Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-04 19:06:25    
Barua 0302

cri

Katika matangazo ya kipindi hiki cha tarehe24 mwezi huu, tulisema kuwa, siku hizi kutokana na vurugu zilizotokea nchini Kenya, mawasiliano yetu na wasikilizaji wetu wa Kenya yamepungua kiasi, hatujui kama hali ya vurugu, huenda iliathiri kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kazi ya posta. Kila siku tulikuwa na wasiwasi kuhusu amani na utulivu nchini Kenya na wasikilizaji wetu waliopo pote pale, tumefurahi kusikia kuwa serikali ya Kenya na chama cha upinzani zimefikia makubaliano ya kukomesha ghasia nchini humo, ni matumaini yetu kuwa kazi zote nchini humo zitarudishwa katika hali ya kawaida, mwanga wa matumaini unaonekana ni matumaini yetu kuwa shughuli zote zitarudi katika hali ya kawaida. Juzijuzi tulipata barua kutoka wasikilizaji wetu wa Kenya wakitueleza kuhusu hali hiyo.

Bw Philip M. Machuki wa sanduku la posta 646, Kisii Kenya Bw. Philip M. Machuki juzi juzi ametuletea barua pepe akisema, kwenye kipindi cha sanduku la barua cha tarehe 24 alisikia kuwa barua kutoka Kenya zimepungua, sababu moja inaeleweka vyema kuwa ni kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyosababisha hali hiyo, lakini pia Shirika la posta huko Kenya siku hizi pia linakataa bahasha ambazo zimelipiwa na Radio China Kimataifa. Lakini hata hivyo anasema yeye na wasikilizaji wengine wana furaha kwa kuwa wanazidi kuyapokea matangazo yetu siku hadi siku, na wanazidi kuyaenzi na kutushukuru kwa bidii zetu. Bwana Machuki pia anasema anapenda kutumia fursa hii kutupongeza kwa jinsi tulivyotangaza habari juu ya uchaguzi wa Kenya uliopita, na yale yote ambayo yametokana na matokeo ya huu uchaguzi wenyewe. Anaamini kuwa hali ya kawaida itarejea polepole na wanatarajia kuwa Kenya itakuwa na amani ya kudumu, anakamilisha kwa kusema Mungu ibariki Kenya Mungu ibariki CRI.

Na msikilizaji wetu Bw. Telly-Wambwa ametuandikia barua pepe akisema yeye anaendelea vizuri, na anashukuru kwa barua pepe tuliyomwandikia. Bw Wambwa anasema wao ni wazima na wana furaha kubwa, kwa sababu usuluhishi wa kisiasa kwenye mkutano wa kutafuta amani kati ya serikali na Chama cha upinzani ulioongozwa na Bw. Koffi Anani umefika mwisho kwa ufanisi mkubwa. Anasema sasa Kenya itakuwa na waziri mkuu, na hii inaonesha kuwa amani inayorejea nchini Kenya itaimarika. Anasema China na nchi nyinginezo zitanufaika kibiashara na utalii utafufuka.

Bwana Wambwa pia anasema atafuatilia kwa makini sana kupitia matangazo na kwenye tovuti kwenye mtandao internet, mikutano ya baraza la mashauriano ya kisiasa na Bunge la umma la China na kutuma maoni yake. Anafuatilia pia maandalizi ya michezo ya Olimpiki na anafurahi kuwasiliana nasi na kutarajia kutembelea Beijing wakati wa Michezo ya Olimpiki.

Na msikilizaji wetu Francis Njuguna wa Nairobi Kenya tarehe 28 Februari ametuletea barua pepe akisema, kwanza salamu nyingi kutoka Nairobi Kenya kwa watangazaji na watayarishaji wa vipindi wa Radio China Kimataifa, na pili anapenda kutupongeza kwa kazi ya kuandaa vipindi vyetu vinavyowapa wasikilizaji fursa ya kufahamu mengi kutoka mbali kwa njia iliyonyooka kabisa. Kwake yeye angependa uhusiano mwema kati ya China na Afrika uendelezwe vizuri siku hadi siku, anasema ni muhimu kwa kuwa wananchi katika bara hizi mbili watanufaika vilivyo. Anafahamu kwamba kuna baadhi ya watu ambao hawapendelei kuona jambo hili likifanikiwa. Ikumbukwe kwamba nchi ya China ni rafiki wa karibu sana kwa bara la Afrika, na urafiki huo upo kwenye mambo kadha wa kadha, ikumbukwe ya kwamba China haikushiriki kamwe katika kugawana bara la Afrika kama walivyofanya wakoloni. Ni swala la kusikitisha kuona na kusikia wengine wakilalamika urafiki kati ya China na Afrika, wanapoona urafiki huu unaimarika. Kila ikisikika kwenye vyombo vya habari kuwa China iko mbioni kustawisha uhusiano wa kibiashara, kijamii na kiuchumi na nchi za Afrika, wengine wanaanza kutilia mashaka, lakini ikumbukwe ya kwamba kuna usemi unaosema ya kwamba kelele za vyura hazimzuii ng'ombe kunywa maji.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu Philip Machuki, Telly Wambwa na Francis Njuguna kwa barua zao za kutuelezea hali ya nchini Kenya, tunafurahia habari kuhusu amani na utulivu nchini Kenya, ni matumaini yetu kuwa, hali ya kawaida itarudishwa nchini Kenya, na wananchi wa makabila mbalimbali wa Kenya wataishi katika hali ya maafikiano na masikilizano chini ya uongozi wa serikali ya muungano ya Kenya.