Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-26 16:50:31    
Jeshi la Iraq lafanya operesheni kabambe dhidi ya "Jeshi la Mehdi"

cri

Alfajiri ya tarehe 25 jeshi la Iraq lilianza operesheni kabambe katika mji mkubwa wa pili wa Iraq Basra, lakini lengo la operesheni hiyo sio magaidi bali ni kundi la wanamgambo "Jeshi la Mehdi". Habari zinasema operesheni hiyo ni kubwa kabisa katika miaka yote mitano tokea vita vya Iraq kuzuka. Chanzo cha operesheni hiyo ni migogoro mfululizo iliyotokea hivi karibuni kati ya jeshi hilo na vikosi vya wanamgambo. Katika siku hiyo kwenye makao makuu ya jeshi la Iraq yaliyopo sehemu ya magharibi ya mji wa Basra na hoteli inayotumiwa na maofisa wa jeshi la Iraq zilishambuliwa kwa makombora, inasemekana kuwa mashambulizi hayo yalifanywa na vikosi vya wanamgambo ambavyo havifuati utawala wa serikali.

Habari zinasema jeshi la Iraq lilizingira sehemu tatu za mjini zilizodhibitiwa na "Jeshi la Mehdi", pande mbili zilipambana vikali. Vyombo vya habari vinasema cha kufuatiliwa zaidi ni kwamba operesheni hiyo iliongozwa na waziri mkuu wa Iraq Nouri Maliki ambaye ni kamanda mkuu wa jeshi la Iraq. Tarehe 24 baada ya kufika mjini Basra Bw. Nouri Maliki alisambaza barua yake kwa wakazi, akisisitiza kwamba serikali ya Iraq inaunga mkono idara za utawala za Basra na itajitahidi kutimiza hali ya usalama, utulivu na utaratibu wa jamii. Jeshi la Uingereza nchini Iraq tarehe 25 lilithibitisha kwamba Bw. Nouri Maliki akiwa kamanda mkuu, hivi sasa anaongoza operesheni, na kusema kwamba katika operesheni hiyo hakuna askari hata mmoja wa Uingereza anayeshiriki, ni operesheni ya jeshi la Iraq peke yake.

Hidi sasa operesheni hiyo imesababisha vifo vya raia kumi kadhaa. Kutokana na kuwa mapambano bado yanaendelea, idadi vya vifo hakika itaongezeka. Operesheni hiyo imeathiri moja kwa moja maisha ya wakazi, Basra na miji mingine jirani tarehe 25 inaendelea kupiga marufuku kutembea wakati wa usiku, kuanzia usiku wa tarehe 24 mji wa Basra ulianza kupiga marufuku magari yote, na magari yote ya serikali yanasimamiwa na polisi. Kuanzia asubuhi ya tarehe 24 shule zote za msingi, sekondari na vyuo vikuu zimefungwa kwa siku tatu. Na barabara zote kutoka Basra hadi mipakani zilifungwa kwa siku tatu kuanzia tarehe 25.

Wachambuzi wanaona kuwa lengo la operesheni hiyo iliyoongozwa na Nouri Maliki ni la mbali. Kwanza Nouri Maliki anatumai kupunguza nguvu za "Jeshi la Mehdi" kupitia operesheni hiyo ili kuweka msingi wa kufyeka kabisa jeshi hilo pamoja na nguvu za kundi la wakurd nchini Iraq. Bw. Nouri Maliki wakati wote anaona kuwa jeshi la Iraq ni jeshi linalowajibika na usalama wa Iraq na vikosi vya wanamgambo vinavyoenea kwenye sehemu mbalimbali nchini ni vikundi vya kuathiri utulivu wa Iraq, kwa hiyo ni lazima vifutwe mapema iwezekanavyo. Zaidi ya hayo, Bw. Mouri Maliki anatumai kupitia operesheni hiyo kushinikiza kisiasa vuguvugu la Muqtada al-Sadr ili lisiendelee kuipinga serikali ya Iraq.

Wachambuzi wanaona kuwa matumaini hayo ya Nouri Maliki hayatakuwa rahisi kutimizwa. "Jeshi la Mehdi" ni moja ya vikundi vya wanamgambo vyenye nguvu kubwa, uwezo wake wa kupigana vita ni mkubwa hata kuliko jeshi la Iraq, kwa hiyo sio rahisi hata kidogo kwa jeshi la Iraq kulishinda jeshi hilo. Zaidi ya hayo tarehe 25 Muqtada al-Sadr ilitangaza kutaka wafuasi wake wafanye maandamo na kutaka serikali isimamishe mapambano dhidi ya "Jeshi la Mehdi". Bw. Muqtada al-Sadr alisema kama serikali ya Iraq ikiendelea na mapambano yake dhidi ya wafuasi wa Muqtada al-Sadr basi atachukua hatua nyingine. Kwa hiyo mapambano hayo kati ya serikali na "vuguvugu la Muqtada al-Sadr" yatakuwaje, bado ni kitandawili.

Idhaa ya kiswahili CRI 2008-03-26