Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-18 10:24:11    
Barua 0316

cri

Bw Charles Nyachaki Mwamba P. O. Box 2832 Kisumu, Kenya ametuletea barua akitoa Maelezo kuhusu Michezo ya Olimpiki ya Mwaka 2008 ya Beijing Moyoni Mwangu" Anasema anafuraha kupata fursa hii ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika chemsha bongo isemayo "Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki", katika idhaa ya Kiswahili ya CRI. Hii ni motisha kubwa kwa wasikilizaji wa radio China kimataifa na huenda hivi karibuni tukakutana mjini Beijing.

Anasema makala zote 4 zina mafunzo mengi zaidi kuhusu maandalizi ya michezo, mwito wa kauli mbiu ya "Dunia Moja na Ndoto Moja". Pia amefurahishwa na jinsi serikali ya China imejitolea kuhakikisha kuwa michezo hii inafana na kuwa maalum, na tarehe ambayo imepangwa kufanyika kwa michezo hiyo yaani Agosti 8 hadi 24, 2008 ni nzuri. Anaipongeza serikali ya China kwa kujiandaa vilivyo katika kuona ya kwamba viwanja vitakavyotumika, majumba yanayohitajika, usalama wa wachezaji, mashabiki na wageni watakaohudhuria kwenye michezo hii umeimarishwa kikamilifu. Hii inaonesha wazi jinsi ambavyo serikali ya China inavyoshughulika, ili kuhakikisha kuwa Michezo ya Beijing inakuwa na umaalumu wa kiwango cha juu sana. Anasema ombi lake ni kuona ya kwamba ufunguzi wa michezo kwenye Kiota unafanyika akiwa mmoja wa wale mashabiki ambao watakaohudhuria. Kama si hivyo, basi ufungaji wa hii michezo usimpite, hiyo ni moja ya sababu ya yeye kushiriki kwenye shindano hili.

Anasema moyoni mwake anaona kuwa, Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 ya Beijing itakuwa ni michezo ya hali ya juu na yenye umaalum wa kipekee, na anaweza kuona jinsi Wachina walivyojitolea kuona kwamba Michezo ya Beijing inaandaliwa kwa mafanikio. Pia asingekuwa na fursa ya kushiriki katika mashindano haya na kujua mengi kuhusu China kama si juhudi za Radio CRI-China na CRI-Nairobi. Anaomba tuendelee kuwaelimisha zaidi, na ni matumaini yake kuwa siku kumi nchini China kamwe hazitampita.

Na msikilizaji wetu mwingine Damas M. Bundala ambaye barua zake huhifadhiwa na Fabian Amasi wa sanduku la posta 46116, Dar es Salaam, Tanzania Vilevile ametuletea barua kuhusu Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya Mwaka 2008, anasema kwanza kabisa anapenda kutupongeza kwa kuwafafanulia mengi kuhusu Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 mjini Beijing China. Chemsha Bongo hii ya "tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki" imewafumbua macho juu ya michezo hii mwaka huu wa 2008. Na hili limemfanya awe na hamu sana ya kuendelea kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa na ana ndoto ya kweli kwamba tutakutana Beijing karibuni. Anasema amefuatilia makala zetu nne kuhusu michezo ya Olimpiki, na amevutiwa kwa kujua mengi kupitia makala hizo.

Anasema kwenye makala ya kwanza ambayo inazungumzia juu ya maandalizi ambayo yanafanywa na serikali ya China, amepata kuona jinsi waandaaji wanavyojitolea ili kufanya michezo ya Olimpiki iwe mizuri na ya kuvutia. Pia wakati ambao umewekwa wa hii michezo ya Agosti tarehe 8, mwaka 2008 hadi tarehe 24 Agosti ni wakati mzuri sana kwani wengi watapata nafasi ya kuhudhuria katika michezo hii.

Pia katika makala ya pili alivutiwa na mwito wa kauli mbiu ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing ambao ni "Dunia Moja na Ndoto Moja", hii inaonesha sifa ambayo China imejipatia kwa kuyaunganisha mataifa mbalimbali ya dunia kwa kauli mbiu hiyo. Anasema ana hamu sana ya kupatana na wanasesere watano ambao ni Beibei, JingJing, Huanhuan, Yingying, na Nini.

