Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-27 15:18:11    
Mpiga fidla maarufu wa China Lin Zhaoliang

cri

Hivi karibuni mpiga fidla maarufu wa China Lin Zhaoliang alifanya maonesho hapa Beijing. Muziki wake aliopiga kwa fidla yake uliwavutia sana watazamaji.

Bw. Lin Zhaoliang alizaliwa mwaka 1960 kisiwani Taiwan, alianza kujifunza kupiga fidla alipokuwa na umri wa miaka mitano. Alipokumbuka wakati huo alisema,

"Nilikulia kisiwani Taiwan katika mji mdogo wa Xinzhu. Nilipokuwa na umri wa miaka mitano, mtoto mmoja wa jirani alikuwa akijifunza kupiga fidla, nilivutiwa na upigaji wake, wazazi walinipatia fidla moja ndogo ya kuchezea na nilianza kuichezacheza. Wazazi wangu waliona nina kipaji cha muziki, wakaninunulia fidla ya kweli na kunipeleka kwenye shule. Tokea hapo nilipokuwa na umri huo wa miaka mitano sikuacha kupiga fidla."

Bw. Lin Zhaolin licha ya kuwa na kipaji cha muziki pia alifanya mazoezi bila kusita toka alipokuwa mtoto mdogo, na alipokuwa na umri wa miaka kumi alipata ubingwa wa kikundi cha watoto katika mashindano ya muziki wa fidla kisiwani Taiwan. Baadaye Bw. Lin Zhaolin aliendeleza usanii wake nchini Australia na Marekani, na alipokuwa na umri wa miaka 17 alijipatia umaarufu duniani. Alisema,

"Wakati huo nilikuwa nimemaliza tu shule ya sekondari, nilikuwa na umri wa mika 17. Nilipokuwa nchini Hispania nilishiriki kwenye mashindano ya muziki wa fidla ya shule ya kimataifa ya muziki ya Sophia na nilipata nafasi ya kwanza. Kutoka hapo maisha yangu yalibadilika kabisa, nilianza kuwa na shughuli nyingi za maonesho nchini Hispania. Kufanya maonesho mbele ya watazamaji kuliniwezesha kujipatia uzoefu. Kwa sababu kufanya mazoezi chumbani hata ukifanya mara ngapi huwezi kuwa jasiri kama usipofanya maonesho halisi mbele ya wasikilizaji. Kwa hiyo nilifurahia kufanya maonesho."

Bw. Li Zhaoliang alisema kujifunza kupiga fidla ni kazi ngumu lakini yenye furaha. Jambo la ajabu liliwahi kutokea kwamba, siku moja Bw. Lin Zhaoliang alimwachia fidla yake mwanamuziki mmoja mashuhuri wa fidla, aligundua kiajabu kwamba mwanzoni sauti ya fidla yake aliyopiga mwanamuziki huyo ilikuwa sawa na sauti ya fidla aliyopiga kila siku mwenyewe lakini baada ya dakika tano hivi sauti ikabadilika na kuwa kama ya fidla ya yule mwanamuziki. Bw. Li Zhaoliang alisema kama si jambo alilofanya yeye mwenyewe, kamwe haamini kama fidla inaweza kutoa sauti ya ajabu kama hiyo. Na Sasa Bw. Li Zhaoliang ana mazoea ya kutembea na fidla yake kila mahali. Alisema,

"Mimi ni mtu mwenye furaha daima, napenda sana muziki, naona kupiga fidla ni jambo la kunifurahisha. Lakini huku naelewa kwamba watu wengi wanakuwa na matatizo mengi wanapojifunza, kwani hakuna mwanamuziki asiyewahi kukutana na matatizo, cha muhimu ni namna ya kukabiliana na matatizo hayo? Kwanza lazima uwe na msukumo, na msukumo huo ni kitu ambacho mwanamuziki anakitafuta katika miaka yake yote. Mwanamuziki akiwa amepoteza hamu yake na juhudi za kutafuta msukumo huo, basi hatakuwa mwanamuziki tena, ni afadhali astaafu."

Muziki anaopiga Bw. Lin Zhaoliang unavutia kwa sauti laini na kuonesha hisia za ndani ya muziki. Kila anapojitokeza tu jukwaani huonekana mwenye tabasamu na uchangamfu, na watazamaji wote wanaona wako karibu naye. Alisema ni bora mwanamuziki awe karibu na watazamaji. Ni matumaini yake kuwa kila maonesho yake yanaweza kuwaletea furaha watazamaji wake. Alisema,

"Ninapenda muziki wa aina nyingi ikiwa ni pamoja na muziki wa kale na wa kisasa, ninapopiga muziki wa zama fulani ni matumaini yangu kuwa naweza kuwafahamisha watazamaji ufahamu wangu kuhusu mtunzi wa muziki niliopiga, na ufahamu huo ni matokeo baada ya kuchuja tena na tena, na hii ndio furaha yangu. Wanamuziki wanapopiga muziki mmoja wanatofautiana kutokana wanavyopiga muziki, hakuna mwanamuziki anayepiga muziki sawa na mwingine."

Katika miaka zaidi ya ishirini iliyopita Bw. Lin Zhaoliang amekubalika duniani kuwa ni mpiga filda mashuhuri duniani. Alipozungumzia fikra zake alizopata katika muda huo alisema,

"Ustadi wa kupiga fidla ni kitu muhimu sana, kama huna au ustadi wako hautoshi huwezi kupiga vizuri, lakini ukiniuliza katika muziki wangu ninatilia mkazo katika ustadi au muziki wenyewe nakuambia natilia mkazo muziki wenyewe. Ustadi ni sehemu tu ya muziki lakini sio lengo la mwisho. Ukiwa mwanamuziki unapaswa kuingiza hisia zako miyoni mwa watazamaji kwa muziki wako."

Bw. Lin Zhaoliang ana matumaini kuwa wanamuziki wengi zaidi wa China watajulikana duniani kwa muziki wao unaowavutia wasikilizaji wa nchi mbalimbali.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-27