Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-05 16:04:17    
Kijiji cha Yingpan cha kabila la Wabuyi

cri

Mnaosikia ni wimbo unaoimbwa na watu wa kabila la Wabuyi. Watu hao wanaishi kwenye kijiji cha Yingpan cha kitongoji cha Guiyang, mji mkuu wa mkoa wa Guizhou. Katika miaka kadhaa iliyopita, kutokana na maendeleo ya utalii kwa kutegemea raslimali ya historia na utamaduni, kijiji cha Yingpan kimekuwa kinaendelea kwa kasi, na maisha ya wanakijiji pia yameboreshwa sana.

Kijiji cha Yingpan ni kijiji cha kabila dogo, na asilimia 96 ya wakazi wake ni wa kabila la Wabuyi. Bw. Cen Desong mwenye umri wa miaka 40 ni mkuu wa kijiji hicho. Alisema alichaguliwa kuwa mkuu wa kijiji cha Yingpan mwaka 2002, wakati huo kijiji hicho kilikuwa kinakabiliwa na changamoto ya kuendeleza uchumi na kuongeza mapato ya wanakijiji. Alisema,

"Zamani pengo kati ya watu maskini na matajiri kwenye kijiji chetu lilikuwa kubwa, mazingira ya kimaumbile yalikuwa mabaya na maendeleo ya uchumi yalikuwa nyuma. Watu wachache walioendesha mikahawa na maduka walikuwa na mapato mazuri, ambapo watu wengine wengi waliokuwa wanajishughulisha na kilimo hawakuwa na mapato makubwa kutokana na upungufu wa mashamba."

Ili kubadilisha hali hiyo, Bw. Cen Desong aliamua kuvutia uwekezaji kutoka nje, na kutarajia kuwa makampuni kutoka sehemu za nje zitawasaidia wanakijiji wa Yingpan kuondoa umaskini. Lakini kijiji cha Yingpan kiko kwenye sehemu ya kuhifadhi maji ya mji wa Guiyang, serikali imeweka masharti magumu kwa makampuni na viwanda kuingia kwenye sehemu hiyo, na makampuni mengi yaliyopanga kuhamia kwenye kijiji cha Yingpan yalizuiwa na masharti hayo. Hali hiyo ilimlazimisha Bw. Cen Desong abadilishe mpango wake wa kuendeleza uchumi wa kijiji cha Yingpan. Alisema,

"Kijiji chetu kina ngome nyingi zilizojengwa wakati wa enzi ya Ming, pia kina utamaduni wenye umaalumu wa kabila la Wabuyi. Hivyo nafikiri kuwa tunaweza kuendeleza shughuli za utalii."

Miaka zaidi ya 600 iliyopita, kijiji cha Yingpan kilikuwa sehemu ya kuweka majeshi ya wafalme wa enzi ya Ming, na ngome nyingi zilijengwa kijijini. Watu wakisimama kwenye ngome iliyoko juu ya mlima, wanaweza kuona mandhari nzuri na kuhisi mapambano yaliyotokea katika karne kadhaa zilizopita. Kwa kutegemea mabaki ya kale na utamaduni unaovutia wa kabila la Wabuyi, Bw. Cen Desong aliongoza wanakijiji wenzake kuanzisha kampuni ya burudani ya ngome ya Yingpan. Bw. Cen Desong alikusanya pesa zaidi ya yuan milioni nane kutoka kwa makampuni na wanakijiji ili kukarabati ngome hizo, na pesa hizo zilibadilishwa kuwa hisa za kampuni hiyo.

Baada ya kuanzishwa kwa kampuni ya burudani ya ngome, shughuli za utalii za kijiji cha Yingpan zilistawi siku hadi siku. Kampuni hiyo inayoendelea vizuri imetoa nafasi za ajira kwa wanakijiji, hata wakulima kutoka vijiji vingine walikwenda kijiji hicho kufanya kazi za vibarua. Ili kuwawezesha wakulima hao watoe huduma nzuri kwa watalii, Bw. Cen Desong alichukua hatua mbalimbali, alisema,

"Tuliajiri walimu wa chuo cha utalii kuwafundisha wanakijiji wetu ujuzi kuhusu shughuli za utalii. Aidha ili kuonesha umaalumu wa kijeshi wa ngome za kijiji cha Yingpan, tuliwaalika wanajeshi kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wanakijiji."

Utalii kwenye ngome kwenye kijiji cha Yingpan unawavutia wakazi wengi wa mji wa Guiyang. Kwenye kijiji hicho watalii wanaweza kupanda milima, na kuona mabaki ya kale ya kijeshi. Baada ya kutembelea kwenye ngome, watalii wanaweza kwenda kwenye mikahawa rahisi ya wanakijiji wa Yingpan, na kuonja vyakula vya wakulima wa kabila la Wabuyi, huku wakijiburudisha kwa nyimbo na ngoma za kabila hilo. Shughuli za utalii wa kijiji cha Yingpan zinapamba moto mwaka hadi mwaka. Bw. Cen Desong alieleza kuwa ustawi wa shughuli za utalii zimeleta mabadiliko makubwa kwa kijiji hicho. Alisema,

"Tangu tuanzishe kampuni ya burudani ya ngome ya Yingpan, mali ya kijiji chetu imeongezeka kutoka yuan milioni 10 ya zamani hadi kufikia milioni 30. Maisha ya wanakijiji yameboreshwa sana, na mazingira ya kijiji chetu pia yameboreshwa."

Walipozungumzia mabadiliko ya kijijini kutokana na maendeleo ya shughuli za utalii, wanakijiji wa Yingpan walifurahi sana. walisema sasa barabara ya kwenda nje imejengwa, nyumba nzuri zimejengwa, na hata baadhi ya familia za kijiji hicho zimenunua magari. Mbali na hayo wanakijiji wanapata fursa nyingi zaidi kuwasiliana na watu wa nje, na wengi wao wanajua kutumia mtandao wa Internet.

Ingawa sasa kampuni ya burudani ya ngome ya Yingpan inaendelea vizuri, lakini Bw. Cen Desong anaona kuwa, kutokana na kutokuwa na uzoefu wa kuendesha kampuni, ni vigumu sana kwa kampuni ya Yingpan kupata maendeleo makubwa zaidi. Sasa ana matarajio kuwa kampuni ya kijiji cha Yingpan itaweza kushirikiana na kampuni ya kimataifa ya utalii, ili kupata vitega uchumi zaidi na mtizamo wa kisasa wa kuendesha kampuni, hivyo shughuli za utalii wa kijiji cha Yingpan zitaendelezwa zaidi, na maisha ya wanakijiji yataboreshwa zaidi. Alisema,

"Nina matumaini makubwa na mustakabali wa kampuni ya burudani ya ngome ya kijiji cha Yingpan. Siku zijazo tutafanya ushirikiano na kampuni moja ya kimataifa, ambayo itatuletea vitega uchumi na mbinu nzuri za kuendesha kampuni, ili tuendeleze zaidi shughuli za utalii kwenye kijiji chetu. Aidha tunafikiria kushirikiana na wafanyabishara wa nyumba, ili kujenga nyumba za kisasa kijijini."

Idhaa ya kiswahili 2008-03-05