mawili, akisema,
"Hatutarajii kuwa China itapatwa na athari mbaya au matatizo kutokana na mambo ya Sudan, na wala hatutaki michezo ya Olimpiki isusiwe. Sasa kuna kauli kutoka nchi za magharibi inayoitaka China iingilie suala la Darfur moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kauli hiyo si sahihi. Ninaona serikali ya Sudan, ambayo ni rafiki wa China, inawajibu wa kubadilisha msemo huo."
Waziri Alor alisema hivi sasa utatuzi wa kisiasa wa suala la Darfur uko nyuma kabisa ya mchakato wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, tatizo kubwa ni kwamba makundi mbalimbali ya kisiasa ya upinzani kwenye sehemu ya Darfur, hayawezi kushiriki kwenye mazungumzo yakiwa na maoni ya namna moja, alisema?
"Kitu muhimu kwa suala la Darfur ni kuweko umoja wa vikundi vyote vya upinzani vilivyoko kwenye sehemu ya Darfur. Hivi sasa kuna makundi mengi yenye silaha kwenye sehemu ya Darfur, vikundi zaidi ya 20 hivyo vinashindwa kufikia maoni ya namna moja katika muda mfupi, hili ni tatizo kubwa linalotukabili, tunashindwa kufanya mazungumzo na makundi ya upinzani vyenye maoni ya aina mbalimbali."
Waziri Alor alieleza kuwa ingawa kuna matatizo mengi kwenye utatuzi wa suala la Darfur, lakini serikali ya Sudan itaendelea kufanya juhudi za kuleta amani kwenye sehemu ya Darfur, alisema;-
"Kwanza, ni lazima makundi ya upinzani yawe na msimamo wa namna moja, kisha yachague mwakilishi mmoja au wawakilishi wawili kushiriki kwenye mazungumzo. Pili, tunahitaji kuboresha uhusiano na Chad, bila kufanya hivyo, utatuzi wa suala la Darfur utakabiliwa na shida. Mbali na hayo, tunahitaji kupanga jeshi la mseto la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika mahali yanapotakiwa, bila kuboreshwa kwa hali ya usalama, upangaji wa jeshi la kulinda amani pia utapatwa na shida."
|