Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-12 19:12:23    
China yatumia fursa ya michezo ya Olimpiki kusukuma mbele udhibiti wa uvutaji sigara

cri

Kama tunavyojua uvutaji sigara unaleta madhara makubwa kwa afya ya binadamu, nchini China kila mwaka watu watapao milioni moja wanakufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na uvutaji wa sigara. Ili kuweka mazingira mazuri ya kijamii yanayosaidia kupiga marufuku uvutaji sigara, serikali ya Beijing hivi karibuni imeweka kanuni na kuagiza kwa mara ya kwanza kupiga marufuku uvutaji sigara katika sehemu za umma zikiwemo mikahawa, hoteli na vituo vya mafunzo, kanuni hizo zinafuatiliwa sana katika jamii.

"nachukia sana akivuta sigara, siwezi kumzuia kwa hiyo namkwepa. Akivuta sigara, namkwepa, nafungua madirisha."

Mliyemsikia ni Bi. Sun Xiaoli anayeishi kwenye jumuiya ya makazi ya Wangjing mjini Beijing akilalamika kuhusu mume wake kuvuta sigara. Mume wake Bw. Li Jianhua amevuta sigara kwa muda zaidi ya miaka 30, tabia hiyo imekuwa sehemu ya maisha yake. Bi. Sun alisema, kila mara akimshawishi aache kuvuta sigara, anatafuta visingizio kadhaa wa kadhaa. Bw. Li Jianhua alisema:

"wakati wa furaha au wasiwasi, wageni wengi wakija au nikiwa kwenye tafrija, mambo yote hayo yanaweza kusababisha uvutaji sigara."

Hivi karibuni, kanuni mpya kuhusu kupiga marufuku uvutaji sigara katika sehemu za umma mjini Beijing imetangazwa kwenye tovuti husika ya serikali ya Beijing kwenye mtandao wa Internet. Kanuni hizo zimepanua sehemu zinazopiga marufuku uvutaji wa sigara, na kwa mara ya kwanza inaagiza kupiga marufuku uvutaji sigara ndani na nje ya sehemu za umma ikiwemo mikahawa na hoteli. Kanuni hizo pia zinaagiza kuwa kama wakazi wakivuta sigara kwenye sehemu hizo, watapigwa faini isiyozidi Yuan 50.

Habari zinasema kanuni hizo zitaanza kutekelezwa mwishoni mwa mwezi Mei. Kidhahiri idara ya afya ya Beijing inataka kutumia fursa ya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 kusukuma mbele kazi ya kupiga marufuku uvutaji sigara.

Kanuni hizo mpya zimefuatiliwa na wakazi wa Beijing, watu wengi wanaiunga mkono na kuona kuwa kupiga marufuku uvutaji sigara ni vizuri kwa afya ya watu, pia kutasadia kuweka mazingira mazuri ya kijamii kwa michezo ya Olimpiki. Bi. Sun pia ni mmoja wa waungaji mkono wa kanuni hiyo. Bi. Sun alisema,

"naunga mkono kabisa kanuni hizo, bila kujali kwenye sehemu za umma au ndani ya nyumba, uvutaji sigara unaleta madhara kwa jamaa na marafiki yako, hivyo haupaswi kutenda jambo hilo linalodhuru afya yako mwenyewe na ya watu wengine."

Wataalamu wanasema kuwa moshi unaotolewa wakati wa kuvuta sigara una vitu zaidi ya 40 vinavyoweza kusababisha ugonjwa wa saratani, pamoja na vitu zaidi ya 10 vinavyohimiza maendeleo ya ugonjwa huo, vitu vinavyoleta madhara makubwa zaidi katika moshi wa sigara ni nicotine na carbon monoxide. Kiasi cha Nicotine kilichomo kwenye sigara moja kinatosha kuua panya mmoja, lakini jambo baya zaidi ni kwamba madhara yanayosababishwa kwa watu wengine huenda ni zaidi ya inavyodhaniwa. Utafiti husika umeonesha kuwa uvutaji sigara unaleta madhara makubwa zaidi kwa wavutaji wenyewe kuliko kwa watu walioko karibu nao. Mtaalamu wa idara ya kusaidia wagonjwa waache kuvuta sigara katika hospitali ya urafiki wa China na Japan ya Beijing Bi. Yu Hongxia alisema, nchini China watu zaidi ya laki moja wanakufa kutokana na uvutaji usio wa moja kwa moja, watoto na wanawake ndio wanaoathiriwa zaidi. Bi. Yu Hongxia alisema:

"watoto hawana ufahamu kuhusu uvutaji usio wa moja kwa moja, tena ni rahisi zaidi kwa mapafu na njia ya kupumua ya watoto kupatwa na magonjwa, hivyo kuna hatari kubwa zaidi kwa watoto kupatwa na magonjwa ya njia ya kupumua na pumu, hali hiyo hutokea kwa wanawake. Uwezekano wa kupatwa saratani ya mapafu kwa watu walioathiriwa na uvutaji usio moja kwa moja ni mkubwa zaidi kuliko kwa wavutaji sigara wenyewe."

Imefahamika kuwa madhara ya tumbaku ni moja kati ya matatizo makubwa kabisa ya afya ya umma duniani. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani WHO, watu wapatao bilioni 1.3 duniani wanavuta sigara, na kila mwaka watu milioni 5 wanakufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na uvutaji sigara. Ripoti kuhusu afya duniani kwa mwaka 2002 inasema, kama vitendo vya uvutaji sigara havitadhibitiwa, ifikapo mwaka 2020, watu milioni 9 watakufa kutokana na tabia hiyo kila mwaka.

Huu ni mwaka wa tatu tangu mkataba wa udhibiti wa tumbaku uanze kutekelezwa nchini China, kuimarisha utekelezaji wa mkataba huo na ujenzi wa mtandao wa kudhibiti tumbaku ni kazi muhimu ya kudhibiti uvutaji sigara nchini China mwaka huu. Naibu mkurugenzi wa ofisi wa udhibiti wa uvutaji tumbaku katika taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya China Bi. Jiang Yuan alisema, China imejenga utaratibu kamili wa utekelezaji wa mkataba huo na kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha mkataba huo unafanya kazi kwa ufanisi. Bi. Jiang Yuan anaona kuwa toka kanuni mpya ya kupiga marufuku uvutaji sigara ianze kutelekezwa mjini Beijing, idadi ya watu wanaovuta sigara kwenye sehemu za umma itapungua siku hadi siku, na idadi ya wavuta sigara mjini Beijing pia itazidi kupungua.

Baada ya siku mia moja hivi, michezo ya 29 ya Olimpiki itaanza kufanyika mjini Beijing, serikali ya China imetoa ahadi ya kuandaa michezo ya Olimpiki isiyo na uvutaji sigara kwa kamati ya Olimpiki ya kimataifa, na pia inafanya harakati za kupiga marufuku uvutaji sigara katika miji husika inayoandaa michezo hiyo.