Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-27 14:54:32    
Wilaya ya Yanchi mkoani Ningxia nchini China yapata ufanisi mkubwa katika kuzuia kuenea kwa jangwa

cri

Mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahui wa Ningxia ulioko kaskazini magharibi mwa China, ni mmoja kati ya mikoa iliyoathiriwa vibaya kabisa na jangwa nchini China. Katika miaka 20 iliyopita, eneo la ardhi yenye hali ya jangwa la wilaya ya Yanchi mkoani Ningxia lilichukua karibu asilimia 42 ya eneo la wilaya hiyo. Lakini hivi sasa, wilaya hiyo imeondoa vilima vya mchanga, na kutimiza lengo la kuzuia kuenea kwa hali ya jangwa kwenye ardhi.

Wilaya ya Yanchi iko kusini magharibi mwa jangwa la Maowusu. Kutokana na athari za kimaumbile na vitendo vya binadamu, eneo la ardhi yenye hali ya jangwa linaongezeka siku hadi siku. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika mwaka 1983, eneo la ardhi yenye hali ya jangwa wilayani humo lilichukua zaidi ya asilimia 40 ya eneo la wilaya hiyo, kuna sehemu 5 zenye mchanga unaohamahama. Mwanakijiji wa Yuzhuangzi wilayani Yanchi Bw. Yu Hu akizungumzia mazingira mabaya ya asili ya wakati huo alisema,

"Zamani upepo wenye mchanga ulipovuma tulikuwa hatuwezi kuona vitu vilivyoko kwenye umbali wa mita 10, kondoo walikumbwa na upepo na kupotea, na watu walikuwa hawawezi kurudi nyumbani, kwa sababu hawakuweza kuziona nyumba zao. Zamani watoto kadhaa walifukiwa na mchanga na kufa kutokana na upepo wenye mchanga uliovuma."

Kuenea kwa ardhi yenye hali ya jangwa kumekuwa sababu kubwa inayokwamisha maendeleo ya uchumi wa wilaya ya Yanchi, pia ni sababu ya moja kwa moja iliyofanya sehemu hiyo iwe maskini kwa muda mrefu, na watu wake wasiweze kutatua tatizo la kukosa nguo na chakula cha kutosha. Ili kubadili hali hiyo, serikali ya wilaya ya Yanchi ilitoa wazo la "kuzuia kuenea kwa ardhi yenye hali ya jangwa ili kuishi maisha". Naibu mkuu wa idara ya misitu ya wilaya hiyo Bw. Liu Weize alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa,

"Kuenea kwa ardhi yenye hali ya jangwa kunawaathiri vibaya binadamu, hasa kunaathiri vibaya uzalishaji na maisha ya wakulima wa huko, kunasababisha mashamba kuwa na hali ya jangwa, na kiwango cha uzalishaji wa mashamba kinapungua, hivyo ni lazima kuzuia kuenea kwa ardhi yenye hali ya jangwa, ndipo inapoweza kuboresha mazingira ya kiviumbe, na kuinua uzalishaji wa mashamba, ili kuboresha mazingira ya uzalishaji kwa wakulima wa huko, na kuinua kiwango cha maisha yao."

Kwa kufuata hali halisi ya huko, serikali ya wilaya ya Yanchi ilitumia mbinu za kupanda miti, huku ikiwazuia watu wasiingie milimani, kupanda miti, vichaka na majani kwa pamoja, na kutumia teknolojia ya viumbe huku hatua za kuendeleza miradi zikichukuliwa ili kudhibiti hali ya kuenea kwa ardhi yenye hali ya jangwa. Serikali hiyo ilipanda miti ya aina zinazoweza kukua vizuri huko, na kueneza teknolojia ya kisasa ya kukinga ukame na kupanda miti. Kutokana na juhudi za miaka mingi, wilaya hiyo imejenga sehemu ya kaskazini ya kuzuia upepo na kuhama kwa mchanga, sehemu ya kati ya misitu ya kulinda hali ya viumbe na sehemu ya kusini ya miti ya matunda ya kiuchumi. Licha ya kutilia maanani kazi ya kuzuia kuenea kwa ardhi yenye hali ya jangwa kwa njia za kisayansi, serikali ya wilaya ya Yanchi pia iliimarisha ushirikiano na nchi mbalimbali, na kupata miradi ya kupanda miti kutoka kwa idara husika za Japan na Ujerumani bila malipo. Naibu mkurugenzi wa idara ya misitu ya wilaya hiyo Bw. Liu Weize alisema,

"Ujenzi wa miradi inayosaidiwa na nchi za nje umeboresha kidhahiri mazingira ya hali ya viumbe ya wilaya yetu. Ujenzi wa miradi hiyo sio tu umetoa fedha kwetu, bali jambo muhimu zaidi ni kutuletea uzoefu na teknolojia ya usimamizi, na tuwe na imani kusimamia vizuri mchanga."

Hivi sasa, eneo la ardhi yenye hali ya jangwa la wilaya ya Yanchi ni chini ya hekta elfu 70. Takwimu zinaonesha kuwa, kimsingi wilaya hiyo imeondoa vilima vya mchanga.

Mafanikio iliyoyapata wilaya ya Yanchi yameonesha juhudi kubwa zilizofanywa na mkoa mzima wa Ningxia katika kupanda miti na kudhibiti kuenea kwa ardhi yenye hali ya jangwa. Habari zinasema kuanzia mwaka 2002, mkoa wa Ningxia ulitekeleza mradi wa kushughulikia hali ya jangwa na kupanda miti kwa kukinga upepo wa mchanga, baada ya ujenzi wa miradi hiyo, eneo la misitu na majani katika sehemu zinazotekeleza miradi limepanuka hadi asilimia 48 kutoka asilimia 5 ya zamani, na mazingira ya asili yanaboreshwa kidhahiri. Hivi karibuni, idara ya misitu ya China imekubali rasmi mkoa wa Ningxia kuwa mkoa wa vielelezo vya kushughulikia hali ya jangwa na kukinga upepo wa mchanga nchini China. Naibu mkuu wa idara ya misitu ya China Bw. Zhu Lieke alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema,

"Kuzuia kuenea kwa ardhi yenye hali ya jangwa ni majaribio ya ujenzi wa ustaarabu wa kiikolojia. Hii ni hatua muhimu ya kuhimiza binadamu kuishi katika hali ya kupatana na mazingira ya maumbile. Ardhi kuwa hali ya jangwa ni tatizo sugu katika kujenga ustaarabu wa mazingira ya asili kwa binadamu, lakini mkoa wa Ningxia unatoa mfano mzuri katika upande huo. Hivyo tuna imani kuwa tutahimiza binadamu kuishi katika hali ya kupatana na mazingira ya asili."

Idhaa ya kiswahili 2008-03-27