Chini ya uendeshaji wa katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan, serikali ya Kenya na chama cha upinzani vilifanya mazungumzo ya wiki kadhaa, tarehe 28 viliafikiana na kusaini makubaliano kuhusu kuunda serikali ya muungano. Saa 11 na dakika 10 ya jioni ya tarehe 28, rais Mwai Kibaki wa Kenya na kiongozi wa chama cha upinzani Raila Odinga walisaini makubaliano ya kuunda serikali ya muungano kwenye ikulu ya Kenya huko Nairobi huku wakishuhudiwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan, rais wa zamani wa Tanzania Bw. Benjamin Mkapa, na mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika ambaye ni rais wa Tanzania Bw. Jakaya Kikwete pamoja na waandishi wa habari wa Kenya na wa nchi mbalimbali duniani. Baadaye pande hizo mbili zilitoa hotuba kwenye sherehe ya kusaini makubaliano hayo, pande zote zimeahidi kutekeleza kithabiti makubaliano hayo. Rais Kibaki kwa niaba ya serikali ya Kenya alieleza nia ya kutekeleza kithabiti makubaliano hayo, akisema:
"Serikali ya Kenya itatekeleza kithabiti makubaliano hayo yaliyofikiwa kwenye mazungumzo, mpaka kupatikana kwa matokeo ambayo sote tunayatarajia. Kufikiwa kwa makubaliano hayo kutaiwezesha serikali na chama cha ODM vianzishe uhusiano wa kiwenzi kwa pande zote, kuanzishwa kwa uhusiano huo kutaiwezesha serikali yetu iweze kukabiliana na changamoto zinazoikabili katika kazi zote".
Bw. Raila Odinga kwa niaba ya chama cha upinzani ODM alieleza kuunga mkono makubaliano hayo akisema:
"Kusainiwa kwa makubaliano hayo kumefungua ukurasa mpya wa historia ya Kenya, kutokana na kusainiwa kwake, Kenya imeingia kwenye zama za ushirikiano kutoka zama za mapambano, sisi wa chama cha ODM tutafanya juhudi zote kuhakikisha makubaliano hayo yanaweza kutekelezwa kwa mafanikio".
Kuhusu mambo halisi yaliyowekwa kwenye makubaliano hayo, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alidokeza kwenye sherehe ya kusaini makubaliano kuwa, pande mbili zilizofanya mazungumzo zimekubaliana kuunda serikali ya muungano, na serikali hiyo itaweka nyadhifa za waziri mkuu na manaibu wake wawili. Bw. Kofi Annan alisema:
"Chama tawala cha Kenya na chama cha ODM vimefikia makubaliano kuhusu masuala makubwa kama yafuatayo: Pande mbili zimekubaliana kuwekwa kwa wadhifa wa waziri mkuu kwenye serikali ya muungano, waziri mkuu huyo ana majukumu ya kuratibu na kusimamia mambo ya serikali"
Bw. Annan alisema, kutokana na makubaliano hayo, kiongozi wa chama chenye viti vingi kwenye bunge au kiongozi wa shirikisho la vyama atakuwa waziri mkuu, na manaibu wawili wa waziri mkuu watateuliwa na vyama viwili vitakavyounda serikali ya muungano, kila chama kitamteua mmoja. Waziri mkuu na manaibu wake hawataweza kuondolewa madarakani ila tu katika hali ambayo kura za imani kwa serikali hazipitishwa kwenye bunge la taifa. Kutokana na hali ya hivi sasa, chama cha ODM kimekuwa ni chama kikubwa cha kwanza kwenye bunge, na kiongozi wake Bw. Raila Odinga hakika atakuwa waziri mkuu wa Kenya. Na mawaziri wa serikali ya muungano watateuliwa na vyama mbalimbali na kuamuliwa kutokana na kiasi cha viti vya kila chama kwenye bunge la taifa.
Bw. Kofi Annan alisema, kuanzia asubuhi ya siku ya pili yaani tarehe 29 Februari, mazungumzo kati ya serikali ya Kenya na chama cha upinzani yataingia kwenye kipindi cha mwisho, ambapo pande hizo mbili zitafanya majadiliano kuhusu utaratibu wa muda mrefu wa kukomesha msukosuko, pamoja na mgawanyo wa ardhi na raslimali.
|