Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-05 14:54:49    
Eneo la mafunzo ya ufundi wa kazi la mji wa Changzhou mkoani Jiangsu

cri

Kwenye kipindi cha leo, tanawaletea maelezo kuhusu eneo la mafunzo ya ufundi wa kazi la mji wa Changzhou mkoani Jiangsu linalojulikana kote duniani. Hivi sasa eneo hilo ambalo lina vyuo vingi vya mafunzo ya ufundi wa kazi, limekuwa kituo kinachojumuisha shughuli za elimu na utafiti pamoja na viwanda vinavyotumia teknolojia mpya katika uzalishaji, ili kutimiza mahitaji ya kudumu kwa wafanyakazi wenye ujuzi wa ufundi yanayotokana na ongezeko la kasi la uchumi.

Mji wa Changzhou ulioko kwenye sehemu ya delta ya mto Changjiang ambayo ni eneo muhimu la ongezeko la uchumi nchini China unakaribia miji iliyoendelea kiuchumi ya Shanghai, Nanjing na Suzhou, hali hiyo ya kijiografia imekuwa ya manufaa dhahiri kwa maendeleo ya mji huo. Mji wa Changzhou ulianza kujenga eneo la elimu na sayansi kuanzia mwaka 2002, na kulifanya liwe eneo la majaribio la mageuzi ya elimu ya ufundi wa kazi mkoani Jiangsu. Hivi sasa shule tano za ufundi zimejengwa kwenye eneo hilo, ambazo zinafundisha ufundi wa sekta mbalimbali zikiwemo teknolojia ya upashanaji habari, ufumaji na ushonaji na teknolojia za mashine na umeme. Mkurugenzi wa ofisi ya kamati ya usimamizi wa eneo hilo Bw. Lu Jinlin alisema, katika miaka mitano iliyopita sehemu hiyo imejengwa na kufikia eneo la mita za mraba milioni mbili, pia linaandikisha wanafunzi kutoka mikoa mingi kote nchini. Bw. Lu Jinlin alisema:

"shule tano za eneo hilo zinaandikisha wanafunzi kutoka kwenye mikoa 14 kote nchini, hivi sasa zina wanafunzi elfu 76, na zimekuwa sehemu kubwa ya elimu yenye vifaa na miundombinu kamili."

Bw. Lu Jinlin alisema, eneo hilo pia lina kituo cha viwanda vya kisasa, kituo cha usanifu na utengenezaji na maabara mbalimbali. Tofauti na shule za kawaida za ufundi wa kazi ni kuwa, shule hizo zimefanya raslimali zao ziweze kutumika kwa pamoja, ikiwemo miundombinu ya ufundishaji na vituo vya kufanyia mazoezi. Kwa njia hii si kama tu imepunguza matumizi ya raslimali ya ardhi, bali pia imeinua ufanisi wa matumizi ya vifaa. Bw. Lu Jinlin alisema:

"kituo cha viwanda vya kisasa kilijengwa kwa pamoja na mkoa wa Jiangsu na mji wa Changzhou, hivi sasa tumejenga vituo 13 vya kufanyia mazoezi. Kila mwaka wanafunzi elfu 40 hadi 50 wanaenda kwenye vituo hivyo kufanya mazoezi, vifaa na vituo hivyo vyote vinatumika kwa pamoja."

Katika eneo hilo kuna vituo vya kufanyia mazoezi ya teknolojia ya udhibiti wa kisasa, ufundi wa kukalibu na mashine zinazodhibitiwa kitarakimu. Vituo hivyo si kama tu vimepunguza gharama na kuinua ufanisi, bali pia vimeleta manufaa makubwa kwa wanafunzi, tofauti na vyuo vya kawaida, shule za ufundi zinatilia maanani kuinua uwezo wa wanafunzi kutenda kazi halisi na ufundi wa kazi fulani kwa njia ya kufanya mazoezi ya kazi hizo. Kwa kawaida walimu si kama tu watafundisha wanafunzi namna teknolojia fulani ilivyobuniwa, na zaidi ni kuwafahamisha namna ya kutumia teknolojia hiyo kwa urahisi, ufanisi na kisayansi?

Katika kituo cha mazoezi ya ufundi wa kazi ya kuunganisha vyuma kwa kuchomelea na kufanya upimaji, wanafunzi walikuwa wanafanya mazoezi kwa utaratibu katika karakana kubwa. Mwanafunzi wa darasa la ufundi wa kuchomolea Shi Jing aliyekuwa anafanya mazoezi alisema, alianza kufanya mazoezi katika kituo hicho kuanzia mwaka wa pili, na mazoezi hayo yanahusiana moja kwa moja na ufundi wa kazi watakazofanya katika siku za baadaye. Shi Jing alisema:

"ninatoka mji wa Huai'an mkoani Jiangsu, nilichagua masomo ya ufundi wa kuchomolea. Naona mpango wa masomo uliowekwa na shule ni mzuri sana, kwa kuwa unahusiana moja kwa moja na kazi nitakayoifanya baada ya kuhitimu. Sasa niko mwaka wa tatu, nitahitimu mwakani, jana nilisaini makubaliano ya ajira na kampuni moja."

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na marekebisho ya muundo wa uchumi wa China, shughuli za utengenezaji na utoaji huduma zimeendelea kwa kasi, makampuni yana mahitaji makubwa kuhusu wafanyakazi wenye ufundi wa kazi. Lakini kwa kuwa elimu ya ufundi wa kazi nchini China iko nyuma, bado haiwezi kukidhi mahitaji ya jamii. Hali hiyo imetoa fursa nzuri ya maendeleo kwa wanafunzi wa shule hizo za ufundi wa kazi.

Mkurugenzi wa ofisi ya kamati ya usimamizi wa eneo la elimu na sayansi la Changzhou Bw. Lu Jinlin alisema, kutokana na mpango mwafaka wa masomo na mbinu nzuri za ufundishaji, wanafunzi walioandaliwa katika shule tano za ufundi wa kazi za eneo hilo wanalingana na mahitaji ya makampuni, kiwango cha kupata ajira kwa wanafunzi wa shule hizo kinachukua nafasi za mbele mkoani Jiangsu. Bw. Lu Jinlin alisema:

"katika muda wa miaka minne iliyopita, wanafunzi wetu wote waliajiriwa, hata wanafunzi wa darasa la moja au pili wanatakiwa na makampuni."

Naibu mkurugenzi wa idara ya elimu ya mji wa Changzhou Bw. Hang Yongbao alisema, serikali ya Changzhou inatilia maanani maendeleo ya elimu ya ufundi wa kazi, hivi sasa mji huo una shule na vyuo 36 vya ufundi, serikali pia imeweka sera mbalimbali nafuu kwa shule hizo. Hivi sasa idadi ya wanafunzi wanaosoma katika shule za ufundi imezidi ile ya wanafunzi wanaosoma katika shule za sekondari ya juu. Bw. Hang Yongbao alisema:

"idadi ya wanafunzi wanaosoma katika shule za ufundi wa kazi mjini Changshu imezidi laki 1.8, na asilimia zaidi ya 96 ya wanafunzi hao watapata ajira. Tunashikilia kueneza elimu ya ufundi wa kazi katika jamii, tunazichukulia kazi za kuendeleza elimu hiyo kuwa shughuli moja muhimu katika mkakati watu wa kustawisha mji wa Changzhou kwa njia ya elimu na sayansi."