Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-27 16:38:46    
Kundi la okestra la New York lafanya maonesho ya kihistoria mjini Pyongyang

cri

Kundi maarufu la muziki la Marekani yaani Kundi la Okestra la New York, tarehe 26 lilifanya maonesho ya kihistoria mjini Pyongyang, mji mkuu wa Korea ya Kaskazini. Hii ni mara ya kwanza kwa kundi la muziki la Marekani kufanya ziara nchini Korea ya Kaskazini tokea nchi hiyo iasisiwe Septemba 1948. Maonesho yamepata mafanikio makubwa.

Watazamaji walipiga makofi kwa shangwe wakati mwongoza muziki wa kundi hilo alipopanda jukwaani akiwa amevaa suti nyeusi. Jukwaani kwenye upande wa kushoto ilitundikwa bendera ya taifa ya Korea ya Kaskazini, na kwenye upande wa kulia ilitundikwa bendera ya taifa ya Marekani, jumba lenye viti 1,500 lilikuwa limejaa kabisa. Muziki wa kwanza ulikuwa wimbo wa taifa wa Korea ya Kaskazini, na uliofuata ni wimbo wa taifa wa Marekani.

Kisha kundi hilo lilipiga sehemu ya muziki wa opera ya mwanamuziki wa Ujerumani Bw. Wagner na Simfoni No. 9 ya 'Kutoka Bara Jipya' iliyotungwa na mwanamuziki mkubwa wa Czechoslovakia ya zamani Bw. Dvorak na muziki uitwao "Mmarekani mmoja mjini Paris".

Kabla ya kupiga muziki huo, mwongoza muziki wa kundi hilo alisema machache ambayo yalisababisha watazamaji kucheka na kupiga makofi. Alisema,

"Muziki ufuatao ni muziki mashuhuri uliotungwa na mwanamuziki mkubwa wa Marekani Bw. Gershwin, unaitwa 'Mmarekani mmoja mjini Paris'. Natumai baadaye utatokea muziki uitwao 'Mmarekani mmoja mjini Pyongyang'. Karibuni msikilize."

Maonesho yalikuwa ya muda wa saa moja na nusu, wanamuziki walipiga muziki kwa umahiri na watazamaji walisikiliza kwa makini, na kila baada ya muziki mmoja kumalizika makofi hupigwa kwa muda mrefu. Baada ya muziki wote kumalizika kundi hilo lilipiga muziki mwingine mara tatu kutokana na kuombwa na watazamaji kwa makofi ya muda mrefu. Muziki wa mwisho ni wimbo ulioenea sana miongoni mwa watu wa Korea ya Kaskazini, unaitwa "Arilang".

Muziki wa "Arilang" ulipopigwa ushangiliwa sana. Baada ya maonesho kumalizika mtunzi mmoja wa muziki wa Korea ya Kaskazini alisema,

"Nimefurahi sana kusikiliza muziki wa Kundi la Okestra la New York. Kila muziki ulipigwa kwa umahiri mkubwa, maonesho kweli ni mazuri."

Maonesho hayo yanafuatiliwa sana na vyombo vya habari vya Korea ya Kusini. Shirika la Habari la Korea ya Kusini tarehe 26 lilichapisha makala ya mhariri ikisema maonesho hayo ya kihistoria mjini Pyongyang yameionesha dunia kwamba Korea ya Kaskazini ina nia ya kuboresha uhusiano kati yake na Marekani, na vyombo vingine vya habari vinasema maonesho hayo yamedhihirisha kuwa "diplomasia ya kiutamaduni" ya Korea ya Kaskazini imezaa matunda, maingiliano ya kiutamaduni yanasaidia kuboresha uhusiano kati ya Korea ya Kaskazini na Marekani na kutatua suala la nyuklia la Peninsula ya Korea.

Kabla ya maonesho, mwongoza muziki wa kundi hilo pia alisema, ziara ya kundi la okestra la New York mjini Pyongyang ni hatua ndogo iliyopigwa katika maingiliano ya kiutamaduni kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini, ana matumaini kuwa kwaya na makundi ya opera ya Marekani pia yatafanya ziara mjini humo na kusukuma maingiliano hayo kweye mambo mengi zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-27