Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-17 15:41:34    
Michezo ya sanaa ya Quyi yastawishwa mjini Tianjin, China

cri

Quyi ni jina la michezo ya sanaa zinazoeleza mambo kwa kuongea au kuimba, ni aina ya michezo ya sanaa iliyopatikana kutoka fasihi simulizi na kueleza mambo kwa kuimba baada ya mabadiliko ya muda mrefu. Mji wa Tianjin ni chimbuko la Quyi nchini China, na kwa kiasi kikubwa inastawisha maisha ya watu kiutamaduni.

Mjini Tianjin kuna mazingira mazuri ya Quyi, na hasa kwenye mikahawa ya chai, wakazi hupitisha muda wa mapumziko ndani ya mikahawa na kusikiliza ngonjera ya vichekesho, namna ya kuishi hivyo kumekuwa ni namna ya maisha yao ya kisasa. Kwenye jukwaa wasanii wawili wa ngonjera wanavaa joho na kipepeo au kuwa na leso mkononi, wanapozungumza watazamaji wanapiga makofi na kucheka. Msikilizaji Bw. Ding alisema,

"Mji wa Tianjin ni chimbuko la Quyi, ingawa inawezekana kuwa watazamaji wamesikiliza ngonjera fulani za vichekesho mara nyingi, lakini hawachoki. Wasanii wa ngonjera huwa wanaanza kujifunza mjini Beijing na kupata maendeleo na kuwa mashuhuri mjini Tianjin. Quyi ya Tianjin inajulikana kote nchini China."

Kila siku jioni kunakuwa na maonesho mengi ya Quyi katika sehemu mbalimbali mjini Tianjin. Mjini humo kuna makundi mengi yanayoonesha ngonjera, na watazamaji huwa wengi.

Katibu mkuu wa Shirikisho la Michezo ya Quyi Bw. Wang Yongliang anaona kuwa kuna sababu kadhaa zinazofanya michezo ya Quyi iwe na hali moto moto mjini Tianjin: Moja ni kuwa mji wa Tianjin una msingi mzuri wa utamaduni huo wa jadi, na ni chanzo cha ngonjera ya vichekesho ambayo mpaka sasa imekuwa na miaka zaidi ya mia moja; Pili ni kuwa watu wengi wanaipenda Quyi, na sababu ya tatu ambayo ni muhimu zaidi ni kuwa serikali inasaidia sana kuistawisha michezo hiyo ya sana hiyo. Bw. Wang Yongliang alisema,

"Kila baada ya miaka mitatu tunafanya tamasha la michezo ya Quyi, wachezaji wanaonesha michezo yao waliyotunga au michezo ya zamani waliyogundua. Kwa kufanya tamasha hilo michezo ya Quyi ikiwemo ngonjera ya vichekesho inastawi zaidi. Pamoja na kufanya tamasha kila baada ya miaka mitatu huku tumeunda jopo la watunzi wa ngonjera ya vichekesho na kupitia na kuboresha miswada mpaka ioneshwe jukwaani."

Mwanzoni mwa miaka ya 90 michezo ya Quyi ilikabiliwa na changamoto ya utamaduni kutoka nchi za nje. Maonesho ya michezo mara nyingi hayakuwa na watazamaji wengi, Quyi ilikuwa na hali mbaya. Wakati huo serikali ya mji ilichukua hatua nyingi ikiwa ni pamoja na kuunda makundi ya watoto na kuchagua wanafunzi watoto kutoka shule za Quyi na kuwapeleka kwenye shule ya ngazi ya juu kuendeleza usanii wao, watoto hao baada ya kuhitimu wanapelekwa kwenye makundi ya Quyi, sasa wamekuwa uti wa mgongo katika makundi yao. Pamoja na hayo serikali ya Tianjin inajitahidi kuwabakiza wachezaji vijana kwenye makundi ya michezo hiyo ya sanaa hiyo. Bw. Wang Yongliang alisema,

"Idara ya Utamaduni ya Tianjin mara nyingi ilifanya maonesho ya ngonjera ya vijana ili kuwapatia nafasi nyingi za kujipatia uzoefu, na tuliwaalika wataalamu kuwasaidia."

Tianjin ikiwa ni chimbuko la Quyi, walijitokeza wasanii wengi hodari wakiwemo Liu Baoquan, Ma Sanli, Zhang Shouchen na Hou Baolin, mazingiza mazuri ya michezo ya Quyi mjini Tianjin yamewasaidia wachezaji vijana kukua kisanii. Lakini kila aina ya sanaa haipatikani bila juhudi. Bw. Huang Tieliang ni mtu muhimu katika kundi lake la michezo, hivi sasa ingawa amekuwa na umri wa miaka 70 na anafundisha katika shule ya michezo ya Quyi, lakini kila siku jioni bado anakwenda kwenye jumba la michezo kuonesha michezo yake. Alisema, anapenda sana ngonjera ya vichekesho, kwa hiyo haoni uchovu. Bw. Huang anafurahia hali ya sasa ya ngonjera ya vichekesho mjini Tianjin. Alisema,

"Mji wa Tianjin ni chimbuko la Quyi, watazamaji wengi wanaipenda sanaa hiyo, kwa hiyo sanaa hhiyo haiwezi kuzorota. Hivi sasa kuna makundi manne au matano hivi yanayoonesha michezo yao kila siku na watazamaji ni wengi."

Mjini humo hivi sasa watazamaji wengi ambao ni vijana wanaingia mikahawani kusikiliza ngonjera ya vichekesho. Bw. Chen Zhiming aliyeonesha ngonjera kwa miaka 54, ameshuhudia mabadiliko ya hali ya michezo ya sanaa hiyo. Alianza kuonesha ngonjera tokea alipokuwa na umri wa miaka 7 na alipita kwenye kipindi cha kufikia kileleni na kushuka bondeni kwa michezo hiyo ya sanaa. Alisema, hivi sasa mabadiliko makubwa yametokea ikilinganishwa na zamani. Alisema,

"Hapo zamani nilipoanza kuonesha ngonjera ya vichekesho watazamaji wengi walikuwa wazee, lakini sasa jambo la kufurahisha ni kuwa idadi ya wazee haikupungua na idadi ya wasikilizaji vijana imeongezeka wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, hali hiyo ni ya kufurahisha sana, na hii ni nguvu ya uhai wa ngonjera."

Ustawi wa Quyi hauwezi kutengana na uungaji mkono wa serikali ya Tianjin. Naibu mkuu wa Idara ya Utamaduni ya Tianjin Bw. You Qingbo alisema,

"Ili kuandaa wasanii wa michezo ya sanaa ya Quyi tumeanzisha shule mbili za Quyi, na mwaka 2002 shule hizo zimepandishwa ngazi ya chuo, licha ya shule hizo mbili pia kuna Chuo Kikuu cha Quyi kilichoanzishwa mwaka 1986."

Bw. You alisema, ili kuwaburudisha wakazi serikali ya mji inafanya matamasha ya Quyi mara kwa mara, ili michezo hiyo sanaa hiyo iote mizizi miongoni mwa wakazi.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-17