Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-25 15:57:33    
Bw. Li Changchun afanya mazungumzo na wanafunzi wa Algeria waliorudi kutoka China

cri

Mjumbe wa kudumu wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China Bw. Li Changchun ambaye yuko ziarani nchini Algeria, tarehe 24 kwenye hoteli aliyofikia alifanya mazungumzo na wanafunzi wa nchi hiyo waliorudi kutoka China.

"Kumbukumbu niliyopata nchini China ni moyo wa Wachina wa kupenda kuwasaidia wengine, moyo wao wenye uvumilivu na uzalendo wao, na picha nyingine niliyopata ni vyakula tele wanavyokula katika sikukuu ya Spring, kwa mfano mshikaki, bata wa kuokwa na tambi zenye supu ya nyama ya ng'ombe."

Mjumbe wa wanafunzi Bw. Mohamed Kerbouche anayeweza kuzungumza vizuri lugha ya Kichina, aliwahi kusoma katika Chuo Kikuu cha Biashara ya Kimataifa cha Beijing kwa miaka minne na alipata shahada ya pili. Alisema miaka yake yenye furaha nchini China ilimpatia nafasi nzuri ya kujifunza Kichina na kufahamu utamaduni mkubwa wa China, cha muhimu zaidi ni kwamba amepata uwezo wa kazi kwa sasa na kwa siku zijazo.

Kuandaa wataalamu wa nchi za nje ni aina moja muhimu ya misaada inayotolewa na China kwa nchi za nje. Katika miaka ya hivi karibuni maofisa na mafundi waliofundishwa nchini China wameongezeka kutoka watu elfu moja mwaka 2003 hadi kufikia zaidi ya elfu kumi mwaka 2007. Tokea mwaka 2005 hadi 2007 maofisa na wahandisi wa Algeria zaidi ya mia moja walikuja nchini China kushiriki kwenye masomo. Kupitia masomo na maisha nchini China, marafiki wa Algeria wameielewa zaidi China ilivyo. Mwandishi wa habari wa gazeti kubwa la Algeria Bw. Titouche Ali alisema,

"Naona ajabu jinsi China kubwa ilivyo kwa eneo na nguvu zake za kiuchumi, na nyuma ya maendeleo yake ya haraka nimegundua kuwa China inapenda amani na ni nchi ya kirafiki."

Baada ya wanafunzi hao kusema, Bw. Li Changchun alizungumza nao kwa ukunjufu, akisema,

"Kwenye mazungumzo yenu nyote mmesema kwamba ingawa muda wenu nchini China ulikuwa si mrefu, lakini mavuno mliyopata si madogo, kwanza mmepata elimu mpya, pili mmezidi kuielewa China, na tatu mmezidi kuwa na urafiki na China. Sera za kimsingi za ushirikiano kati ya China na Afrika ni kuimarisha uwezo wa kujitegemea wa nchi za Afrika, kwa hiyo tunataka kuongeza zaidi nguvu za kuwafundisha wataalamu wa nyanja mbalimbali kutoka nchi za Afrika."

Bw. Li Changchun alisema, mwezi Novemba mwaka 2006 kwenye mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika Rais Hu Jintao alitangaza hatua nane za ushirikiano huo, kati ya hatua hizo hatua ya kuandaa wataalamu wa nchi za Afrika ni hatua muhimu. Katika muda wa miaka mitatu tokea mwaka 2007 hadi 2009 China itawaandaa wataalamu wa nchi za Afrika 15,000 na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata msaada wa masomo. Katika mwaka mmoja tu uliopita, China iliwaandaa wataalamu wa nyanja mbalimbali wa nchi za Afrika elfu sita. Mazungumzo yalipomalizika, Bw. Li Changchun alisema anawakaribisha kutembelea China mara kwa mara.

"Kwanza, natumai kuwa watu mliosoma China mtakuwa uti wa mgongo wa taaluma mbalimbali nchini Algeria; Pili ni matumaini yangu kuwa mtakuwa watu mtakaoeneza urafiki kati ya China na Algeria; Tatu ninatumai kuwa mtasukuma mbele ushirkiano kati ya China na Algeria, na ninatumai kuwa mtaichukulia China kama ni maskani yenu ya pili, na mara kwa mara mrudi nyumbani."

Idhaa ya kiswahili 2008-03-25