Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-11 14:58:39    
Madereva wa Taxi wa Beijing wafanya juhudi za kufanya maandalizi ili kutoa huduma bora wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing

cri
Wakati Michezo ya Olimpiki ya Beijing inapokaribia, watu wa sekta mbalimbali wanafanya juhudi kubwa kwa ajili ya maandalizi ya michezo hiyo, ikiwa ni pamoja na madereva wa taxi ambayo ni moja ya njia muhimu za mawasiliano kwa wakazi wa Beijing. Ili kuwakaribisha wageni kutoka nchi mbalimbali duniani wakati wa Michezo ya Olimpiki, madereva wa taxi wanafanya juhudi kubwa ili waweze kutoa huduma bora wakati wa michezo hiyo.

Watalii wakifika kwenye mji fulani, huwa wanakutana kwanza na madereva wa Taxi. Kutokana na hali hiyo, sura ya madereva wa taxi inaweza kuonesha kiwango cha maendeleo ya ustaarabu wa mji huo. Wakati Michezo ya Olimpiki ya Beijing inapokaribia, madereva wa taxi wa Beijing pia wanatoa mchango wao kwa kukaribisha michezo hiyo kwa hatua halisi. Dereva Wang Jiansheng kutoka Kampuni ya Taxi ya Kaskazini ya Beijing ni mmoja kati ya madereva hao.

Kwenye Taxi anayoendesha Bw Wang Jiansheng kuna nyota yenye pembe tano juu yake, na hii ni alama ya madereva bora mia moja waliochaguliwa mjini Beijing. Kabla ya kuwa dereva wa taxi, Bw. Wang Jiansheng alifanya kazi mbalimbali kwenye kiwanda kikubwa cha kiserikali, kiwanda cha kijiji na kampuni iliyowekezwa na wafanyabiashara kutoka nje. Baada ya kuchagua mara nyingi, Bw. Wang Jiansheng aliamua kujiunga na Kampuni ya Taxi ya Kaskazini ya Beijing na kuwa dereva wa taxi. Akizungumzia chaguo lake hilo, Bw. Wang Jiansheng alisema:

"Jambo muhimu zaidi kwa mtu ni kufanya kazi anayopenda. Napenda sana kazi hiyo. "

Ingawa kazi ya kila siku ni ngumu na ya uchovu kwa Bw. Wang Jiansheng, lakini anafurahia maisha hayo, kwani kazi hiyo inatoa fursa kwa yeye kujifunza zaidi ili aweze kutoa huduma kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki. Bw. Wang alisema:

"Kazi yangu inaniletea furaha kubwa. Gari langu ni kama chuo kikuu, ingawa ipo sehemu ndogo tu ndani yake, lakini linatoa huduma kwa watu mbalimbali kila siku, ama profesa au watu kutoka sehemu mbalimbali wanaofanya kazi za vibarua mjini Beijing. Watu hao wananifundisha mambo mbalimbali ambayo hayafundishwi shuleni, hali ambayo inanivutia sana."

Kwa mujibu wa Mpango wa maandalizi ya sifa ya madereva wa Taxi kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki", tangu mwaka 2005 shughuli mbalimbali zinazohusika zimefanyika, zikiwa ni pamoja na shughuli za kutoa mafunzo kwa madereva, tathmini ya imani ya watu wa jamii kwa kazi ya madereva, ushindani wa usalama wa uendeshaji wa taxi, kuondoa harufu mbaya na kupiga marufuku kuvuta sigara ndani ya taxi. Baada ya kufanyika kwa shughuli hizo, kiwango cha utoaji wa huduma za madereva wa Taxi kimeinuka kwa udhahiri. Aidha serikali ya Beijing inatoa mwito wa kuinua kiwango cha utoaji wa huduma kwa pande zote kwa madereva wa taxi kote mjini, ili kutoa huduma bora wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing.

Wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing, watalii na wageni wengi watatembelea mji wa Beijing au kutazama mashindano. Kutokana na hali hiyo, Bw. Wang Jiansheng anajifunza Kiingereza kwa bidii katika siku za mapumziko, ili kuongeza uwezo wake wa kuwasiliana na wageni, na kutoa huduma nzuri zaidi kwao. Bw. Wang Jiansheng alisema anajifunza Kiingereza kwa njia yake pekee, alisema:

"Nazungumza na wageni kwa Kiingereza mara kwa mara, ili kujiwekea mazingira mazuri ya lugha."

Safari moja, mgeni mzee alipanda taxi iliyoendeshwa na Bw. Wang Jiansheng kwenda kwenye Hoteli ya Jianguo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa, lakini ilikuwa vigumu kwake kutamka kwa kichina majina ya sehemu aliyotaka kwenda. Baada ya kutambua tatizo la mgeni huyo, Bw. Wang Jiansheng alizungumza na mgeni huyo kwa Kiingereza, hali ambayo ilimfurahisha sana abiria huyo. Usiku ule mgeni huyo alimpigia simu Bw. Wang Jiansheng kumtaka awapokee marafiki zake wawili kwenye Uwanja wa Ndege. Baada hapo Bw Wang Jiansheng alipata marafiki wengi wa kigeni kwa njia hiyo. Bw. Wang Jiansheng alisema:

"Natoa huduma nyingi zaidi kwa wageni kwa lugha ya kigeni niliyojifunza. Kwa upande mmoja naona fahari kuwa nimeonesha sura nzuri ya madereva wa taxi wa Beijing, kwa upande mwingine mapato yangu pia yanaongezeka. Shughuli za taxi ni njia nzuri kwa wageni kufahamu Beijing. Ili kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 na kuwahudumia vizuri wageni watakaokuja Beijing, kiwango cha lugha za kigeni cha madereva wa taxi kinapaswa kuinuka."

Nyuma kwenye taxi anayoendesha Bw. Wang Jiansheng, kuna karatasi nyingi ambazo zimeandikwa majina ya wageni, hao ni abiria waliopanda gari la Bw. Wang, na wengi kati yao wanapanda taxi hiyo mara kwa mara, na kuwa marafiki wa Bw. Wang Jiansheng, hayo yanatokana na uwezo wake wa kuongea lugha ya Kiingereza. Muda mfupi uliopita, kwenye Mashindano ya lugha ya Kiingereza" yaliyofanyika kwenye kampuni ya taxi ambayo Bw. Wang Jiansheng anayofanyia kazi, bw. Wang alitunga mpango kutokana na uzoefu wake, na kupewa tuzo ya nafasi ya pili.

Hivi sasa Michezo ya Olimpiki ya Beijing inakaribia, wageni wanaokuja Beijing wanaongezeka siku hadi siku, hali ambayo inamletea Bw. Wang Jiansheng fursa nyingi zaidi. Kutokana na uzoefu wake halisi, Bw. Wang Jiansheng amefahamu umuhimu mkubwa wa lugha ya Kiingereza katika utoaji wa huduma kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki. Alisema:

"Wageni wengi wana matarajio makubwa juu ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, na madereva wa taxi pia watakuwa na fursa nyingi zaidi kuwahudumia, hali ambayo inawataka madereva wawe na kiwango cha juu zaidi cha lugha za kigeni. Naona kuwa Kiingereza ni lugha muhimu kwa shughuli za taxi, ni matumaini yangu kuwa madereva wote wa taxi watafanya juhudi za kujifunza lugha ya Kiingereza."

Ingawa kazi ya madereva wa Taxi ni ya kawaida, lakini Bw. Wang Jiansheng na madereva wengine wengi kama yeye wanatoa mchango wao kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, na wataonesha ukarimu na urafiki wao kwa wageni wote watakaokuja Beijing kwa huduma zao bora.

Idhaa ya kiswahili 2009-03-11