Na kwenye makala ya tatu anasema, imeonesha kuwa China ilijiandaa vya kutosha kwa kuonesha ustadi wake katika kazi ya ujenzi wa viwanja na majumba 37 ya michezo ambayo yanahitajika, ili michezo hiyo iwe na umaalumu wa kiwango cha juu. Anasema alishiriki kwenye shindano hili kwa madhumuni kuwa, anaweza kupata bahati ya kuona kiwanja ambacho kimejaa watazamaji.

Makala ya nne inazungumzia juu ya miji itakayoshirikiana na Beijing kuandaa michezo ya Olimpiki ambayo ni Tianjin, Qinhuangdao, Shanghai, Shenyang, Qingdao na Hongkong. Roho yake itadunda kwa furaha kufika mji wa Hongkong ambao utaandaa mchezo wa ustadi wa farasi, mchezo ambao anaupenda mno. Maoni yake moyoni ni kwamba "anawaombea" wanamichezo wa Olimpiki wa Mwaka 2008, ambayo itakuwa ni moja ya michezo yenye mafanikio makubwa. Anamaliza barua yake kwa kuipongeza Radio China Kimataifa kwa kuwapatia wasikilizaji wake nafasi nzuri ya kusoma mengi na kusikia mengi kuhusu michezo mapema huku maandalizi yakiendelea, hongera CRI China, hongera 91.9 FM Nairobi.

Bw. Kaziro Dutwa S. L. P 209 Songea Ruvuma-Tanzania ametuletea barua akisema, anayo furaha kubwa kupata fursa hii kwa mara nyingine kutuandikia waraka huu, matumaini yake ni kuwa sote tu buheri wa afya.

Madhumuni ya waraka huu ni kutaka kutoa dukuduku lake kuhusu bidhaa hafifu zisizofikia kiwango, na huduma duni zinazotolewa na watu binafsi na makampuni yasiyokuwa na uwezo wa kutengeneza bidhaa zenye kiwango au huduma inayostahili. Katika siku za karibuni kumekuwa na malalamiko mengi sana toka kwa serikali, wizara na mtu mmoja mmoja kwa ama kuuziwa vifaa duni au kandarasi za kibabaishaji mathalani ujenzi wa barabara, majengo na miundo mbinu mingine muhimu kwa maendeleo.

Vitu ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa sana na watu kutofikia viwango ni kama Televisheni, radio, simu, majiko ya umeme, taa za umeme na vyombo vinginevyo vya elektroniki; kingine ni kandarasi za ujenzi wa majengo na miundo mbinu, nyanja hii muhimu ambayo makampuni ya kichina yalikuwa yanaaminika sana siku za nyuma kwa umakini na ustadi wa kazi zao, lakini sasa sifa yake inachafuliwa! Sasa hivi ile sifa iliyokuwa ikipewa kazi za wachina iko mashakani kutokana na uduni wa bidhaa hizi kutokana na teknolojia na malighafi hafifu inayotumika kutengeneza bidhaa na zana za matumizi ya kila siku. Kuna mifano michache tu juu ya haya: Bila shaka China ilipata hasara kubwa kutokana na kuondolewa katika soko kwa mamilioni ya wanasesere kutoka Marekani na nchi za Ulaya, kukatishwa kwa kandarasi za ujenzi zinazofanywa na makampuni ya China, haya ni kwa uchache tu kuna mengi mengineyo. Hii ni hatari sana kwa biashara ya China kwani kutokana na ukuaji wake wa haraka wa uchumi na teknolojia ya kisasa, dunia inategemea kuwa China itachukua uongozi wa mambo ya kiufundi na uchumi ulimwenguni, lakini Je! nani yuko tayari kuuziwa bidhaa hafifu au miundo mbinu duni?

