Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-25 10:43:34    
Naibu meneja mkuu wa kampuni ya dawa ya Astellas Bw. Hideaki Mochizuki

cri

Bw. Hideaki Mochizuki ni naibu meneja mkuu wa kampuni ya dawa ya Astellas ya Japan nchini China, anafanya kazi mjini Shenyang, China.

Bw. Mochizuki alianza kufanya kazi zinazohusu dawa baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu, mpaka sasa amefanya kazi hizo kwa miaka 23. Kabla ya kuanza kufanya kazi mjini Shenyang, alifanya kazi katika kiwanda cha kampuni ya Astellas nchini Marekani kwa miaka 6. Bw. Mochizuki alisema kutokana na maisha ya miaka 6 katika nchi ya nje, amezoea kufanya kazi mjini Shenyang. Alipozungumzia hali ya mwanzoni baada ya kufika mji huo, alisema,

"Nilipofika Shenyang kwa mara ya kwanza, niliona taa chache kwenye uwanja wa ndege wa Taoxian, na niliona majengo machache kwenye barabara ya kasi inayoelekea mjini. Lakini baada ya kuingia mjini, niliona kuwa mji huo ni mkubwa ambao una taa zinazong'ara na majengo mengi."

Bw. Mochizuki alisema mwanzoni Shenyang ilimpa picha ambayo si nzuri wala si mbaya. Lakini katika miaka miwili iliyopita, alizoea kufanya kazi na maisha ya huko, na kuupenda mji huo. Alisema,

"Mji wa Shenyang hauwezi kumpa mtu picha ya mji wenye pilika pilika za kazi. Maisha ya hapa ni tulivu, na yananifaa."

Kampuni ya Astellas ni kampuni inayoshughulikia utafiti na uzalishaji wa dawa. Katika miaka miwili iliyopita, kampuni hiyo ikiongozwa na Bw. Mochizuki, ilipata maendeleo ya haraka. Thamani ya uuzaji kwa mwaka imeongezeka kuwa Yuan milioni 600 kutoka Yuan milioni 200 miaka miwili iliyopita. Ingawa kampuni hiyo imepata faida kubwa, lakini Bw. Mochizuki alisema kampuni hiyo haizingatii faida tu. Akiwa ni kiongozi wa kampuni hiyo, anatilia maanani uhifadhi wa mazingira, na kampuni hiyo inafanya uzalishaji usiochafua mazingira. Mara nyingi Kampuni hiyo inasifiwa kuwa ni kampuni nzuri ya kuhifadhi mazingira mjini Shenyang. Alipozumgumzia jambo hilo alisema,

"Katika miaka zaidi ya 10 iliyopita tangu kampuni yetu ijengwe hapa, haijatokea ajali ya kuchafua mazingira kwenye kampuni yetu."

Habari zinasema kampuni hiyo imetenga Yuan milioni moja kupanda majani, na inatumia Yuan laki 1 kuhifadhi majani na miti. Hewa chafu na maji taka yanayoletwa wakati wa uzalishaji, yanatolewa baada ya kusafishwa na vifaa maalum. Kampuni hiyo inatumia maji taka yaliyosafishwa kufuga samaki na kumwagilia kwenye majani. Hatua hiyo si kama tu inazuia uchafuzi wa mazingira, bali pia inabana matumizi ya tani elfu 20 za maji kwa mwaka. Bw. Mochizuki alisema,

"Nataka kuthibitisha kuwa uhifadhi wa mazingira ni muhimu sana, nina matumaini kuwa watu wengi zaidi watakuwa na maoni ya pamoja kuhusu jambo hilo, na watachukua hatua kufuatilia na kuhifadhi mazingira."

