Wapendwa wasikilizaji, maonesho ya kimataifa ya 78 ya magari ya Geneva yalifunguliwa tarehe 6 mwezi Machi. Katika maonesho ya safari hii ya siku 11, wafanyabiashara zaidi ya 260 kutoka nchi zaidi ya 30 wameshiriki maonesho hayo, na kuonesha teknolojia zao za kisasa pamoja na aina mpya za magari yao, kati ya magari yanayooneshwa kwenye maonesho ya Geneva kuna magari ya BYD na Brilliant ya China.
Maonesho ya magari ya Geneva yanafanyika mwezi Machi kila mwaka, na ni maonesho yanayofanyika mapema katika kila mwaka ikilinganishwa na maonesho mengine ya magari barani Ulaya. Hivyo maonesho ya magari ya Geneva huchukuliwa kuwa ni ishara ya mwelekeo wa hali ya masoko ya magari ya kimataifa, na pia ni mahali pazuri kabisa pa kuonesha aina mpya za magari yanayotaka kuingia kwenye soko la magari la Ulaya na masoko mengine ya magari ya duniani. Hadi kufikia mwaka jana, magari ya China yalianza kuonekana kwenye maonesho ya magari ya Geneva. Gari la Brilliant likiwa gari la kwanza la China linalooneshwa kwenye maonesho ya magari ya Geneva, lilikuwa moja ya vivutio vya maonesho ya magari ya Geneva. Kwenye maonesho ya magari ya Geneva ya mwaka huu, gari la BYD lenye teknolojia ya kisasa limeongeza nguvu za sekta ya magari ya China.
Kwenye sehemu inayoonesha magari ya Brilliant iliyoko kwenye ukumbi wa pili, balozi wa China aliyeko Uswisi Bw. Zhu Bangzao na mkewe walikuwa wanaangalia magari. Balozi Zhu alijaribu aina zote tatu za magari ya Zhonghua zinazoshiriki maonesho, tena aliyapapasapapasa na kusema,
"Magari mazuri! Mtu akikaa ndani anasikia raha! Endapo tunalinganisha magari ya bei moja, magari hayo ni mazuri kuliko baadhi ya magari ya Ulaya."
Maneno hayo ya balozi Zhu yaliungwa mkono mara moja na mkurugenzi wa wakala wa mauzo wa sehemu ya Ulaya Bw. Hans Ulrich Sachs akisema, ingawa magari ya Zhonghua yanayooneshwa kwa mara ya pili kwenye maonesho ya Geneva ni aina zile zile zilizooneshwa kwenye maonesho ya mwaka jana, lakini magari hayo ni bora sana kuliko yale ya zamani. Alisema,
"Ni kweli kwamba ubora wa magari ya Zhonghua unatakiwa kuwa salama au usanifu umeinuka sana. Wataalamu na mabingwa wa sekta hiyo wanasema, ubora wa magari ya Zhonghua umefikia kiwango cha magari ya Japan."
Mwaka jana magari ya Zhonghua yaliyoshiriki kwenye maonesho yaliuzwa kwenye masoko ya Ulaya baada ya maonesho kumalizika. Lakini matokeo ya majaribio ya kugonganisha magari ya Brilliant BS6 yalitia watu mashaka kuhusu usalama wa magari ya aina hiyo. Kuhusu suala hilo, Bw. Sachs alisema, upimaji husika uliofanyika hapo baadaye ulionesha kuwa magari ya Zhonghua yalifikia kiwango cha nyota 3 cha Ulaya. Yeye pia alieleza kinaganaga kuwa mauzo ya mwaka uliopita hayakuwa ya kuridhisha. Alisema,
"Mauzo ya magari ya Zhonghua ya kampuni yetu ya mwaka jana hayakutimiza lengo lililowekwa, lakini mwaka jana tuliimarisha ujenzi wa mfumo wa mauzo kwenye nchi za Ulaya, na tulijiandaa kwa mauzo ya mwaka unaofuata, mwaka huu tuna imani ya kutimiza lengo letu la mauzo."
Bw. Sachs pia alisema, maonesho ya magari ya Geneva ya mwaka huu yameonesha wazi mwelekeo wa maendeleo ya sekta ya magari katika siku za usoni. Akitoa mapendekezo kwa sekta ya magari ya China, alisema,
"Kuzalisha injini na magari yanayookoa nishati na kutumia aina mbili za nishati ni mwelekeo wa maendeleo ya sekta ya magari, viwanda vya magari vya China vingefuata mkondo huo."
Kwenye maonesho hayo ya mwaka huu, kampuni kubwa za Ulaya, Marekani na Japan zilionesha aina mpya za magari yanayotumia nishati mpya. Magari ya aina ya BYD ya China, ambayo yanachukua nafasi ya mbele katika teknolojia ya betri, yalifika kwa wakati. Magari ya China yaliyoshiriki kwenye maonesho ya magari ya Geneva yanafuatiliwa na kampuni nyingi za sekta ya magari, zinafuatilia sana mwelekeo wa maendeleo ya washindani wao.
|