Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-26 16:43:04    
Je, uchumi wa Marekani unaokabiliwa na hatari ya kuzorota utaathiri ongezeko la uchumi duniani?

cri

Tokea mwezi Aprili mwaka jana msukosuko wa mikopo ya nyumba ulipotokea nchini Marekani, uchumi wa Marekani umekuwa katika hali ya kusuasua. Kutokana na hali mbaya ya soko la ajira, idadi ya watu wanaopoteza ajira kuongezeka na kupungua kwa imani ya wateja, wataalamu wengi wanaona kuwa uchumi wa Marekani umekuwa katika hali ya kuzorota, na baadhi wanaona kuwa hivi sasa Marekani imekuwa ikisababisha mfumuko wa bei na kuathiri maendeleo ya uchumi duniani. Lakini baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa hali hiyo ya Marekani, haitasababisha uchumi wa dunia nzima kuzorota.

Ripoti ya "Shirika la Kitaifa la Uchumi wa Biashara" la Marekani tarehe 25 ilisema, 45% ya wataalamu wa shirikisho hilo wanaona kuwa uchumi wa Marekani utakumbwa na hali ya kuzorota, na wataalamu 55% wanaona kuwa ingawa uchumi wa Marekani hautakumbwa na hali ya kuzorota, lakini ongezeko lake litakuwa kiasi cha 1.8% tu, ambacho ni chini kabisa ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita, na mwezi Juni mwaka huu pengine uchumi utapungua badala la kukua.

Mwenyekiti wa zamani wa Hazina ya Marekani Bw. Alan Greenspan tarehe 25 alisema ongezeko la uchumi wa Marekani limeanza kutulia, ongezeko lake ni sufuri. Alisema muda wa kutulia kwa ongezeko la uchumi wa Marekani ukiwa mrefu zadi uwezekano wa kuzorota kwa uchumi huo ambao ni muhimu duniani, utakuwa mkubwa zaidi.

Hali ya kuongezeka polepole kwa uchumi imesababisha Hazina ya Marekani kuchukua sera ya kupunguza riba, ili kuchochea ongezeko. Tokea mwezi Septemba mwaka 2007, Hazina ya Marekani ilipunguza kiwango cha riba hadi 3% kutoka 5.25% na pengine kiwango hicho kitapungua hadi kufikia 2.25% mwishoni mwa mwaka huu. Lakini sera ya kupunguza riba pamoja na bei kubwa ya mafuta, hakika vitasababisha mfumuko wa bei nchini Marekani. Kwa mujibu wa wizara ya kazi ya Marekani, mwezi Januari bei ya bidhaa kwa wastani ilipanda 4.3% ikilinganishwa na mwaka jana, na bei ya chakula inapanda zaidi. Mwezi Januari kiasi cha ongezeko la mfumuko wa bei kimeongezeka kwa 2.5% ambacho ni kikubwa kuliko kilichokadiriwa na Hazima ya Marekani, yaani kati ya asilimia moja na mbili.

Kutokana na utandawazi wa uchumi duniani na biashara huria, mfumuko wa bei nchini Marekani hakika utaathiri uchumi wa dunia. Baadhi ya wataalamu wanaona kuwa kwa sababu baadhi ya nchi za Asia zinaendelea na sera za kujihusisha na thamani ya dola za Marekani, sera ya kupunguza riba nchini Marekani hakika itasababisha mfumuko wa bei wa dunia nzima, kwa hiyo Marekani imekuwa ikisababisha mfumuko huo nje ya Marekani.

Hivi sasa nchi ambazo zinahusiana na uchumi wa Marekani kwa karibu zaidi, zimekuwa zikikumbwa na mfumuko wa bei kwa viwango tofauti. Mfumuko wa bei nchini Saudi Arabia umekuwa mkubwa ambao haukuwahi kutokea katika miaka 16 iliyopita. Na mfumuko huo nchini Uswisi umekuwa mkubwa ambao haukuwahi kutokea miaka 14 iliyopita, na Singapore imekuwa na mfumuko huo ambao haukuwahi kutokea katika miaka 25 iliyopita. Katika nchi zinazotumia Euro kiasi cha mfumuko huo imefikia 3.2% ambacho hakikuwahi kutokea katika miaka 14 iliyopita.

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wanakadiria kwamba ingawa hali mbaya ya uchumi wa Marekani itaathiri uchumi duniani, lakini haitaathiri hadi kusababisha kushuka kwa uchumi duniani. Hivi sasa msukosuko wa mikopo unaathiri sehemu ndogo tu ya uchumi wa Marekani, na hali ya uchumi kwenye sekta nyingine kwa ujumla ni nzuri. Zaidi ya hayo sera ya Rais George Bush ya kutenga dola bilioni 168 na hatua ya Hazina ya kupunguza riba, zitachochea ongezeko la uchumi wa Marekani. Hii inamaanisha kuwa hata kama uchumi wa Marekani ukitokewa na hali ya kuzorota, muda wake ni mfupi tu, na cha muhimu zaidi ni kuwa utandawazi na uhuria wa biashara duniani, vitapunguza makali ya hali mbaya ya uchumi wa Marekani. Na licha ya Marekani, nchi za Umoja wa Ulaya na Japan, nchi nyingine kama Brazil, India, China na Russia na nchi nyingi nyingine zinazoendelea, zitasukuma mbele maendeleo ya uchumi wa dunia.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-26