|
Msemaji wa jumuiya ya nchi zinazotoa mafuta ya petroli duniani(OPEC), ambayo hivi sasa inafanya mkutano huko Vienna, Bw. Ibrahim Hussein, tarehe 5 alitangaza kuwa mkutano wa 148 wa mawaziri wa nchi za OPEC umeamua kudumisha kiwango cha utoaji mafuta cha hivi sasa. Hii ni mara ya pili kwa OPEC kuamua kudumisha kiwango cha utoaji wa mafuta ya petroli ili kukabiliana na shinikizo kutoka baadhi ya nchi ikiwemo Marekani baada ya mkutano wa mawaziri wa mwezi Februari.
Uamuzi huo wa OPEC kwa kiwango kikubwa unatokana na tatizo la uchumi wa Marekani. Bw. Hussein alisema, kupungua kwa kasi ya ongezeko la uchumi wa Marekani huenda kutasababisha kupungua kwa mahitaji ya mafuta ghafi kwenye soko la dunia. Mwenyekiti wa OPEC ambaye pia ni waziri wa nishati na madini wa Algeria, Bw. Chakib Khelil alisema wazi kuwa soko la mafuta duniani limeathirika kutokana na usimamizi usio mwafaka wa uchumi wa Marekani. Alisisitiza kuwa chanzo cha kupanda kwa bei ya mafuta hivi sasa ni mgogoro wa soko la fedha la Marekani, kupungua kwa thamani ya dola za kimarekani na migogoro ya kikanda, wala siyo upungufu wa mafuta masokoni. Alisema OPEC itaifuatilia sana hali ya soko la mafuta na kufanya uingiliaji mwafaka kabla ya kufanyika kwa mkutano wa mawaziri wa OPEC mwezi Septemba.
Mkutano wa mawaziri wa OPEC wa safari hii ulifanyika katika hali ambayo bei ya mafuta ya duniani inavunja rekodi mara kwa mara, na nchi za viwanda za magharibi ikiwemo Marekani zinataka kuongeza utoaji wa mafuta ili kuepusha uchumi wao kuathirika kutokana na bei kubwa ya mafuta. Tarehe 3, bei ya mafuta mepesi ya petroli kwenye soko la New York ilikaribia dola za kimarekani 104 kwa pipa. Hivyo rais George Bush wa Marekani alitoa wito wa kutaka kuongeza utoaji mafuta kabla ya kufanyika kwa mkutano wa OPEC. Rais Bush alisema, ni kosa kwa uchumi wa nchi zinazotumia mafuta kwa wingi kama Marekani kuathirika kutokana na bei kubwa ya mafuta. Serikali ya Marekani inaona, hali ya wasiwasi ya hivi sasa itapungua endapo OPEC itaongeza kidogo tu utoaji wa mafuta hadi kufikia mapipa laki 3 hadi 5 kwa siku. Nchi nyingine zilizotoa wito wa kutaka kuongeza utoaji wa mafuta ni Japan na nchi za Umoja wa Ulaya. Lakini nchi kubwa wanachama wa OPEC zinaona kuwa, hivi sasa kuna mafuta mengi kwenye soko la mafuta, tena hakuna haja ya kubadilisha kiwango cha utoaji mafuta, licha ya hayo kuna baadhi ya nchi wanachama ambazo zinataka kupunguza utoaji mafuta. Waziri wa mafuta na madini wa Saudi Arabia, ambayo ni nchi inayozalisha mafuta kwa wingi kabisa duniani Bw. Ali al-Naimi alisema, kwa jumla hali ya soko ni nzuri, biashara ya magendo ni chanzo kikubwa kinachosababisha kupanda kwa bei ya mafuta. Hivyo si ajabu kwa OPEC safari hii kufanya uamuzi wa kutobadilisha kiwango cha utoaji wa mafuta.
Wachambuzi wanasema, uamuzi huo wa OPEC ulifanywa baada ya kufikiria wasiwasi kuhusu matarajio ya mahitaji ya mafuta ya dunia na maslahi yake yenyewe. Kwanza, kutokana na mgogoro wa mikopo ya pili na mfumuko wa bei za vitu, ongezeko la uchumi wa Marekani limepungua kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo limezuia matumizi ya mafuta nchini Marekani. OPEC ina wasiwasi kuwa hali mbaya ya uchumi wa Marekani inaweza kuathiri uchumi wa dunia na kupunguza mahitaji ya mafuta ya duniani. Kutokana na athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa na akiba nyingi za mafuta ya kibiashara, OPEC inaona kuongeza utoaji wa mafuta kumekuwa ni jambo lisilo la maana.
Pili, kupungua kwa thamani ya dola za kimarekani, migogoro ya sehemu muhimu za utoaji mafuta duniani, biashara ya magendo na uwekezaji kuhusu mafuta yatakayotolewa hapo baadaye baada ya kuanguka kwa uwekezaji kwenye masoko ya hisa ya duniani, vimesababisha kupanda kwa mfululizo kwa bei ya mafuta.
Tatu, OPEC iliongeza utoaji mafuta hadi mapipa laki 5 katika mwezi Septemba mwaka jana, lakini hatua hiyo haikuwa ufanisi. Hivi sasa bei ya mafuta ya duniani imepanda hadi kufikia zaidi ya dola 100 kwa pipa, baada ya OPEC kutangaza kudumisha kiwango cha utoaji mafuta.
|