Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-28 15:55:05    
Maandalizi ya uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe yakamilika

cri

Tarehe 29 Marchi Zimbabwe itafanya uchaguzi mkuu, uchaguzi wa bunge na uchaguzi wa serikali za mitaa. Hivi sasa maandalizi yote yamekamilishwa na uchaguzi huo umeanza kupiga hodi. Serikali ya Zimbabwe inataka uchaguzi huo uwe wa haki, uadilifu na utulivu, zaidi ya wito huo serikali imetoa sheria maalumu ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizotolewa na tume ya uchaguzi na polisi, kabla ya uchaguzi huo pande zote haziruhusiwi kufanya shughuli kubwa, na mikutano yoyote ya hadhara isiyopata kibali itakuwa haramu. Katika siku ya uchaguzi nchi nzima itakuwa kwenye mapumziko na kila kituo cha kupigia kura kitalindwa na askari polisi ili kuhakikisha usalama.

Kutokana na maelezo ya tume ya uchaguzi, tarehe 29 wapiga kura milioni 5.6 watapiga kura zao kwenye vituo zaidi elfu tisa. Kama hakuna mgombea wa urais atakayepata zaidi ya nusu ya kura, duru ya pili ya uchaguzi itafanyika tena ndani ya wiki tatu. Vyombo vya habari vinaona kuwa uchaguzi huo wa Zimbabwe unafuatiliwa sana, kwa sababu:

Kwanza, uchaguzi kama huo unaohusisha chaguzi tatu kwa pamoja haujawahi kutokea kusini mwa Afrika. Ili kuufanya uchaguzi huo uwe halali, mwezi Septemba mwaka jana bunge la Zimbabwe lilirekebisha katiba, na katiba hiyo imepitishwa na imeanza kutekelezwa mwezi huu. Chama tawala ZANU PF kilisema kufanya chaguzi tatu kwa pamoja ni kwa ajili ya kuokoa fedha za umma, hivi sasa Zimbabwe iko katika hali mbaya kiuchumi, hakuna haja ya kuwachosha na kuwagharimu wananchi kwa kufanya uchaguzi mara kadhaa. Chama cha upinzani MDC ingawa kiliwahi kupinga kufanya chaguzi tatu kwa pamoja, lakini mwishowe kimekubali ushauri wa chama tawala.

Pili, rais wa sasa Bw. Robert Mugabe ametangaza kutaka kuendelea kuwa rais, hilo jambo linafuatiliwa ndani na nje ya Zimbabwe. Bw. Robert Mugabe aliyezaliwa miaka 84 iliyopita ni rais aliyekaa madarakani kwa miaka mingi kabisa barani Afrika. Mwezi Desemba mwaka jana chama ZANU kilifanya mkutano maalum wa bunge na kumpendekeza awe mgombea pekee wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2008. Mzee Robert Mugabe hapo awali alishiriki kwenye mapambano ya kuipigia uhuru Zimbabwe, mwezi Aprili mwaka 1980 akawa waziri mkuu baada ya Zimbabwe kupata uhuru. Mwaka 1987 Zimbabwe ilirekebisha katiba na kugeuza mfumo wa utawala wa waziri mkuu kuwa mfumo wa utawala wa rais, Bw. Robert Mugabe akawa rais na kuendelea na madaraka mpaka sasa, kwa ujumla amekuwa madarakani kwa miaka 28.

Mwaka 2000 Bw. Robert Mugabe alianza kutekeleza mageuzi ya umiliki wa ardhi, hatua yake ya kutaifisha ardhi ya Wazungu iligusa maslahi ya Uingereza na nchi nyingine za magharibi nchini Zimbabwe, na kusababisha malalamiko mengi. Mwaka 2002 baada ya uchaguzi mkuu kufanyika, nchi za Marekani na Uingereza zilimshutumu Bw. Robert Mugabe kwa kufanya udanganyifu kwenye uchaguzi na kuanza kuiwekea Zimbabwe vikwazo vikali na kusababisha uchumi wa nchi hiyo kuwa na hali mbaya. Mwezi Desemba mwaka 2003 kutokana na kushawishiwa na Uingereza, mkutano wa viongozi wa Jumuyia ya Madola uliisimamisha Zimbabwe uanachama wa jumuyia hiyo. Baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2005 Uingereza ilitangaza kuwa haitambui matokeo ya uchaguzi. Safari hii Bw. Robert Mugabe kushiriki kwenye uchaguzi hakika ni kuwakatisha tamaa watu waliokuwa wanatumaini Robert Mugabe aondoke madarakani. Kutokana na hali ilivyo sasa Bw. Robert Mugabe bado ana ushawishi mkubwa.

Cha kuvutia zaidi ni kuwa mgombea huru aliyekuwa waziri wa fedha na uchumi alitangaza ghafla kuwa atashiriki kwenye uchaguzi huo mwezi mmoja tu uliopita, na amekuwa mpinzani mkubwa dhidi ya Bw. Robert Mugabe. Hivi sasa barabara zote zimebandikwa makaratasi ya manjano ya kumwunga mkono. Na kiongozi wa chama cha upinzani MDC Bw. Morgan Tsvangirai ni mgombea mwingine wa urais. Bw. Tsvangirai ana msimamo wa kupendelea nchi za magaharibi na mara kwa mara anaisumbua tume ya uchaguzi kwa kusema chama tawala kinafanya udanganyifu.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-28