Bw. Mochizuki alisema kampuni ya Astellas inapojiendeleza, haisahau wajibu wake wa kijamii. Mwaka 2003 wakati watu wengi waliambukizwa virusi vya SARS, kampuni hiyo ilitoa fedha kununua mashine za kuua vijidudu kwa ajili ya shule za msingi na za sekondari mjini Shenyang. Mwaka 2006 ili kuitikia kampeni ya utaratibu wa aina mpya wa matibabu ya ushirikiano vijijini na maendeleo ya hospitali ya mitaani mijini mkoani Liaoning, kampuni hiyo ilichangia dawa zenye thamani ya Yuan laki 4 kwenye chama cha msalaba mwekundu cha mji wa Shengyang. Katika miaka kadhaa iliyopita, kampuni hiyo ilitoa misaada kwa mara nyingi kwa sehemu zilizokumbwa na maafa na zilizo nyuma kiuchumi. Hadi sasa kwa ujumla kampuni hiyo imechangia Yuan milioni 2. Bw. Mochizuki alieleza matumaini kuwa makao makuu ya kampuni ya Astellas yatatafiti na kuzalisha dawa nyingi mpya, na atafanya juhudi ili dawa hizo zitengenezwe mapema zaidi nchini China na kuwatibu wachina wengi, alisema,

"Ninafanya juhudi kuharakisha usimamizi kuhusu kiwanda chetu mjini Shengyang, ili kiwanda hicho kipate maendeleo zaidi. Nina malengo na mawazo mengi, na nimejiandaa kukabiliana na changamoto nyingi zaidi."

Bw. Mochizuki anafanya kazi katika kampuni kwa muda mrefu kila siku, hivyo anakutana na wafanyakazi wengi wa China. Moyo wao wa kufanya kazi kwa juhudi umempa picha nzuri, alisema,

"Nimewawekea wafanyakazi wetu malengo magumu. Ingawa malengo hayo ni magumu, lakini wanafanya kazi kwa bidii ili kuyatimiza. Wakati fulani wanahitaji kushiriki kwenye mafunzo mbalimbali, juhudi na nia zao za kutimiza malengo zinanifurahisha sana."

Kampuni hiyo Astellas iko kwenye eneo la maendeleo ya uchumi na teknolojia la mji wa Shenyang. Bw. Mochizuki anafanya kazi kwa muda mrefu. Na wakati wa mapumziko, yeye na mkewe wanatembea mjini, ili kujionea maisha ya wakazi wa kawaida mjini humo. Bw. Mochizuki anajua mambo mengi kuhusu mabaki ya kihistoria mjini humo. Kasri la kifalme na kaburi la wafalme la kaskazini ni sehemu ambazo anatembelea mara kwa mara. Alisema anaweza kujionea historia ya mji huo na utamaduni unaong'ara wa China, alisema,

"Nafikiri China ni nchi yenye utamaduni unaong'ara na historia ndefu. China ina historia ya miaka elfu tano, na mabaki mengi ya kihistoria yamehifadhiwa, likiwemo kasri la mfalme na kaburi la kaskazini."

Bw. Mochizuki alisema anataka kuendesha gari na kutembea kwenye mitaa mbalimbali mjini humo kama wakazi wa kawaida wa Shenyang. Lakini kanuni za makao makuu ya kampuni ya Astellas haziwaruhusu wasimamizi wa Japan nchini China kuendesha magari kwenda kazini. Alisema katika miaka miwli iliyopita, ameweza kuona kuwa mji huo unabadilika kila siku, ambao umekuwa mzuri na wa kisasa zaidi, alisema,

"Katika miaka ya hivi karibuni maendeleo ya mji wa Shenyang yamekuwa ya kushangaza watu. Majengo marefu yamekuwa yanajengwa hapa na pale. Rafiki yangu alisema mji huo unabadilika kila saa na kila dakika. Na mtu mwingine alisema mji huo una uchangamfu mkubwa."

Wakati fulani Bw. Mochizuki pia anatembelea miji mingine ya China, alisema,

"Japan imeendelezwa na kuingia kwenye kipindi cha maendeleo ya utulivu, hivyo haitapata maendeleo makubwa zaidi. Lakini China ni tofauti na Japan, ina uwezo mkubwa wa kupata maendeleo, na itaendelea kupata maendeleo makubwa katika siku za usoni."

Bw. Mochizuki aliwahi kuwaalika jamaa na marafiki zake wengi wa Japan kutembelea mji wa Shenyang. Ana matumaini kuwa watoto wake watatu wanaoishi nchini Japan watapata fursa ya kutembelea mji huo. Pia alisema ana matumaini ya kutoa mchango kwa urafiki kati ya watu wa China na Japan.