Tarehe 20 Machi miaka mitano iliyopita, pamoja na mlio wa king'ora jeshi la Marekani lilianzisha vita dhidi ya Iraq. Leo baada ya miaka mitano kupita vita hivyo vinavyoongozwa na Marekani licha ya kutatua suala la Iraq, vimeizamisha nchi hiyo kwenye hali mbaya zaidi. Katika muda wote huo wa miaka mitano, wananchi wa Iraq wamekumbwa na matatizo mengi, na mustakbali wao bado hauweleweki. Ifuatayo ni ripoti ya mwandishi wetu kutoka Iraq.
Tarehe 19 Machi mwaka 2003 kabla ya vita Bw. Ali Walid aliongoza familia yake na kuzungukazunguka mwishowe alifanikiwa kuondoka Iraq na kukimbilia Umoja wa Falme za Kiarabu. Alisema,
"Nilikuwa na nyumba kubwa, baada ya vita askari wa jeshi la Marekani walivunja mlango wa nyumba yangu na kuingia ndani, sasa sina chochote nyumbani. Mimi sipendi Iraq ya zamani na vile vile sipendi Iraq ya sasa. Zamani rais Saddam alituumiza, na sasa tunaendelea kuumizwa, kwani hali ya sasa na ya zamani ina tofauti yoyote? Kama kuna tofauti, basi hali ya sasa ni mbaya zaidi kuliko zamani!"
Katika kipindi cha miaka mitano baada ya vita kuanza, Bw. Ali Walid aliwahi kurudi Baghdad mara tatu, hali ya kusikitishwa mjini humo inamkatisha tamaa.
"Muda si mrefu baada ya kutokea vita nilirudi Iraq kwa mara ya kwanza, wakati huo nilikuwa na furaha moyoni kwa kufikiri kwamba pengine hali ya Iraq ingekuwa nzuri, lakini baada ya mwaka mmoja niliporudi kwa mara ya pili, hali niliyoona ilikuwa mbaya zaidi kuliko niliyoiona mara ya kwanza. Baada ya mara ya tatu niliwaambia watu wa familia yangu waache kabisa hamu ya kurudi nyumbani, kila kitu kimeharibu.
Hali ya Ali Walid ni mfano tu wa hali ilivyo kwa raia wote wa Iraq. Katika muda wa miaka mitano, milipuko, mashambulizi na vitendo vya kigaidi, migogoro ya kikabila iliendelea katika ardhi hiyo na kuharibu utamaduni wa Babylon wenye miaka elfu moja. Ingawa katika nusu ya pili ya mwaka 2007 matukio ya milipuko yalipungua lakini tatizo la Iraq linaendelea kuwepo. Bw. Audday al-Katib anafahamu zaidi tatizo hilo, alisema,
"Sababu kubwa ya kuwepo kwa mgogoro wa Iraq hivi sasa ni kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Iraq. Baada ya jeshi la Marekani kuingia nchini, Iraq imekuwa uwanja wa vita kati ya jeshi la Marekani na wapinzani wake, miji imeharibiwa vibaya, na kuingilia kati mambo ya Iraq kumesababisha migogoro ya kikabila nchini humo na kusababisha vitendo vya mauaji. Jeshi la Marekani pia limefanya mauaji, kama jeshi hilo na makampuni ya usalama ya Marekani yakikabiliwa na hatari yanatumia silaha na kuwaua raia. Kadhalika kuwepo kwa jeshi la Marekani pia kumesababisha Iraq kuwa jukwaa la nchi jirani na nguvu za kimataifa kufanya shughuli zao nchi Iraq."
Matokeo mabaya yametokea baada ya jeshi la Marekani kuivamia Iraq, lakini kitu cha kutia wasiwasi zaidi ni kuwa wakati watu wa Iraq wanapokuwa tayari kujenga upya nchi yao na kuleta maafikiano ya kikabila wamegundua kuwa jeshi la Marekani halitaki kuondoka na badala yake linataka kubaki kwa muda mrefu zaidi na hata linataka kuota mizizi huko. Bw. Audday al-Katib alisema,
"Jeshi la Marekani halikusimama kujenga vituo vyake nchini Iraq, na viongozi wa Marekani mara nyingi walisema jeshi la Marekani halitaondoka nchini Iraq, kwa sababu jeshi hilo likiendelea kuwepo nchini humo linaweza kudhibiti eneo la Ghuba, na eneo hilo ni muhimu sana kwa Marekani kutokana na kuwa na mafuta na mahali ilipo kijiografia kwa vita, kudhibiti eneo hilo ni sawa kudhibiti dunia nzima."
Kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Iraq kumesababisha malalamiko mengi kwa watu wa Iraq, wanaona hawatalegeza msimamo wa kuliondoa jeshi la Marekani. Bw. Abdulla al-Khater kwa hasira alisema,
"Jeshi la Marekani lazima liondoke! Watu wa Iraq hawataki kukaliwa! Na jeshi la Marekani nchini Iraq ni jeshi la ukaliaji. Kutokana na maslahi ya Marekani jeshi hilo linang'ang'ani kubaki nchini humo. Bila ya jeshi hilo kuondoka, Iraq kamwe haitapata usalama!"
|