Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-11 15:16:22    
Barua 0309

cri

Msikilizaji wetu Bw. Kaziro Dutwa ametuletea barua akisema kuwa, anafurahi sana kupata fursa hii tena kuweza kutuandikia waraka huu akiwa na matumaini makubwa kuwa sisi sote hatujambo na tunaendelea na majukumu yetu kama kawaida, kama ndivyo hivyo basi hii ni furaha kubwa sana kwake. Anasema hali yake ni njema wala tusimhofie bali anatuhofia sisi tu kwani tuko mbali sana naye, japo anaendelea kutusikia Radio China Kimataifa karibu kila siku jioni. Bw. Dutwa anasema, Mkutano wa Kimataifa kuhusu mazingira ulifanyika mwezi Desemba mwaka 2007 kwenye mji wa Bali nchini Indonesia, mkutano huo ulikuwa ni muhimu sana kwani uligusia uhai wa kila kiumbe hapa duniani; hali ya kuongezeka kwa joto duniani kila mwaka na athari zake mbalimbali kwa pande zote za dunia.

Anasema vimbunga, mafuriko, ukame na madhara mengine lukuki yasiyokoma ni matokeo ya kuongezeka kwa joto kwenye sayari yetu ya dunia, hakika watu wameanza kuzungumzia ongezeko hili tangu muda mrefu uliopita, lakini kutokana na viburi na tamaa zetu za kutaka maendeleo na kutaka kuishi kama tupo mbinguni vinachangia sana kuharibu utaratibu wa hali ya hewa japo nchi nyingi zinapuuza viashiria hivi ambavyo hivi sasa ni bayana kabisa! Nani hajashuhudia visiwa vingi vidogovidogo vikimezwa na maji? Nani hajashuhudia maji yanayozidi kuparamia kingo za pwani? Nani hajashuhudia barafu inayoyeyuka kwenye miamba ya barafu kwenye ncha za dunia za Arctic na Antarctica? Ncha hizi zinatumiwa na dunia yetu kama vipoza hewa, sasa barafu iliyoko huko ikiyeyuka yote dunia itapozwa na nini? Hivi ni viashiria vichache tu hakika vipo vingi sana mwenye macho haambiwi tazama!

Kabla ya Mkutano huo, watu wengi walikuwa wanajua kuwa China ndiye mchafuzi mkubwa wa hewa kuliko nchi zote, lakini baada ya Mkutano huu kuanza China ikatangazwa kuwa ni mtunzaji namba moja wa mazingira! Anasema japo mtunzaji namba moja ni Sweden bila shaka ukiangalia ukubwa na idadi ya wakazi, China inastahili kuwa ya kwanza pamoja na Sweden. Nchi kama Marekani imetajwa kuwa ni nchi inayoongoza kwa uzalishaji wa hewa chafu duniani, lakini imekataa kusaini "Mkataba wa Kyoto" kwa kuhofia athari za uchumi wao! Anauliza hivi uchumi na maisha kipi bora? Pamoja na uchanga wake wa uchumi, Dunia ya tatu imekubali kusaini mkataba wa Kyoto na kuuridhia, kwa nini nchi zenye nguvu kiuchumi hazitaki? China inastahili kupongezwa kwa juhudi hizi za makusudi na za kuigwa, kutoka nchi inayotoa hewa chafu kwa wingi hadi nchi inayopunguza utoaji wa hewa chafu, kwani hatari iliyo mbele ya dunia ni kubwa kuliko tunavyofikiria.

Tunamshukuru kwa dhati Bw. Kaziro Dutwa kwa barua yake inayoeleza mengi na vizuri kuhusu Mkutano wa uhifadhi wa mazingira na umuhimu wa kuhifadhi mazingira. Kweli maelezo kama hayo yanasaidia watu waongeze ufahamu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira. Kama kila mtu duniani anaweza kutoa mchango wake kwa uhifadhi wa mazingira ya asili, dunia yetu hii itakuwa na mazingira mazuri. Maoni yake pia yametuonesha ni jinsi gani Bw Dutwa anafuatilia matangazo yetu, na jinsi gani anaitakia mema dunia yetu kutokana na hali halisi inayotukabili sote. Tunakushukuru sana.

Msikilizaji wetu Jim Godfrey Mwanyama wa Klabu ya Mobile Fans Sanduku la Posta 1097 Wundati Taita, Kenya ametuletea barua akitoa salamu na pongezi nyingi kwa watangazaji na watayarishaji wa vipindi wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa kazi nzuri ya kutoa habari kemkem zinazoelimisha na kufundisha. Anasema anapenda kutoa wito kwa idhaa ya Kiswahili ya CRI kuendelea hivyo hivyo bila kuchoka, na yeye pamoja na wasikilizaji wengine wanaendelea kuitegea sikio Radio China Kimataifa kila wakati inapokuwa hewani. Anamalizia barua yake kwa kuwatakia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa heri na fanaka kwa kazi za kila siku.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Jim Godfrey Mwanyama kwa barua yake ya kututia moyo kuendelea na juhudi za kuwahudumia wasikilizaji wetu.

