Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-03 16:05:48    
Mwandishi wa hadithi za watoto Bw. Zheng Yuanjie

cri

Mwandishi wa hadithi za watoto Bw. Zheng Yuanjie anajulikana sana nchini China. Miaka 20 iliyopita alisawiri panya wawili waitwao Shuka na Beita kwenye hadithi aliyotunga inayoitwa "Hatari Zilizowakuta Shuka na Beita", panya hao wawili wanakumbukwa na kupendwa sana na wasomaji watoto hadi leo.

Bw. Zheng Yuanjie ana umri wa miaka 53, alianza kuandika hadithi za watoto mwishoni mwa miaka ya 70, mpaka sasa ametunga hadithi zenye maneno zaidi ya milioni 10. Mwaka 1985 alianzisha jarida lake "Msimulizi Mkuu wa Hadithi za Watoto". Hadithi zote kwenye jarida hilo alitunga yeye mwenyewe. Jarida hilo limekuwa linauzwa sana katika muda wa miaka yote 23 toka lilipoanzishwa, na nakala zake zilifikia zaidi ya milioni mia moja. Jarida hilo la kila mwezi linalouzwa sana kama hilo halipatikani duniani. Bw. Zheng Yuanjie alisema mafanikio hayo yanatokana na mafunzo kutoka kwa familia yake. Alisema,

"Mafanikio yangu yanahusiana na mafunzo niliyopata kutoka familia yangu. Mama yangu ni mtu mwenye tabia tofauti na wengine, na toka nilipokuwa mtoto alinifundisha niwe mtu kama yeye. Toka nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi, nilikuwa tofauti na watoto wenzangu ikiwa ni pamoja na insha zangu na jarida langu ambalo naliandikia hadithi peke yangu. Jarida kama hilo halikuwahi kutokea nchini China na hata nchi za nje katika historia."

Maisha aliyopitia Bw. Zheng Yuanjie hayakuwa ya kawaida. Alizaliwa katika familia ya ofisa wa jeshi mkoani Hebei, baadaye familia yake ilihamia Beijing, na alipata elimu ya shule ya msingi tu. Kutokana na kupenda ndege toka alipokuwa mtoto, alijiunga na jeshi la anga na kufanya kazi kwa miaka mitano. Alipokuwa jeshini alijiunga na mafunzo ya ufundi na kuhitimu mapema kwa nusu ya mwaka kutokana na matokeo mazuri na juhudi zake, na alipewa kazi ya kutunza ndege za jeshi. Baada ya kukamilisha lengo lake la kufanya kazi jeshini aliamua kuwa mfanyakazi wa kiwanda kimoja na kupewa kazi ya kutunza pampu ya maji, ni wakati huo ndipo alipoanza utunzi wake.

Mwishoni mwa miaka ya 70, China ilianza kutekeleza sera za mageuzi, mambo yote yalianza kustawi ikiwa ni pamoja na fasihi, wakati huo vijana wegni walianza kujihusisha na utunzi wa fasihi, mmoja wao ni Bw. Zheng Yuanjie. Baada ya kujaribu aina nyingi za fasini mwishowe alichagua kuandika hadithi za watoto. Alisema,

"Nina uhakika kuwa wengine hawawezi kunishinda katika utunzi wa hadithi za watoto. Elimu yangu ya msingi ilikuwa ni ya miaka minne tu, sikutumia muda mwingi kusoma shuleni, kwa hiyo muda wangu wa kuwaza mambo ulikuwa mwingi. Sikuona taabu ya kuandika hadithi, na mara nyingi hadithi zangu zilipata tuzo, kutokana na hayo najiamini zaidi, ninaandika mpaka sasa, na hadithi zangu zimekuwa na maneno zaidi ya milioni 10."

Hadithi za Zheng Yuanjie zilizo maarufu zaidi ni "Hadithi ya Pipilu", "Hadithi ya Luxixi" na "Hatari Zilizowakuta Shuka na Beika". Pipilu na Luxixi ni ndugu mapacha, walikuwa watukutu na wenye tamaa nyingi za kufahamu mambo. Marafiki wakubwa wa Pilipu na Luxixi ni panya Shuka na Beita, wanaongea kwa lugha ya binadamu, panya hao ni werevu, wenye hamu ya kujua mambo, ni jasiri na wenye roho nzuri. Panya Shuka aliendesha helikopta, panya Beika aliendesha kifaru, walikwenda kila mahali kupambana na uonevu na kuwasaidia watu wenye shida, hao ni panya wanaopendwa sana na wasomaji watoto.

