Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-13 15:37:17    
Masuala yanayohusu maisha ya wananchi yafuatiliwa zaidi

cri

Bi. Wei Wei mwenye umri wa miaka 60 anatoka chama cha umoja wa demokrasia cha China, tawi la mkoa wa Shanxi. Yeye amekuwa mjumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China kwa awamu tatu za mfululizo. Tangu mwaka 1998 mjumbe huyo amekuwa anakuja Beijing kila mwezi wa Machi, kuhudhuria mkutano wa mwaka wa baraza hilo, na kutekeleza wajibu wake wa kutoa maoni na mapendekezo kuhusu sera na hatua za serikali. Bi. Wei Wei alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, alisema

"Miaka 10 iliyopita nilipoteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa mjumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa la taifa la China, nilifurahi sana. Lakini hivi sasa furaha hiyo imepungua sana, badala yake ninatafakari kwa makini na kwa kina zaidi, kwani ninafahamu wajibu ninaobeba."

Mahojiano hayo na Bi. Wei Wei yalifanyika wakati alipokuwa anapata kifungua kinywa, kwani anapaswa kuwa na muda ili kupitia tena hotuba atakayoitoa kwenye kikao cha kundi lake kilichotakiwa kufanyika siku hiyo hiyo, na kuangalia tena mapendekezo atakayowasilisha kwenye sekretarieti ya mkutano. Alisema "Kufanya maandalizi kabla ya utekelezaji, hii ni tabia yangu katika miaka 10 iliyopita tangu nianze kutekeleza wajibu wa kushiriki na kutoa maoni na mapendekezo kuhusu sera na hatua za serikali. Hebu tuzungumze huku tukiwa tunapata chakula, hii inasaidia kutumia muda ipasavyo."

Kutoa mapendekezo kwa serikali kuu ya China ni njia muhimu ya wajumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la taifa la China kutekeleza wajibu wa kutoa maoni kuhusu sera na hatua za serikali kuu. Katika miaka 10 iliyopita, kila mwaka kwa wastani Bi. Wei Wei alitoa mapendekezo matano. Na mwaka huu ameandaa mapendekezo kumi, ambayo yanahusu kuanzisha mfumo wa pamoja wa kuhesabu gharama za matibabu kote nchini, kuhifadhi mazingira kwenye maeneo ambayo mifereji ya mradi wa kupeleka maji ya sehemu ya Kusini hadi sehemu ya Kaskazini inapita, kuondokana na umaskini katika miji na wilaya za sehemu ya Magharibi na jinsi ya kusaidia maendeleo ya vyuo vikuu vya binafsi mkoani Shanxi. Masuala yaliyomo kwenye mapendekezo hayo yote yanahusiana kwa karibu na maisha ya watu wa kawaida.

Takwimu zinaonesha kuwa, katika miaka mitano iliyopita wajumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la taifa la China waliwasilisha mapendekezo zaidi ya elfu 20, na asilimia 99 ya mapendekezo hayo yalikubaliwa au kutekelezwa.

Bi. Wei Wei alisema kinachomfurahisha zaidi ni kutoa mapendekezo kabla ya serikali kufanya uamuzi, na kuwasaidia watu wa kawaida kuondoa kero zilizowasumbua. Alitoa mfano wa shughuli za ukarabati wa kijiji kiitwacho Jiuzhaizi. Kijiji hicho chenye familia 230 kipo mjini Xi'an, mkoani Shanxi. Wanakijiji walikuwa wanasumbuliwa na tatizo la umeme kutokana na zana kongwe za umeme. Mwanakijiji Fang Hongsheng alisema

"Kwa miaka mingi ilikuwa nyanya za umeme zinatandikwa ovyo, hali ambayo iliharibu mitambo mingi umeme na umeme kukatika kwa siku 3, 4 kila wiki. Iliponyesha mvua au kuwepo kwa upepo mkubwa, kwa uhakika umeme ulikuwa umekatika."

Wanakijiji wengi ni maseremala. Kutakika kwa umeme si kama tu kuliwasumbua sana kimaisha, bali pia kuliharibu shughuli zao. Mwanzoni mwa mwaka 2004, kwa kupitia gazeti moja la huko, Bw. Fang Hongsheng alimfikishia Bi Wei Wei ujumbe kuhusu matakwa ya kuboresha vifaa vya umeme vya kijiji hicho. Bi. Wei Wei alitembelea kijiji hicho, ambapo alijionea kuwa mbali na tatizo la umeme, njia ya huko ilikuwa mbaya na kulikuwa hakuna huduma ya maji safi, wanakijiji walipaswa kuchimba visima wao wenyewe. Mjumbe huyo alisema  "Siku zote kijiji hicho kilikuwa kinakabiliwa na matatizo sugu ya barabara, umeme na maji. Tangu mwaka 2004 nilitoa mapendekezo kadhaa kuhusu kero hizo zinazokikabili kijiji hicho, niliwasilisha mapendekezo hayo kwenye mikutano ya Baraza la mashauriano ya kisiasa la taifa na la mkoa."

Zaidi ya hayo baada ya ziara ya ukaguzi, Bi. Wei Wei aliona kuwa matatizo yaliyotokea kwenye kijiji cha Jiuzhaizi pia yapo kwenye vijiji vingine vya mikoa mingine nchini China. Mwaka 2005 kwenye mkutano wa mwaka wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la taifa, aliwasilisha pendekezo kuhusu kuboresha nyaya za umeme za vijijini. Na alipata majibu kwa haraka. Bi. Wei Wei alisema "Serikali ya mji wa Xi'an ililiomba baraza la mashauriano ya kisiasa la mji huo lishughulikie jambo hili, kwa hiyo nilipata mwaliko wa kushiriki kwenye mchakato mzima kwani ni mimi niliyetoa pendekezo hilo. Tulishirikiana na idara husika za mji wa Xi'an, zikiwemo idara ya kilimo, idara ya mawasiliano na idara ya umeme, tulitembelea kijiji hicho kwa pamoja."

Baada ya kufanya ukaguzi, serikali ya mji wa Xi'an ilitoa jibu la maandishi kwa pendekezo hilo, ikiahidi kutenga fedha mwezi wa Aprili mwaka huo huo katika mradi wa ukarabati wa huduma za maji, umeme na barabara kwenye kijiji cha Jiuzhaizi. Hivi sasa familia zote za kijiji hicho zimebadilishiwa mita mpya za umeme na zinapata huduma za uhakika za umeme bila kuathirika na mvua au upepo. Mwanakijiji Fang Hongsheng alisema "Baada ya nyaya za umeme kufanyiwa ukarabati, hivi sasa tuna taa zinazong'aa, barabara pana, na tunapata huduma ya maji safi. Tunafurahi kweli."

Kuwa mjumbe wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China ni wajibu mkubwa na kazi ngumu. Hata hivyo Bi. Wei Wei alisema anapenda kutoa mchango mkubwa zaidi katika kuwasilisha maoni ya watu wa kawaida na kuisaidia serikali katika jitihada za kuondoa kero za wananchi.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-13