Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-04 15:31:39    
Timu ya soka ya wanawake ya China yajipima kwa kupitia mashindano ya soka ya Asia Mashariki

cri
Mashindano ya pili ya soka ya Asia Mashariki yalifanyika mwezi Februari kwenye miji ya Chongqing na Yongchuan, kusini magharibi nchini China. Mashindano hayo yalizishirikisha timu nne zenye uwezo mkubwa duniani zikiwa ni pamoja na timu za Japan, Korea ya Kusini, Korea ya Kaskazini na China. Kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, timu ya soka ya wanawake ya China ilikuwa ina matumaini ya kujipima uwezo wake kwa kupitia mashindano yenye kiwango cha juu kama hayo, ili kupata maendeleo mapya.

Kwenye mashindano hayo, timu ya China iliifunga timu ya Korea ya Kusini kwa mabao matatu kwa mawili kwenye mechi ya kwanza iliyofanyika tarehe 18 mwezi Februari. Kwenye mechi hiyo, timu ya China ilidhibiti hali ya mchezo, lakini walipoteza fursa nyingi nzuri za kufunga magoli. Hata hivyo kocha mkuu wa timu ya China kutoka Ufaransa Bibi Elisabeth Loisel alisema:

"Ingawa washambuliaji wetu wengi walipoteza fursa kadhaa, lakini hali hii haikutokana na juhudi zao zisizo za kutosha au kukosa umakini. Mazoezi yetu ya siku za kawaida hufanyika kwa vipindi mbalimbali. Mara kwa mara yalifanyika kuanzia mazoezi ya ulinzi, halafu mazoezi ya ushirikiano katika sehemu za nyuma na katikati uwanjani, na mazoezi kuhusu kufunga magoli hufanyika katika kipindi cha mwisho. Nimepanga kutimiza malengo mbalimbali hatua kwa hatua, hivyo ni matumaini yangu kuwa watu wote wanaweza kuwapatia wanasoka mazingira mazuri ya kufanya mazoezi, na kuwatia moyo. Nina imani kubwa juu yao na kikundi cha makocha."

Bibi Elizabeth amekuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya wanawake ya China kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2007. Aliahidi kuisaidia timu ya China kupata medali kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing itakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu. Lakini katika miezi kadhaa iliyopita, mbinu zake kadhaa za ufundishaji ailitiwa shaka na baadhi ya wanasoka. Kwa mfano anabadilisha mara kwa mara idadi ya washambuliaji, na wachezaji wa kiungo. Watu wengi hawaelewi hatua hiyo ya Bibi Elizabeth. Kutokana na hali hiyo Bibi Elizabeth alieleza kuwa, hatua hiyo inalenga kuwasaidia wachezaji wazoee mikakati mbalimbali zinazotekelezwa uwanjani, na kuongeza uwezo wao wa kufanya ulinzi. Alisema:

"Nataka kutoa fursa nyingi zaidi kwa wanasoka ili wazoee mbinu nyingi zaidi. Tunapaswa kuwa na uvumilivu wa kutosha kutokana na makosa yanayotokea kwenye ushirikiano kati yao. Kwenye mazoezi hayo, pia tumegundua matatizo yaliyokuwepo kwenye hatua ya kufanya ushambuliaji na ufungaji. Hadi sasa kuna muda usiozidi miezi sita uliobaki kabla ya kufunguliwa kwa Michezo ya Olimpiki ya Beijing, kwenye mazoezi katika siku za baadaye nitachukua hatua za kuimarisha uwezo wao wa kufanya ulinzi."

Kwenye mashindano hayo ya Soka ya Asia Mashariki yaliyofanyika hivi karibuni, Bibi Elizabeth pia alibadilisha mbinu mbalimbali uwanjani. Je, wanasoka wa China wanachukua msimamo gani kutokana na hali hiyo? Mwanasoka wa katikati Zhang Na alisema atafanya juhudi za kuzoea mabadiliko hayo, na kuunga mkono mpango wa kocha mkuu, akisema:

"Kwa kweli mwanzoni sikuzoea mtindo huo wa kocha mkuu, lakini baada ya michezo mbalimbali, hivi sasa naona kuwa nimezoea zaidi. Tutafuata mbinu zitakazotekelezwa wakati wa michezo."

Mashindano ya soka ya Asia Mashariki ni mashindano makubwa ya kikanda, lakini kupata mafanikio kwenye mashindano hayo si lengo muhimu kwa timu ya soka ya China kushiriki kwenye mashindano hayo. Wakati wa kipindi muhimu cha kufanya maandalizi kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki, timu ya soka ya China inatumia fursa zote kugundua na kuondoa matatizo yaliyopo kwenye hatua yake ya kufanya maandalizi kwa kupitia michezo mbalimbali. Kocha mkuu Bibi Elizabeth pia ana matumaini ya kupima hali ya mazoezi na uwezo wa timu hiyo kwa kupitia mashindano kama hayo ya Asia Mashariki. Matokeo ya mashindano hayo yamethibitisha kuwa Bibi Elizabeth amepata mafanikio, na timu ya China pia ilijipatia uzoefu mzuri. Bibi Elizabeth alieleza kuwa timu ya China itakuwa na imani kubwa zaidi na kuwa na uzoefu zaidi kutokana na michezo mbalimbali.

Timu ya soka ya China iliwahi kupata medali ya fedha kwenye Michezo ya Olimpiki ya Atlanta ya mwaka 2006, hayo vilevile ni mafanikio makubwa zaidi iliyopata timu hiyo kwenye michezo hiyo. Ingawa timu hiyo haikupata matokeo yanayowafurahisha watu kwenye michezo mbalimbali iliyofanyika katika miaka ya hivi karibuni, lakini Bibi Elizabeth ana imani kubwa kuwa timu ya China itapata mafanikio makubwa kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Akizungumzia mashindano ya soka ya Asia Mashariki alisema:

"Nataka kusisitiza kuwa kiwango cha mchezo wa soka ya wanawake duniani kinapata maendeleo kwa kasi, timu zote zinafanya juhudi bila ya kusita, na kati ya timu zinazoshika nafasi 15 za mwanzo duniani kwenye Shirikisho la soka la kimataifa, hali ambayo timu moja kuishinda nyingine inawezekana kutokea. Hii ni hali nzuri kwa maendeleo ya mchezo wa soka wa wanawake, juhudi za timu zote zitahimiza kuinua kwa kiwango cha mchezo wa soka ya wanawake."

Hadi sasa zimebaki siku 160 kabla ya kufunguliwa kwa Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Katika kipindi kijacho, kila michezo ambayo timu ya China inashiriki, ni hatua ndogo kwake kuelekea kwenye jukwaa la Michezo ya Olimpiki. Endapo timu ya China itagundua matatizo yaliyopo kwa kupitia mashindano mbalimbali na kupata maendeleo mapya, kuna uwezekano kuwa wanasoka wa timu ya China wataonesha tabasamu la kuwafurahisha watu kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-04