|
Wakati tarehe 20 Machi mwaka huu ambayo ni mwaka ya 5 ya kuanzishwa kwa vita vya Iraq inapokaribia, makamu wa rais wa Marekani Bw. Dick Cheney tarehe 17 mwezi huu alifanya ziara ya ghafla nchini Iraq bila kutangaza habari yoyote. Bw. Cheney akiwa ni mpangaji wa vita hivyo, maoni aliyotoa katika ziara hiyo kuhusu vita vya Iraq yanafuatiliwa sana.
Bw. Cheney baada ya kukutana na waziri mkuu wa Iraq Bw. Nouri al-Maliki alisema, vita vya Iraq vilivyoanzishwa na Marekani mwaka 2003 ni juhudi zilizofanikiwa katika kusukuma mbele usalama na mchakato wa siasa wa Iraq. Bw. Cheney pia alifanya mazungumzo na balozi wa Marekani nchini Iraq Bw. Ryan Crocker na kamanda wa jeshi la Marekani nchini Iraq Bw. David Petraeus. Walipozungumzia suala la kuondoa jeshi la Marekani kutoka nchini Iraq, Bw. Cheney alisema, Marekani kuondoa jeshi lake nchini Iraq kutaathiri hali ya usalama inayoboreka nchini humo, hivyo Marekani haipangi kuondoa jeshi lake haraka. Lakini Bw. Cheney pia alisema, Iraq pia inakabiliana na masuala mengi yanayohitajika kutatuliwa, na Marekani inataka kuisaidia Iraq kutatua masuala hayo.
Vyombo vya habari vya Mashariki ya kati vinaona kuwa ziara ya Bw. Cheney ina malengo kadhaa yanayofuata:
Ya kwanza ni kutetea sera ya Marekani kwa Iraq. Bw. Cheney amekiri kuwa, katika miaka kadhaa iliyopita juhudi za jeshi la Marekani nchini Iraq zilikabiliana na matatizo na changamoto. Lakini anaona kuwa, ikilinganishwa na hali ya nchini Iraq miezi 10 iliyopita, hivi sasa matukio ya kimabavu yamepungua kidhahiri, hali hiyo imethibitisha kuwa juhudi za Marekani zimefanikiwa. Bw. Cheney alisema kupatikana kwa maendeleo hayo kunatokana na Marekani kuongeza askari elfu 30 nchini Iraq mwaka jana.
Ya pili ni kueleza msimamo kuwa Marekani haitaondoa jeshi lake nchini Iraq bila kujali maoni ya upinzani kutoka nchini humo na jumuiya ya kimataifa.
Ya tatu ni kupunguza athari za Iran kwenye kanda hiyo. Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran alifanya ziara nchini Iraq mwanzoni mwa mwezi huu, ambayo imeinua kwa ufanisi athari ya kidiplomasia ya Iraq, na hiyo pia ni ushindi mdogo wa Iran katika mapambano dhidi ya Marekani. Lakini Marekani haiwezi kuruhusu kutokea kwa hali hiyo, katika ziara hiyo ya Bw. Cheney alizitaka nchi za kiarabu za Ghuba ya Uajemi kuanzisha uhusiano kamili wa kibalozi na Iraq, na kushirikiana katika kupunguza athari ya Iran kwa Iraq na kwenye kanda hiyo.
Vyomba vya habari pia vimesema kuwa, mwaka huu ni mwaka ambao uchaguzi mkuu wa Marekani utafanyika, chama cha Republic na chama cha Demokrasia vitaanza kugombea urais wa nchi hiyo. Bw. Cheney akiwa ni mtu muhimu wa chama cha Republic, katika ziara hiyo aliendelea kutetea na kutangaza sera za serikali ya Bush kwa Iraq, kidhahiri anataka kujipatia uungaji mkono kwa chama chake katika uchaguzi huo.
|