
Tukio la shambulizi la kigaidi lilitokea tarehe 6 usiku kwenye shule moja ya dini ya kiyahudi huko Jerusalem, na kusababisha vifo vya wanafunzi wanane na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa. Tukio hilo ni la shambulizi la kigaidi lililosababisha vifo na majeruhi ya watu wengi zaidi huko Jerusalem tokea mwaka 2004. Msemaji wa idara husika ya Israel alisema, tukio hilo lilitokea saa 2 na dakika 45 usiku wa siku hiyo, ambapo gaidi mmoja mwenye silaha aliingia kisiri kwenye shule moja ya dini ya kiyahudi iliyoko kaskazini mwa Jerusalem na kufyatua risasi ovyo, wanafunzi walioshtushwa walikimbia na kutawanyika. Baada ya dakika chache, watu wa idara ya usalama ya Israel walifika na kupambana vikali na magaidi, ambapo gaidi huyo alipigwa risasi papo hapo. Meya wa Jerusalem Bw. Uri Lupolianski siku hiyo alitoa hotuba kupitia kituo cha pili cha televisheni cha Israel alisema, usiku huo ulikuwa usiku wa kuhuzunisha kwa Jerusalem.
Tarehe 27 Februari Israel na jeshi la Palestina zilipambana kwenye ukanda wa Gaza na kusababisha hali wasiwasi kwenye sehemu hiyo, tokea hapo, idara ya usalama ya Israel haikuthubutu kufanya uzembe hata kidogo. Ili kukabiliana na matukio ya mabavu yanayoweza kutokea wakati wa ibada ya wikiendi huko Temple Mount, mji mkongwe wa Jerusalem, polisi wa Israel waliimarisha ulinzi kwenye sehemu hiyo. Hata hivyo ofisa wa polisi ya Jerusalem Bw. Aharon Franco alisema, kabla ya kutokea kwa tukio hilo huko Jerusalem, polisi takriban hawakupata habari za upelelezi za uhakika.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo, kundi moja linalojiita ni Batalioni ya kupigania uhuru ya Galilea, ya Imad Mughniyeh ilitoa taarifa kwa kupitia kituo cha televisheni ya Al Manar ambacho matangazo yake yanarushwa kwa kupitia satellite ya chama cha Hezbollah cha Lebanon, likitangaza kuwajibika na tukio hilo. Vyombo vya habari vya Israel vimesema, kundi hilo ni kundi la waarabu wa Israel, na limewahi kutangaza kuwajibika na matukio kadha wa kadha ya mashambulizi ya kigaidi yaliyowahi kutokea nchini Israel. Zaidi ya hayo, Kundi la upinzani la waislamu wa Palestina Hamas lilitoa taarifa huko Gaza, likipongeza tukio hilo na kusema huo ni mwanzo tu wa mashambulizi.

Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert alipopewa ripoti kuhusu tukio hilo mara aliwasiliana na waziri wa ulinzi Bw. Ehud Barak, na kujadili na mshauri wake pamoja na maofisa wengine wa usalama. Usiku huo Israel ilianza kuinua ngazi ya tahadhari ya mapambano dhidi ya ugaidi kote nchini, ili kuzuia shambulizi la kigaidi lisitokee tena. Kikosi ya walinzi wa mipaka cha Israel pia kimeimarisha ulinzi. Hatua hizo zinawafanya watu wawe na wasiwasi kuwa huenda zitaleta athari mbaya kwa mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel ambayo bado hayajarudishwa.
Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Israel Bw. Arye Mekl aliwaondoa watu wasiwasi na kusema, Israel haiwezi kuwaacha magaidi washinde katika jaribio lao la kuharibu amani, na mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yataendelea kufanyika. Tukio hilo limelaaniwa na jumuiya ya Kimataifa kwa kauli moja. Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas ametoa taarifa akilaani shughuli zote za wa kuwashambulia raia, bila kujali ni wapalestina na waisrael. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice alimpigia simu waziri wa mambo ya nje wa Israel Bw. Tzipi Livni akilaani tukio hilo kuwa ni kitendo kiovu cha kigaidi. Rais George Bush wa Marekani aliwasiliana na Bw. Olmert akisema, Marekani inasimama kidete kwenye upande wa Israel. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Bw. Davi Miliband alisema, njia pekee ya kuwakumbuka watu waliouawa katika tukio hilo ni kufanya chini juu kuhimiza mchakato wa amani.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon pia alitoa taarifa akieleza wasiwasi kuwa huenda tukio hilo likasababisha shughuli za mabavu kupamba moto.

|