Na msikilizaji wetu Pius Bitamale wa S.LP 3030 Mwanza nchini Tanzania ametuletea barua akianza kwa salamu na kuwatakia kila la heri wafanyakazi na wasikilizaji wote wa Radio China Kimataifa, yeye ni mzima na anaendelea vizuri na shughuli zake za kila siku. Anasema lengo la barua yake ni kutoa shukrani zake kwa kukumbukwa na kutumiwa zawadi kutoka Radio China Kimataifa. Lakini poa anaomba afahamishwe kuhusu gharama ya radio ndogo ya mkononi aina ya Sony au Panasonic, ili ikiwezekana atume pesa, na Radio China Kimataifa imsaidie kununua kwani sehemu anapoishi hawezi kununua radio nzuri. Bw. Bitamale anaomba atumiwe Kalenda ya Radio China Kimataifa 2008, kadi za salamu, magazeti pamoja na picha za watangazaji wa Radio China Kimataifa, na mwisho anawatakia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa kazi njema na yenye mafanikio, na anaiombea Radio China Kimataifa iendelee kusikika vizuri.

Tunamshukuru sana Bw Bitamale kwa maoni yake na kwa maombi yake. Bila shaka tukiendelea na mawasiliano utatumiwa zawadi hizo, lakini kuhusu radio labda hiyo itakuwa ni ngumu kwetu, ni vigumu sana kwetu kuweza kutuma zawadi kama hiyo na kuwafikia wasikilizaji, kwani zinapita kwenye mikono mingi kwa hiyo uhakika wa kufika na usalama wake ni mdogo.

Msikilizaji wetu Boaz Tiko Omutoko wa Bonyore nchini Kenya anaanza barua yake kwa kuwasalimu wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio china Kimataifa akiwa na matumaini kuwa wote ni wazima, na yeye ni mzima kabisa kwa uwezo wa Mwenyezi wa Mungu.

Lengo la barua yake ni kutoa pongezi kwa Radio China Kimataifa kwa ushirikiano ilionao na KBC katika kufanikisha matangazo. Na pongezi zake pia kwa kuendelea vizuri na kituo cha FM jijini Nairobi. Bw. Boaz anatoa pongezi za dhati kwa Mkurugenzi mkuu wa Radio China Kimataifa bw. Wang Gengnian kwa bidii zake katika kazi, na kujitolea kufanya kazi yake kwa moyo mkunjufu na kwa bidii ili kuwafikishia matangazo wasikilizaji wa Radio China Kimataifa.

Msikilizaji wetu Magembe Jackson wa shule ya Sekondari Milambo, S.LP 356 Tabora Tanzania, anasema kwenye barua aliyotuandikia kuwa ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa hatujambo na tunaendelea vizuri, yeye pia ni mzima anatushukuru sana kwa barua tunazomwandikia, anazipata bila tatizo. Bw. Magembe anasema yeye ni mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya Milambo. Na anapenda kutupa mapendekezo yafuatayo, kwanza anaomba majibu yawe yanatumwa mapema, pia vipindi vya Radio China Kimataifa viongelee mambo kwa kirefu sana kwani vinapoongelea masuala machache huwa vinawaacha wasikilizaji wakiwa na hamu ya kuendelea kusikiliza, jambo lingine ni kwamba anaomba Radio China Kimataifa iboreshe matangazo yake kwa kuwa na vituo vingine vya masafa ya FM, maana ni radio chache sana ambazo zinasikika katika masafa mafupi hivyo inakuwa shida kwa baadhi ya wasikilizaji. Vipindi anavyovipenda ni pamoja na vile vinavyohusu uchumi wa China, mazingira ya China, utamaduni na vingine kadhaa, pia anaomba apewe ratiba kamili ya vipindi kwani kwa sasa anabahatisha tu kusikiliza.

Na msikilizaji wetu Benson Mbigura wa S.L.P 137-50100 Kakamega nchi Kenya ametuletea barua akitoa salamu nyingi kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, na anatoa shukrani za dhati kwa Radio China Kimataifa kwa sababu imekuwa inawatambua wasikilizaji wake wote bila kuwabagua, watoto, wakubwa, maskini na matajiri, anafurahishwa sana jinsi Radio China Kimataifa inavyoeneza habari kila kona dunia. Bw. Benson pia anatoa pongezi kwa Radio China Kimataifa kwa kuwatambua wasikilizaji wenzao na kuwapa nafasi ya kutembelea China, na kupata nafasi ya kujionea mambo mengi waliyokuwa wanasikiliza kupitia matangazo. Na sasa anapenda kuitaarifu Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kuwa hata yeye sasa anapenda kutunikiwa nafasi ya kutembelea China, ili aweze kujionea Ukuta Mkuu wa Beijing, ambao ni ukuta wa kihistoria. Anaomba pia wafanyakazi wa Radio china Kimataifa wakitembelea Kenya wawaite wasikilizaji ili waweze kujumuika pamoja nao, na hiyo itawasaidia wao kuweza kufika nchini China na kujionea wenyewe vivutio vya utalii.

Tunawashukuru msikilizaji wetu Boaz Tiko Omutoko, Magembe Jackson na Benson Mbigura kwa barua zao za kupongeza kazi tunayofanya sisi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, tarehe 28 Februali ilikuwa siku ya kuadhimisha miaka miwili tangu Kituo cha matangazo ya CRI kwenye mawimbi ya FM kianzishwe huko Nairobi Kenya, barua za msikilizaji wetu ni kama uungaji mkono kwa sisi, tutaendelea na juhudi kuandaa vipindi vizuri ya kuwafurahisha wasikilizaji wetu.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-11