Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-19 15:05:36    
Fundi hodari wa kutengeneza Tianqin ambayo ni ala ya muziki ya kabila la Wazhuang

cri
Kwenye wilaya ya Longzhou ya mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi ulioko kusini magharibi mwa China, kuna sanaa ya ala ya kale ya Tianqin ya kabila la Wazhuang. Bw. Qin Huabei mwenye umri wa miaka 43 ni fundi hodari wa kutengeneza ala hiyo, na ametoa mchango mkubwa kwa ajili ya kueneza sanaa hiyo.

Wapendwa wasikilizaji, mnaosikia ni muziki uliopigwa na Bw. Qin Huabei pamoja na binti yake kwa ala ya Tianqin. Tianqin ni ala ya muziki ya kale, na ina historia ya miaka karibu elfu moja. Ala hiyo inaundwa kwa ufito wa mbao, bomba lililotengenezwa kwa kibuyu na nyuzi mbili. Zamani Tianqin ilitumiwa na watu wa mambo ya jadi katika shughuli zao za kufanya ibada na kuomba baraka, na sasa inatumiwa na wasanii wa kabila la Wazhuang kupiga nyimbo za kikabila.

Bw. Qin Huabei wa kabila la Wazhuang alizaliwa kwenye tarafa ya kabila hilo ya wilaya ya Longzhou. Babu yake alikuwa msanii wa Tianqin, na Bw. Qin Huabei alianza kupenda ala hiyo ya muziki alipokuwa na umri mdogo. Alisema,

"Nilipokuwa mtoto mdogo, wakati babu yangu na wenzake walipozitengeneza Tianqin, nilikaa karibu nao mara kwa mara ili kuangalia wanavyozitengeneza. Babu yangu hakuweza kutengeneza Tianqin tu, bali pia aliweza kupiga vizuri sana ala hiyo. Hatua kwa hatua nilianza kupenda muziki wa Tianqin na ala hiyo ya muziki hiyo."

Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, Bw. Qin Huabei alijiunga na kikundi cha maonesho ya michezo ya sanaa cha wilaya ya Longzhou. Baada ya kumaliza shughuli za kawaida, alianza kazi ya kuboresha ustadi wa utengenezaji wa Tianqin. Lakini wakati ule kutokana na sanaa ya Tianqin kutotiliwa maanani na kutohifadhiwa vya kutosha, kazi yake haikupata maendeleo makubwa.

Baada ya kuingia karne ya 21, ili kuokoa sanaa ya Tianqin ambayo iko hatari ya kutoweka, serikali ya wilaya ya Longzhou ilianza kufanya juhudi kubwa ya kuhifadhi sanaa hiyo, na mwaka 2003 ilianzisha kikundi maalumu cha mchezo wa sanaa Tianqin kinachoundwa na wasichana 15 wenye umri wa miaka kati ya 15 na 21, na kutaka kufanya maonesho kwenye tamasha la sanaa la mji wa Nanning yatakayofanyika mwaka huo. Maofisa wa serikali walimtafuta Bw. Qin Huabei na kumtaka atengeneze ala ya Tianqin kwa ajili ya maonesho hayo. Baada ya kusikia habari hiyo, Bw. Qin Huabei alifurahi sana, alisema,

"Mkuu wa idara ya utamaduni na michezo aliniambia matakwa yao, kisha nilitengeneza ala ya Tianqin kwa ajili ya maonesho hayo. Kusema kweli, nilizoea kutengeneza ala hiyo ya muziki, wakati nilipokuwa kwenye kikundi cha maonesho ya michezo ya sanaa niliwahi kuzitengeneza, lakini sikuzionesha hadharani."

Bw. Qin Huabei alianzisha karakana ndogo nyumbani kwake, kila siku baada ya kukusanya malighafi ya kutengeneza Tianqin vijijini wakati wa mchana, alizitengeneza kutuwa kucha. Mwezi Novemba mwaka 2003 kwenye tamasha la tano la kimataifa la nyimbo za kimakabila la mji wa Nanning, kikundi cha wasichana 15 waliovaa nguo zenye umaalumu wa kabila la Wazhuang waliimba nyimbo nzuri huku wakipiga muziki kwa kutumia ala ya Tianqin zilizotengenezwa na Bw. Qin Huabei, maonesho yao mazuri yaliwavutia sana watazamaji wote.

Baada ya hapo kikundi hicho wakichukua ala ya Tianqin zilizotengenezwa na Bw. Qin Huabei walifanya maonesho kwenye sehemu mbalimbali nchini China. Kuanzia mwaka 2003, kwa nyakati totauti, kikundi hicho kilitoa maonesho nchini Austria, Ujerumani na kwenye nchi nyingine, na ala za muziki za Tianqin zilizotengenezwa na Bw. Qin Huabei pia ziliuzwa vizuri kwenye nchi za nje zikiwemo Marekani na Japan.

Kutokana na Tianqin ilivumbuliwa na wenyeji, ilitengenezwa kwa njia rahisi, na ilikuwa na madosari mbalimbali kama vile sauti nyembamba ya muziki na usumbufu wakati wa kupiga. Hivyo katika miaka ya hiv karibuni, Bw. Qin Huabei alifikiri sana namna ya kuboresha ala hiyo ya muziki yenye historia ndefu. Alisema,

"Sifa ya Tianqin haikuwa nzuri. Zamani vibuyu vilivyotumiwa kutengeneza bomba vilikuwa vinakaushwa kwa moto mara moja baada ya kuchumwa, lakini hivyo muziki uliopigwa kwa Tianqin haukuwa mzuri, mbali na hayo vibuyu vilivunjika kwa urahisi."

Baada ya kufanya majaribio kwa mara nyingi, mwisoni Bw. Qin Huabei alitengeneza Tianqin yenye sifa nzuri, sauti nyororo ya muziki na kuweza kupigwa kwa urahisi, hata muziki ya kisasa unaweza kuchezwa kwa kutumia Tianqin mpya.

Hivi sasa idara zinazohusika za wilaya ya Longzhou zinatilia maanani sana kuhifadhi sanaa ya Tianqin, iliweka orodha ya majina ya wasanii wa Tianqin, kutunga muziki mpya kwa sanaa hiyo, na kufundisha sanaa ya Tianqin mashuleni. Sasa Tianqin imekuwa ala nzuri ya muziki inayopendwa na watu wengi kwenye wilaya ya Longzhou. Bw. Qin Huabei anafurahi sana na kuona mabadiliko hayo. Alisema,

"Wanafunzi wengi hasa wasichana walinifuata mara kwa mara baada ya kumaliza masomo shuleni, na kunitaka niwafundishea kupiga ala ya Tianqin, na ninafurahi sana."

Mwezi Mei mwaka 2007 mkutano wa kwanza wa kuwateua warithi wazuru wa utamaduni na sanaa za umma wa China ulifanyika hapa Beijing, na Bw. Qin Huabei akiwa fundi hodari pekee wa kutengeneza Tianqin, aliteuliwa kuwa mmoja kati ya warithi hodari 166 wa utamaduni wa umma nchini China. Bw. Qin Huabei alisema anamatumaini kuwa, atakuwa na karakana nzuri ya kutengeneza Tianqin ili kuendeleza zaidi sanaa hiyo.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-19