Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-06 20:24:47    
Mjumbe mpya wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China Bibi Fan Bingbing wa CRI

cri

Bibi Fan Bingbing ni mjumbe mpya kati ya wajumbe 2237 wa Baraza la awamu ya 11 ya mashauriano ya kisiasa la China. Yeye ni mtangazaji maarufu wa Idhaa ya Kirussia ya Radio China Kimataifa.

Leo tunawaelezea siku ya kwanza ya Bibi Fan Bingbing kuwa mjumbe mpya wa baraza hilo.

Tarehe 3 mwezi Machi ilikuwa ni siku ya ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Baraza la awamu ya 11 ya mashauriano ya kisiasa la China. Siku hiyo ilikuwa siku isiyo ya kawaida kwa Bibi Fan Bingbing. Ingawa mkutano huo ulifunguliwa siku hiyo alasiri, lakini yeye aliamka mapema sana asubuhi ya siku hiyo.

"Ninafurahi sana kuhudhuria mkutano huo, hivyo niliamka mapema ili kuzingatia vizuri zaidi masuala nitakayojadili kwenye mkutano."

Bibi Fan Bingbing anajulikana sana kwa wasilikizaji wa Russia wa Radio China Kimataifa. Ingawa yeye anakaribia umri wa miaka 60, lakini yeye bado ni mwenye nguvu na ari kubwa. Mwezi mmoja uliopita, yeye aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la awamu mpya ya 11 ya mashauriano ya kisiasa la China kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika jitihada za matangazo ya radio kwa nchi za nje.

Wengi kati ya wajumbe 2237 wanaohudhuria mkutano huo wameandaa miswada ya mapendekezo yanayohusu mambo ya siasa, uchumi, jamii, utamaduni, michezo na kadhalika. Na kila mswada wa pendekezo unaandaliwa baada ya kufanya utafiti wa uchunguzi kwa makini, ili pendekezo lenyewe liweze kuonesha maoni ya watu wengi.

Mapendekezo hayo yatajadiliwa kwenye mkutano unaofanyika katika siku hizi. Bibi Fan Bingbing anaona shinikizo kubwa. Ili kufanya maandalizi vizuri zaidi, yeye anakula chakula cha jioni haraka na kuwasiliana na wajumbe waliowahi kuhudhuria mkutano huo. Alisema:

"kwa sababu hii ni mara yangu ya kwanza kuhudhuria mkutano huo, ninapaswa kujifunza mambo mengi kutoka kwa wajumbe waliowahi kuhudhuria mkutano huo. Kuzungumza na wajumbe wengine hasa wajumbe waliowahi kuhudhuria mkutano huo kunanisaidia sana."

Saa tisa, mkutano wa kwanza wa Baraza la awamu ya 11 ya mashauriano ya kisiasa la China ulifunguliwa. Kabla ya hapo, Bibi Fan Bingbing alituambia kuwa, zamani yeye akiwa mwandishi wa habari alikaa kwenye ghorofa ya pili kutangaza moja kwa moja habari za mkutano au kukusanya habari. Leo anaweza kufuatiliwa na watu wengine kwenye ghorofa ya kwanza. Alisema:

"Niliposhiriki kwenye kazi ya idhaa yangu ya Kirussia ya kutangaza moja kwa moja kwenye mkutano wa Baraza, nilikuwa na wasiwasi, kwani nilitaka kutangaza vizuri, na leo nahudhuria Mkutano nikiwa mjumbe nina wasiwasi kwani nahofia kutoweza kutekeleza vizuri wajibu wangu wa mjumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa."

Mkutano wa siku hiyo ulifanyika kwa saa mbili, ambapo ulitoa majumisho ya kazi za Baraza hilo la awamu iliyopita na hali ya utekelezaji wa mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na wajumbe, na kutoa maagizo kuhusu kazi muhimu ya mwaka 2008. Baada ya mkutano huo, Bibi Fan alisema,

"mwanzoni nilifikiri kutoa pendekezo langu au la. Sikujua kama pendekezo langu ni mwafaka au la, na sikujua kama litapokelewa. Lakini baada ya kusikiliza ripoti ya mwenyekiti ya baraza hilo, nimeamua kutoa pendekezo langu. Mapendekezo mengi yaliyotolewa na wajumbe mbalimbali yanatiliwa maanani, kuungwa mkono na kushughulikiwa."

Katika miaka mitano iliyopita, asilimia 99 ya mapendekezo ya wajumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa la China yalipokelewa. Bibi Fan Bingbing anaona kuwa, kitendo hicho kinahimiza juhudi za wajumbe wa sekta mbalimbali kutoa maoni na mapendekezo kuhusu sera na hatua za serikali.