Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-28 15:46:25    
Maisha ya kijana wa India nchini China

cri

Kijana Chaudhari Dilip Giridhar kutoka India anapenda sana mji wa Taiyuan mkoani Shanxi, China. Katika miaka kadhaa iliyopita, sio tu kijana huyo aliwafundisha Kiingereza wanafunzi wa chuo kikuu cha huko, bali pia amejifunza Gongfu, na kuwa shabiki halisi wa Gongfu ya kichina. Alisema,

"Jina langu la Kichina ni Chen Ailong. Kwa kuwa Long yaani dragon inawakilisha utamaduni na sanaa ya China, pia inawakilisha mwana-gongfu ninayempenda Li Xiaolong (Bruce Lee). Napenda sana utamaduni wa China na Bw. Li Xiaolong, pia naipenda China, hivyo ninaitwa Ailong."

Kama walivyo wageni wengi, Bw. Ailong alianza kupenda utamaduni wa China kutokana na filamu za China. Mara moja Chen Ailong alitazama filamu iliyoigizwa na nyota wa Gongfu Li Xiaolong (Bruce lee), moyo wa ujasiri na haki pamoja na vitendo vilivyooneshwa na Bruce Lee katika filamu ile, vilimshangaza sana. Alisema,

"Nilitaka kuelewa utamaduni halisi wa China, na kujifunza Gongfu halisi ya kichina. Nilikuwa na ndoto ya kuja China siku moja. Hii ilikuwa ni ndoto yangu, kuja China na kujionea mwenyewe China halisi."

Mwaka 2002 barua ya mwaliko kutoka chuo kikuu cha ualimu cha Shanxi ilitimiza ndoto yake. Alikuja hapa China kuwa mwalimu wa Kiingereza. Kwa kuwa kabla ya kuja hapa China, Bw. Ailong alikuwa na ufahamu kidogo kuhusu historia na utamaduni wa jadi wa China kwa njia ya filamu tu, hivyo mara tu aliposhuka kwenye ndege na kuelekea nje ya uwanja wa kimataifa wa ndege wa Beijing alishangaa sana. Alisema,

"Mara ya kwanza nilipoondoka India na kuja nchini China, nilifikiri kuwa huenda nitaona majengo ya jadi, na watu waliovaa nguo za jadi, lakini baada ya kuja hapa Beijing, nilivyoona ni tofauti kabisa na niliyoona kwenye filamu. Mji huo ni wa kisasa, ni mji wa kimataifa. Sasa naona kuwa wazo langu la zamani ni la kuchekesha. "

Mwanzoni Ailong hakuzoea kuishi hapa China. Wiki ya kwanza baada ya kuja hapa China, Ailong aliumwa. Alipokuwa anataka kuondoka China, marafiki zake wa China walikwenda kumtazama, kuwasiliana naye, na kufuatilia maisha yake. Ili kujiunga na jamii ya hapa, Ailong alianza kujifunza lugha ya Kichina, kujaribu kuwasiliana na watu wengine, na kujifunza utamaduni wa kichina.

Ili kutimiza ndoto yake ya zamani, Ailong alitumia nafasi kujifunza kutoka kwa walimu, na ametembelea miji mingi ya China. Aliwahi kutembelea Hekalu la Shaolin kwenye misitu ya Milima Songshan mkoani Henan kujifunza Gongfu ya Shaolin, pia aliwahi kujifunza Wushu ya Taijiquan mjini Nanchang mkoani Jiangxi. Bw. Ailong pia aligundua uwezo wake na kujifunza Wushu, na alielewa hatua kwa hatua moyo wa Wushu ya kichina:

"Kujifunza Gongfu unaweza kunyamaza moyoni. Kujifunza Gongfu sio kwa ajili ya kupambana na mwingine, bali ni kwa ajili ya kuwalinda watu tunaowapenda. Gongfu inakufanya uwe mchamgamfu zaidi mwenye ari kubwa, huu ndio moyo wa Gongfu ninaoufahamu, nadhani huo pia unaonesha moyo wa Long."

Kadiri muda unavyopita, ndivyo kazi na maisha ya Bw. Chen Ailong nchini China pia yanaendelea vizuri. Mwaka 2006, katika mashindano ya ujuzi wa jadi ya China kwa wageni yaliyoandaliwa na kituo cha televisheni cha Beijing, Bw. Ailong kwa mara ya kwanza alipata mafanikio katika kipindi cha burudani cha televisheni, na mchezo wake wa Wushu unaoitwa "Wohucanglong" ulipewa tuzo ya nafasi ya tatu. Baadaye akajulikana kwa watazamaji wa China. Watu wamefahamu kuwa kijana huyo mgeni ni hodari kufanya maonesho. Nyimbo maarufu za India alizoimba kwa kutia madoido, ngoma na yoga za India alizocheza, pamoja na michezo ya Wushu ya jadi ya China ya upanga, Wushu ya Taijiquan na Zuiquan zilikuwa ni za kuvutia sana. Mtazamaji mmoja alisema,

"Nilifurahi nilipoona maonesho ya Bw. Ailong, furaha hiyo inatokana na upendo wa mgeni kwa Wushu ya China, na upendo wake kwa utamaduni wa China."

Bw. Chen Ailong alisema, China na India ni nchi jirani marafiki, na nchi hizo mbili zote ni nchi kubwa zinazoendelea. Katika zaidi ya miaka 60 iliyopita, daktari mpasuaji wa India Bw. Kotnis Dwarkanath Shantaram aliambatana na kikundi cha madaktari wa India kilikuja China kutoa msaada, kuwatibu watu waliojeruhiwa ili kuiunga mkono vita ya China dhidi ya Japan. Hadi leo, Bw. Kotnis Dwarkanath Shantaram bado ni shujaa mioyoni mwa watu wa India na China. Bw. Chen Ailong alisema, anataka kufanya shughuli kwa awezavyo kuhimiza urafiki wa India na China kama Bw. Kotnis Dwarkanath Shantaram. Alisema,

"Katika siku zijazo nataka kuanzisha kampuni inayoshughulikia mawasiliano ya utamaduni, sanaa na sayansi na teknolojia ya nchi hizo mbili. Nataka kuwa daraja la mawasiliano kati ya China na India, na kufanya shughuli za kuhimiza uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili, na kuwawezesha watu wa India waifahamu zaidi China. Nina matumaini kuwa wanafunzi wengi zaidi wa India watapata fursa ya kuja China kujifunza utamaduni na sanaa za China; na wanafunzi wa China wanaweza kwenda India kujifunza teknolojia ya mawasiliano ya habari, sayansi na teknolojia, hayo yatakuwa mawasiliano makubwa."

Bw. Chen Ailong ameishi na kufanya kazi nchini China kwa miaka mingi, na amekuwa na marafiki wengi wa China. Alisema,

"Sasa naona kuwa China ni kama taifa langu, naona ninaishi hapa kama naishi nyumbani. Hapa nina marafiki wengi wema, pia nina wanafunzi wengi. Nafurahi kuishi hapa."

Tuna matumaini kuwa, wageni wote wanaoishi hapa China kama Bw. Chen Ailong alivyo wataishi maisha kwa furaha.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-28