Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-06 15:58:24    
Wachimba makaa ya mawe wa China waelezea matarajio yao

cri

Karibu na mgodi wa makaa ya mawe ya Tunlan, Mama Chen Laying alikuwa anatumia kwa ustadi cherehani huku akisikiliza muziki. Kama hali ya kawaida, asubuhi ya siku moja mama huyo mwenye umri wa miaka 57 alikuwa anawasaidia wachimba makaa ya mawe kushona nguo zao chakavu bila malipo. Yeye amefanya shughuli hizo kwa miaka 24.

Mama Chen Laying alisema "Ninafika saa 1 hivi kila asubuhi, katika baadhi ya siku pia ninakuja adhuhuri. Kama nikiwa nyumbani wakati wa adhuhuri, huwa ninashona soksi kwa ajili ya wachimba makaa ya mawe."

Mume wa Bibi Chen Laying alikuwa mchimba makaa ya mawe kabla ya kustaafu kwake mwaka 1993, wakati ambapo mama huyo alikuwa ana wasiwasi na usalama wa mume wake, kiasi kwamba baadhi ya wakati alisindwa kupata usingizi. Mume wake alipostaafu, mtoto wake alianza kufanya kazi ya kuchimba makaa ya mawe. Lakini hivi sasa mama Chen Laying hana wasiwasi mkubwa kama ilivyokuwa hapo awali, kwani katika miaka ya hivi karibuni vifaa vya usalama kwenye mgodi huo viliboreshwa sana, jambo ambalo linaleta uhakikisha zaidi kwa usalama wa wachimba makaa ya mawe wanapofanya kazi chini ya ardhi.

Mchimba mwingine wa makaa ya mawe Bw. Fan Xiuhong mwenye umri wa miaka 47 amefanya kazi kwenye mgodi huo kwa miaka 19. Mwandishi wetu wa habari alimkuta kwenye bweni lililopo kando ya mgodi ambapo alikuwa anakula chakula cha mchana. Bw. Fan alieleza kuridhika na chakula cha bweni hilo. Yeye ni mkaguzi wa usalama wa mgodi huo, anashughulikia kukagua mambo ya usalama kabla ya wachimba makaa ya mawe hawajaingia mgodini. Bw. Fan Xiuhong alisema "Kabla ya wachimba makaa ya mawe kuingia mgodi, ninawakagua kama wanachukua moto au kama wamevaa nguo zinazotakiwa."

Ikilinganishwa na kazi ya wachimba makaa ya mawe, Bw. Fan Xiuhong anafanya kazi rahisi zaidi. Miaka 10 iliyopita ili kupata faida kubwa kabisa, migodi michache sana ya makaa ya mawe ilikubali kuwaajiri watu wanaoshughulikia kuwakagua wafanyakazi kuzingatia mambo ya usalama kabla ya wao kuingia mgodini. Lakini baada ya serikali ya China kuzidi kufuatilia usalama wa migodi, wakaguzi wenzake wa Bw. Fan Xiuhong wanaonekana katika migodi mbalimbali. Kiongozi wa mgodi huo wa Tunlan Bw. Tang Jiang alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kufanya kazi kwa kufuata utaratibu uliowekwa ni sharti la usalama wakati wa uzalishaji mali. Alisema "Katika miaka ya 50 na 60 ya karne iliyopita, wachimba makaa ya mawe waliweza kuingia kwenye mgodi kwa kutumia kamba moja tu, lakini hivi sasa hawawezi. Inapaswa wapata mafunzo ya lazima kabla ya kuanza kufanya kazi ya uchimbaji. Mafunzo hayo yanahusu ujuzi wa usalama na ufundi wa kuchimba makaa ya mawe. Baada ya mafunzo wanapimwa kwa mtihani, ni wale wanaofaulu mtihani tu ndio wanaoweza kupata hati na kuanza kazi. Na wafanyakazi wanaoshindwa mtihani wanazuiwa."

Mwandishi wetu wa habari alivaa kofia na kubadilisha nguo ya kufanya kazi, akishirikiana na wafanyakazi kuchukua taa na vifaa vya kujiokoa, waliingia kwenye mgodi ulio mita 200 chini ya ardhi baada ya kufanyiwa ukaguzi na mkaguzi wa usalama Bw. Fan Xiuhong. Njiani waliposafiri mgodini kwa kutumia gari maalumu, mwandishi wetu wa habari aliona vifaa mbalimbali vya usalama, vikiwemo mitambo ya kutoa gesi na vifaa vya usimamizi na kutoa tahadhari vinavyojiendesha.

Ni hali ya kawaida kwa watu kuwa na hofu ndani ya mgodi wa makaa ya mawe, lakini Bw. Jia Jincai mwenye umri wa 47 ni mfanyakazi mwenye uzoefu, alisema amezoea kazi hiyo. Hivi sasa mitambo inatumika sana katika kuchimba makaa ya mawe, na kazi nyingi ngumu zinafanywa na mitambo badala ya wachimba madini. Bw. Jia alisema  "Watu wengi wamepata picha kuwa kazi ya wachimba makaa ya mawe ni yenye hatari kubwa, lakini hivi sasa kazi hiyo si hatari kama watu wanavyoona. Kusema kweli hii ni kazi ngumu lakini si ya hatari sana."

Hivi sasa kazi ya kuchimba makaa ya mawe si kazi inayopuuzwa na watu. Mwaka 1999 mgodi huo wa Tunlan ulikuwa na kikundi cha kwanza cha wachimba makaa ya mawe ambao ni wahitimu wa vyuo vikuu vya madini. Na mapato ya wafanyakazi yameongezeka sana. Mwaka 2006 kwa wastani pato la kila mfanyakazi wa mgodi wa Tunlan lilikuwa Yuan elfu 30 hivi, huku pato la wastani la wafanyakazi wengine wa mjini wa huko lilikuwa Yuan elfu 10 na zaidi.

Kutokana na kuwepo kwa vumbi nyingi, wachimba makaa ya mawe wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya mapafu. Katika mgodi wa makaa ya mawe ya Tunlan, wafanyakazi waliougua magonjwa ya mapafu walikuwa wachache kuliko migodi mingine kwani vifaa vya kubadilisha hewa na kuondoa vumbi vimefungwa ndani ya mgodi. Bw. Jia alisema  "Utawala wa mgodi wetu na idara inayoshughulikia usimamizi wa migodi ya makaa ya mawe zinashikilia kutuandalia upimaji wa afya mara moja kila mwaka."

Kitu kinachowafurahisha sana wafanyakazi ni kuboreshwa kwa makazi yao. Zamani Bw. Jia na familia yake walikuwa wanaishi katika nyumba ndogo waliyojenga, mwaka 2000 walihamia kwenye nyumba ya kupanga kwa kodi ndogo iliyolipwa na mgodi. Hivi sasa ujenzi wa nyumba za ghorofa unaoongozwa na utawala wa mgodi unakaribia kukamilika, Bw. Jia ana mpango wa kununua nyumba mpya yenye eneo la mita zaidi ya 100. Alisema  "Zamani tuliishi ndani ya nyumba ndogo ya muda. Katika miaka ya hivi karibuni utawala wa mgodi ulijenga nyumba 10 za ghorofa, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hizo 10, wafanyakazi wote wa mgodi wetu wataweza kupata nyumba mpya."

Bw. Jia Jincai ana watoto wawili wenye umri wa miaka 20 hivi, ambao wanasoma kwenye shule ya ufundi ya makaa ya mawe. Baada ya kuhitimu kwao, vijana hao watafanya kazi ya kuchimba makaa ya mawe.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-06