Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-27 15:00:10    
Uchaguzi mkuu wa Zimbabwe utakuwa na mabadiliko mengi

cri

Tarehe 29 Zimbabwe itafanya uchaguzi mkuu, uchaguzi wa bunge na uchaguzi wa serikali za mitaa. Uchaguzi huo unafanyika katika hali ambayo uchumi wa nchi hiyo umedumaa kwa miaka saba mfululizo, na kuwekewa vikwazo na nchi za magharibi kwa miaka mingi, kwa hiyo matokeo ya uchaguzi huo yatakuwa na athari kubwa kwa mustakbali wa Zimbabwe. Maelezo kutoka tume ya uchaguzi yanasema kwamba wapiga kura waliojiandikishwa ni milioni 5.6, na kuna vituo 9,000 vilivyoenea kwenye sehemu mbalimbali, hivi sasa wachunguzi wa uchaguzi huo kutoka nchi zaidi ya 40 wamefika kwenye nafasi zao za kazi, na maandalizi yote yamekamilika.

Kwa kiasi kikubwa uchaguzi huo utaamua mustakbali wa Zimbabwe, na pia utawaletea matumaini makubwa ya kimaisha watu wa Zimbabwe ambao wanaishi katika matatizo mengi kutokana na uhaba wa mahitaji ya kimaisha. Mwezi Desemba mwaka jana chama tawala ZANU kiliitisha mkutano maalumu na kumpendekeza rais wa sasa Bw. Robert Mugabe awe mgombea pekee wa chama hicho na kuwa rais kwa kipindi cha 6 mfululizo. Kutokana na makadirio ya wakati huo, uchaguzi huo usingekuwa na wasiwasi kwa sababu chama cha upinzani kilikuwa hakijapanga kushiriki kwenye uchaguzi huo. Lakini tarehe 5 Februari mwaka huu aliyekuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya chama tawala na mbunge ambaye pia alikuwa ni waziri wa fedha na uchumi Bw. Simba Makoni bila kutarajiwa alitangaza kushiriki kwenye uchaguzi huo wa urais akiwa mgombea huru, na anaungwa mkono na watu wa ndani na nje ya chama ZANU. Hivi sasa Bw. Simba Makoni amekuwa mpinzani mkubwa wa rais Robert Mugabe.

Kati ya watu wanne wanaogombea kiti cha urais, licha ya rais wa sasa Robert Mugabe na Simba Makoni, pia wapo kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC, Bw. Morgan Tsvangirai na kiongozi wa chama kingine cha upinzani cha Umoja wa Chama cha Umma, lakini ametamgaza kuwa anamwunga mkono Bw. Simba Makoni, kwa hiyo kwa yeye ni sawa kujitoa kwenye uchaguzi huo. Kutokana na hali ilivyo sasa na maoni ya raia, wagombea hao watatu wanalingana kwa kiasi cha uungaji mkono, kwa hiyo wote hao watatu wanaweza kushinda kwenye uchaguzi huo, kwa hiyo ushindani kwenye uchaguzi huo utakuwa mkubwa.

Bw. Robert Mugabe aliyezaliwa miaka 84 iliyopita anaendelea kuwa na ushawishi mkubwa kwenye uchaguzi huo. Tokea mwaka 1980 Zimbabwe ilipopata uhuru, Bw. Robert Mugabe amekuwa rais mpaka sasa, na ni rais mwenye miaka mingi kabisa madarakani kati ya marais wote barani Afrika. Ingawa Bw. Rogert Mugabe anakabiliwa na changamoto kubwa katika uchaguzi huo lakini anajiamini kuwa atashinda. Ilani yake ya uchaguzi huo inaendelea kuwa ni uhuru wa kitaifa ikionesha hatasujudi asilani kwa shinikizo kutoka nje na kutaka kupambana na nguvu za magharibi hadi mwisho. Watu wanaomwunga mkono ni wakulima na makabila mengi nchini Zimbabwe, wanamshukuru kwa kuwaokoa kutoka kwenye unyanyasaji wa wakoloni, na moyo wao wa uzalendo ni mkubwa.

Mgombea huru waziri wa fedha na uchumi Bw. Simba Makoni ni mmoja wa wazee wa chama tawala ZANU, ingawa hivi sasa amefukuzwa na chama chake, lakini anaungwa mkono na watu wengi, zaidi ya hayo chama cha upinzani MDC pia kinamwunga mkono, kwa hiyo mgombea huyo anaungwa mkono na pande nyingi. Ilani ya uchaguzi wa urais ni "kuifanya Zimbabwe iwe na uhai", ilani ambayo inavutia zaidi watu wa Zimbabwe. Anaona kuwa hivi sasa tatizo kubwa lililopo ni kuondoa msukosuko wa kiuchuni nchini Zimbabwe, kuondoa ufisadi na kuunda serikali yenye uadilifu.

Kiongozi wa chama cha upinzani MDC Bw. Morgan Tsvangirai aliwahi kuacha kushiriki kwenye uchaguzi huo kutokana na mfarakano ndani ya chama, lakini baada ya Simba Makoni kutangaza kushiriki kwenye uchaguzi huo na kuona hali imebadilika, anataka pia kushiriki kwenye uchaguzi huo. Ilani yake ni demokrasia na utetezi wa haki za biandamu, akiwa kiongozi wa chama kikubwa cha upinzani anaungwa mkono na nchi za magharibi, waungaji mkono wa mgombea huyo wako zaidi kwenye miji mikubwa. Katika uchaguzi uliopita Bw. Morgan Tsvanigirai alimzidi Robert Mugabe kwa idadi ya kura.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-27