Umefika wakati sasa China itoe kauli ikanushe au ithibitishe iwapo bidhaa hizi zinatengenezwa China au ni mchezo tu unachezwa na washindani wa kibiashara na China ili kuichafulia soko lake? Inatia shaka kwani bidhaa hizi huwa hazioneshwi kama zimetengenezwa wapi, au zimetengenezwa na kampuni gani. Na hakuna maelezo yoyote lakini watu hutuhumu kuwa zimetengenezwa na China, hivi ni kwa nini?

Anasema yeye kama rafiki wa China hakika hili linamkereketa sana kwani yeye amekuwa akijivunia sana sifa, ustadi na ustaarabu wa China lakini hili la sasa hakika linamweka njia panda huku akijua kwamba tuhuma za ulaghai kwa China ni sawa na tuhuma kwa ndugu yake. Anaomba China ifanye mambo yafuatayo ili kupunguza kupakwa matope huku na aidha makampuni yake au hila za watu wasioitakia heri China. Yeye anapendekeza China idhibiti utengenezaji na uuzaji wa bidhaa nje, na bidhaa zinazouzwa nje ziwe ni zile zinazokidhi viwango vya kimataifa tu. Pia ianzishe baraza madhubuti linalosimamia utengenezaji na uuzaji wa bidhaa nje. Bidhaa zinazouzwa nje ziwe na alama maalumu ya shirika la viwango la China, jina la mtengenezaji liandikwe bayana na lisiandikwe kwenye vikaratasi tu, lazima iandikwe kwenye bidhaa husika. Makampuni yote yanayopata kandarasi nje ya nchi yathibitishwe na kupata baraka za shirika la viwango la China. Anasema bidhaa za China bado zinapendwa sana duniani, hivyo anaomba serikali ifanye kila liwezekanalo kulinda sifa ya bidhaa zake. Mwisho anawaomba wananchi wa China wanaotoa bidhaa na huduma mbalimbali wazalishe bidhaa bora, siyo bora bidhaa kwani wanajichimbia kaburi lao wenyewe kwa tamaa ya utajiri wa haraka.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Dutwa kutuletea barua kueleza dukuduku lake kuhusu sifa ya bidhaa za China. Kweli mwaka jana Marekani ilirudisha bidhaa za wanasesere zilizotengenezwa na sehemu moja nchini China, tukio hilo lilisababisha mashaka mengi kwa sifa ya bidhaa za China, lakini baadaye vyombo vya habari vya nchi za magharibi vilichapisha makala zikisema kuwa, bidhaa hizo za wanasesere zilitengenezwa kwa kufuata usanifu wa waagizaji wa Marekani, wafanyakazi wa China walitekeleza tu matakwa ya waagizaji. Hivi sasa kweli kuna sehemu nyingi nchini China ni kama karakana za kutengeneza bidhaa kutokana na maombi ya wafanyabiashara wa nchi mbalimbali duniani, ni kweli kuwa kuna baadhi ya bidhaa hazijafikia sifa nzuri na serikali ya China imeweka utaratibu mkali wa kuhakikisha viwanda vyote vinatengeneza bidhaa zinazofikia vigezo, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za magharibi vinavyotia chumvi kuhusu dosari za bidhaa za China pia vina makusudi fulani. Serikali ya China imetilia maanani sana hali hiyo, na imechukua hatua mbalimbali za kusimamia sifa ya bidhaa na usalama wa vyakula, ili kuzuia tukio kama hilo lisitokee. Matatizo kadhaa yanayotokea kwenye mchakato wa kujiendeleza kweli hayaepukiki, lakini tunapaswa kufanya juhudi kuhakikisha mambo ya uchumi wa China yaendelezwa vizuri na kwa kasi, bila kuwa na athari mbaya kwa nchi nyingine. Pia kuna baadhi ya watu binafsi wanaofanya ushirikiano wa kibiashara ambao una athari mbaya kwa ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika, na kama ulivyosema kuna baadhi ya bidhaa hata hazioneshi zinatoka wapi, lakini China ndiyo inabebeshwa lawama, kutokana na juhudi za pamoja katika siku zijazo hali hiyo itadhibitiwa