Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-28 15:27:02    
Wachina wengi wanapenda kwenda kutalii barani Afrika

cri

Katika miaka ya hivi karibuni, uchumi wa Afrika umekuwa ukipata maendeleo makubwa, na migogoro barani Afrika pia inatatuliwa hatua kwa hatua, na nchi nyingi barani Afrika zinachukua hatua za kutangaza vivutio vya utalii kuwa moja ya njia muhimu ya kupata maendeleo endelevu ya uchumi. Hivi saa Afrika imekuwa inavutia watalii wengi kutoka nchi za nje. Takwimu zilizotolewa na shirika la utalii duniani zinaonesha kuwa, shughuli za utalii barani Afrika zimekuwa nguvu kubwa ya kuhimiza maendeleo ya utalii duniani. Katika miaka kadhaa iliyopita, idadi ya watalii wa nchi za nje waliokwenda kutalii barani Afrika iliongezeka kwa asilimia 10 kila mwaka. Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa watalii wengi kati yao ni wachina.

Bi. Zhang ni shabiki wa kutalii, anapenda kutalii kwenye sehemu mbalimbali wakati wa mapumziko. Anapanga kutalii barani Afrika mwezi Oktoba mwaka huu, lakini zamani alitalii nchini China tu, hajapata fursa ya kutalii kwenye nchi za nje, hivyo alikwenda kwenye shirika la utalii na kumwuliza mfanyakazi maswali kuhusu kutalii barani Afrika. Alisema,

"Hivi sasa si ajabu kwa wachina kutembelea nchini Singapore. Malaysia na Thailand, pia ni kawaida kutalii mkoani Hongkong na Macao. Nataka kutalii kwenye sehemu yenye umaalumu. Ikilinganishwa na nchi za Ulaya na Marekani zilizoendelea, bara la Afrika lenye mazingira ya asili linanivutia zaidi."

Mkurugenzi wa shirika moja la utalii mjini Beijing anayeshughulikia soko la kimataifa Bi. Guan alijulisha kuwa, kuna vijana wengi wanaotaka kwenda kutalii barani Afrika kama Bi. Zhang. Alisema,

"Katika miaka ya hivi karibuni wachina wengi zaidi walitalii barani Afrika. Mwaka 2006 mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika hapa Beijing, vyombo vya habari vilijulisha bara la Afrika kwa pande mbalimbali, hii ilihimiza wachina kupenda kwenda kutalii barani Afrika. Nilikumbuka kuwa wakati ule kila siku tulipokea simu zaidi ya mia moja kuhusu mambo ya utalii barani Afrika."

Tangu mwaka 2002 Misri ilipokuwa nchi ya kwanza kupewa hadhi ya kupokea watalii kutoka China, idadi ya wachina waliotalii barani Afrika imekuwa inaongezeka siku hadi siku. Hivi sasa wachina huonekana katika sehemu maarufu za utalii barani Afrika. Bi. Guan alijulisha kuwa vijana wanapenda mambo mapya, ikilinganishwa na sehemu nyingine za utalii, Afrika inawavutia zaidi wachina, hivyo vijana wengi wanapenda kutalii barani Afrika. Kati ya watalii wanaokwenda kutalii barani Afrika vilevile kuna wazee wengi. Bi. Guan alisema,

"wazee hao waliwahi kushiriki kwenye kutoa misaada kwa Afrika, wana hisia nyingi za kirafiki kuhusu Afrika na wanataka kurudi Afrika kuona mabadiliko ya sehemu walipofanya kazi."

Bi. Guan alisema hivi sasa maisha ya wachina yanazidi kuwa mazuri, kutoka kutalii kwenye nchi za Asia ya kusini mashariki hadi utalii barani Ulaya na Afrika, wachina wanataka zaidi kuona utamaduni na vivutio tofauti. Aliona kuwa kutokana na mandhari ya kimaumbile ya bara la Afrika na urafiki mkubwa kati ya China na Afrika, wachina wanapenda kutalii barani Afrika. Mwishoni mwa mwaka jana, Bw. Jiang na mke wake walikwenda kutalii nchini Misri. Alisema,

"Kwa sisi wachina, Afrika ni sehemu yenye miujiza. Ikiwa nchi moja kati ya nchi nne kubwa zenye utamaduni wa kale, Misri ina historia ya muda mrefu na utamaduni wa aina mbalimbali. Tulipokwenda Misri, si kama tu tuliangalia mandhari yake, bali pia tulikwenda kuona ustarabu na mabaki yake ya kale ya utamaduni."

Wakati alipoona mapiramidi, Mto Nile na Sphinx nchini Misri, Bw. Jiang alishangaa sana, alisema,

"Wakati nilipojionea mapiramidi na Sphinx, nilishangaa kwa uwezo mkubwa wa watu wa zama za kale. Katika zama zao ambazo hakukuwa na teknolojia ya kisasa, waliweza kujenga majengo kama hayo, nafikiri ni miujiza."

Licha ya utamaduni na historia ya muda mrefu, maisha yenye umaalumu wa huko pia yaliwavutia Bw. Zhang na mke wake. Bw. Zhang alisema,

"Wakati wa saa nne usiku, wakazi wengi wa Misri walikuwa wanakuja kwenye magulio mjini Cairo na kufanya shughuli mbalimbali za biashara. Nchini China saa nne usiku ni wakati wa kufungwa kwa maduka mengi. Hali hiyo mjini Cairo ilituvutia sana."

Bw. Jiang alisema safari hiyo nchini Misri ilimpa picha nzuri. Ameamua kuwa akiwa na fursa atakwenda kutalii barani Afrika kwa mara nyingine. Alisema,

"Hakina nitakwenda kutalii barani Afrika kwa mara nyingine, kwa sababu sitasahau safari hiyo katika maisha yangu. Kama nitakuwa na fursa, nitatembelea nchi kadha wa kadha za Afrika ya mashariki, kama Kenya, mbuga za wanyama za Kenya ni maarufu sana. "

Kutokana na kuinuka kwa kiwango cha uchumi wa China na kuongezeka kwa mapato ya wananchi nchini China, wachina wanavutiwa na utamaduni na vivutio maalumu barani Afrika. Hivi sasa safari za kutalii kutoka China hadi nchini Misri, Kenya na Afrika kusini zinapendwa sana na wachina, vilevile mashirika kadhaa ya utalii yameanzisha safari za utalii kutoka China hadi Zimbabwe, Mauritius, Shelisheli na Tunisia. Wachambuzi wanaona kuwa kutalii barani Afrika kwa wachina kumeingia kwenye kipindi cha maendeleo makubwa.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-28