Katika fasihi ya zamani ya China kuna panya wengi walioelezwa ndani ya hadithi, lakini panya hao wote ni wanyama wanaochukiza. Kwa mfano, katika riwaya maarufu ya "Safari ya Kwenda Magharibi" kuna panya aliyeiba mafuta ya kibatari ndani ya hekalu la dini ya Kibuddha, kisha akabadilika kuwa shetani wa kike duniani. Bw. Zheng Yuanjie anafuata kanuni ya kutofautiana na wengine aliamua kutunga hadithi ya panya anayependeza. Alisema,

"Nilipoandika hadithi hiyo nilifikiri kwamba hadithi za watoto nilizosoma hugawa watu wema na watu wabaya, watu wabaya hufananishwa na mbwa mwitu na panya, na watu wema hufananishwa na mbuzi, ng'ombe na farasi. Baada ya mimi kuwa maarufu kidogo kutokana na hadithi zangu, nilifikiri nibadilishe sura mbaya ya panya niliyopata nilipokuwa mtoto. Hadithi kuhusu panya ilikuwa fupi inaitwa "Rubani wa Helikopta Panya Mdogo". Mhariri mkuu wa gazeti moja alitokwa machozi baada ya kusoma hadithi yangu, na nilipata tuzo, niliambiwa niandike nyingine tena, basi nikaandika nyingine iitwayo "Askari wa Kifaru Beita", nikapata tuzo tena, baadaye niliweka wahusika hao wawili kwenye hadithi nyingine ya "Hatari Zilizowakuta Shuka na Beita".

Hadithi ya kwanza aliyoandika Bw. Zheng Yuanjie ni "Rubani wa Helikopta Panya Mdogo" ikieleza kuwa panya mdogo Shuka alikuwa mtoto wa kutaka starehe tu, na kila siku alimtaka mama yake ampikie chakula kitamu. Kwa mara ya kwanza mama yake alipomwongoza kwenda kutafuta chakula, ndipo alipofahamu kwamba kumbe maisha yao yanategemea wizi. Panya Shuka hakutaka kuwa mwizi aliondoka nyumbani kwa ndege yake ndogo. Njiani kila mnyama aliyemkuta alimwambia kwamba panya ni mnyama mbaya, Shuka alihuzunika sana lakini mwishowe amepata marafiki kutokana na kupenda kuwasaidia wengine.

Kuanzia mwaka 1982 Bw. Zheng Yuanjie aliandika hadithi ya "Shuka na Beita" kwa miaka 13. Katika muda huo maisha ya panya hao Shuka na Beita pia yanabadilika kutokana na mageuzi na maendeleo ya China.

Alipoandika hadithi ya "Shuka na Beita" pia aliandika hadithi nyingi nyingine za watoto. Hadithi zake zinatokana na uwezo wake mkubwa wa kufikiri. Ni nini kilichomdumishia msukumo mkubwa wa kuandika hadithi katika miongo kadhaa iliyopita? Alisema,

"Naona hata mtu akiwa mkubwa namna gani, kitu muhimu kwake ni kuwa na moyo wa kitoto yaani kupenda kudadisi mambo bila kuchoka, na kuwa na tabia ya kufikiri mambo mengine kutoka jambo moja."

Bw. Zheng Yuanjie ana tabia ya kuchunguza mambo, na anaweza kugundua kitu cha kuandikwa kutoka kwenye mambo ambayo ni ya kawaida kwa wengine. Anaona kuwa ufanisi hauwezi kukosa uwezo wa kufikiri. Na anamfundisha mtoto wake kwa njia ya kipekee, anampa mtoto wake nafasi nyingi za kuwa huru, ili mtoto aweze kuimarisha tabia yake mwenyewe. Hivi sasa mtoto wake amekuwa mtu mzima, amejiajiri kuanzisha "Shule ya Pipilu" kuwasaidia watoto namna ya kuandika makala ya fasihi. Bw. Zheng Yuanjie ni mwalimu mkuu wa shule hiyo. Wazazi wengi wanawapeleka watoto wao kwenye shule hiyo kutokana na umaarufu wa Bw. Zheng Yuanjie. Kwa kuwasiliana na wazazi na watoto Bw. Zhen Yuanjie amekuwa na msukumo mwingine, alisema mwaka huu wa panya wa China ataendelea kuandika hadithi za "Hatari Zilizowakuta Shuka na Beika" alizoacha kwa miaka mingi. Alisema,

"Katika kalenda ya kilimo ya China huu ni mwaka wa panya, nitaandika kitabu kingine cha hadithi mfululizo za "Shuka na Beita", maudhui ya kitabu hicho ni tofauti na mgogoro kati ya vizazi viwili, Shuka na Beita wanajitokeza kutatua mgogoro wao, ni kitabu cha kutoa mafunzo kwa familia."

Idhaa ya kiswahili 2008-03-03