Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-19 19:43:08    
Jumuiya ya kimataifa yaendelea kuhimiza utatuzi wa suala la Darfur

cri
Mkutano wa majadiliano yasiyo ya rasmi kuhusu utatuzi wa suala la Darfur ambao ulianzishwa kwa pamoja na mjumbe maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia suala la Darfur Bw. Jan Eliasson na mjumbe maalum wa suala hilo wa Umoja wa Afrika Bw. Salim Ahmed Salim, ulimalizika tarehe 18 Machi huko Geneva, Uswisi. Mkutano huo ni juhudi nyingine za jumuiya ya kimataifa katika kuondoa mgogoro wa Darfur, na kuhimiza mchakato wa kisiasa upate maendeleo halisi.

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wamekuwa wakisukuma mbele mchakato wa maafikiano ya kisiasa kuhusu suala la Darfur la Sudan. Mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia suala la Darfur Bw. Salim Ahmed Salim alieleza kwenye mkutano huo kuwa, hivi sasa mchakato wa maafikiano ya kisiasa kuhusu suala la Darfur bado unakabiliwa na matatizo mbalimbali. Akizungumzia kama mkutano huo umeweka tarehe halisi kuhusu mchakato wa siasa wa Darfur, Bw. Salim alisema:

"Kazi muhimu si kuweka muda wa mwisho wa miezi sita au tisa kuhusu suala hilo, muhimu zaidi ni kuwa pande zote zinazohusika, wasimamizi na washirika wote wa kimataifa wanaona kwa kauli moja kuwa inapaswa kutatua suala la Darfur kwa kutegemea mchakato wa kisiasa."

Baada ya Mkutano wa mchakato wa amani ya Darfur kufanyika mwezi Oktoba mwaka jana nchini Libya, makundi ya upinzani ya Sudan hayakupenda kurejea kwenye mazungumzo, hali ambayo iliufanya mchakato wa kisiasa wa Darfur ukwame kwa miezi kadhaa iliyopita, na wajumbe wa serikali ya Sudan na jeshi la upinzani hawakushiriki kwenye mkutano wa majadiliano yasiyo rasmi. Mjumbe maalum wa suala la Darfur wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Eliasson anaona kuwa, inapaswa kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa kisiasa wa Darfur. Alisema:

"Pande zote zinazohusika zimefikia makubaliano kuwa, inapaswa kuharakisha mchakato wa kisiasa wa Darfur, kwani watu wengi wanakumbwa na uchungu kutokana na migogoro. Pia tunaona kuwa mchakato huo wa kisiasa unatakiwa kushirikisha makundi ya jamii, viongozi wa madhehebu, makundi ya wanawake na watu wanaoshughulikia mambo ya uchumi."

Sudan ni nchi yenye eneo kubwa zaidi barani Afrika ambayo inapakana na nchi tisa, na iko kwenye sehemu ya mpito inayounganisha sehemu za kiarabu na sehemu zilizoko kusini mwa Sahara, na ina mchanganyiko wa utamaduni wa kiislamu na kidini. Mwelekeo wa hali ya Sudan utaleta athari za moja kwa moja kwa sehemu ya mashariki na ya kati barani Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni jumuiya ya kimataifa imefanya juhudi bila ya kusita kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro wa Darfur. Mjumbe maalum wa serikali ya China anayeshughulikia suala la Darfur Bw. Liu Guijin ambaye alihudhuria mkutano huo alisema,

"China imefanya kazi nyingi katika kusukuma mbele serikali ya Sudan kukubali kuwekwa kwa jeshi la mseto la kulinda amani la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, kazi ambazo zimesifiwa na jumuiya ya kimataifa. China vilevile ni nchi ya kwanza nje ya bara la Afrika kutuma jeshi la kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur. Ingawa jeshi la kulinda amani halijatekeleza jukumu kwa muda mrefu huko, lakini limefanya kazi yenye mafanikio ambayo inasifiwa na Umoja wa Mataifa, na kukaribishwa na serikali ya Sudan na wananchi wa huko. Serikali ya China pia imefanya juhudi kubwa katika utoaji wa misaada ya kibinadamu huko Darfur, na mwaka jana ilitoa vitu vyenye thamani ya Yuan milioni 80 kwenye sehemu hiyo."

Bw. Liu Guijin pia alieleza kuwa, China imefanya juhudi kubwa katika kutatua mgogoro wa Darfur. Alisema: "Lengo la China ni kutafuta njia ya kudumu ya kutatua suala la Darfur, ambalo linalingana na sera za China kwa Afrika na nchi nyingine zinazoendelea. China inapenda kutoa mchango kwa ajili ya amani na maendeleo ya Sudan na utatuzi wa suala hilo."

Bw. Salim pia alisifu juhudi za China katika utatuzi wa suala la Darfur akisema:

"China ni nchi yenye umuhimu mkubwa, kwani China si kama tu ni mjumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, bali pia ni rafiki wa nchi za Afrika, na imefanya kila linalowezekana kwa ajili ya amani ya Darfur. Kuondoa mgogoro wa Darfur kunalingana na maslahi ya wananchi wa Sudan na wakazi huko Darfur watanufaika zaidi."