Mjumbe wa kudumu wa ofisi ya siasa ya Kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China Bw. Li Changchun ambaye yuko ziarani nchini Tunisia tarehe 30 Machi alitembelea Kituo cha utamaduni na michezo cha vijana cha El Menzah ambacho kilijengwa kwa msaada wa China.
Bw. Li Changchun alipofika kwenye kituo hicho, alikaribishwa kwa uchangamfu na vijana na chipukizi wa huko. Kituo cha utamaduni na michezo cha vijana cha El Menzah kilizinduliwa mwezi Juni mwaka 1990, kimekuwa kituo muhimu zaidi cha utamaduni na michezo nchini Tunisia. Kituo hicho kina ukumbi mkubwa wa maonesho ya michezo ya Sanaa, maktaba ya vijana na chipukizi, vyumba vya shughuli za utamaduni, madarasa ya jimnastiki na ngoma, uwanja wa mpira wa meza, na jumba la michezo, eneo la kituo hiki ni zaidi ya mita 5200 za mraba. Bw. Li Changchun kwanza alifika kwenye darasa la uchoraji picha na utengenezaji wa Sanaa ya mikono, akitazama watoto walivyochora picha na kutengeneza Sanaa ya mikono na kuzungumza nao.
Unapenda kituo hicho?
Napenda, walimu wetu wote ni wazuri sana.
Unachora picha darasani hapa, je ulitoa ada?
Kidogo tu, kila mwezi ni Dinari 10 tu.
Ni matumaini yangu utajifunza kwa bidii na kuchora vizuri ili uwe mchoraji siku za mbele.
Baadaye, Bw. Li Changchun na msafara wake walikwenda kwenye ukumbi wa kufanyia mchezo wa Wushu, wakitangaza vijana wa Tunisia walivyoonesha mchezo wa Wushu wa China, na walimu wanaofundisha Wushu wote ni watu wanaojitolea kutoka China.
Ulikuja Tunisia lini?
Nimekuwepo hapa kwa mwezi mmoja.
Unatokea wapi?
Guizhou.
Mlikuja wangapi?
Tumekuja wanne kwa pamoja, wote ni walimu wa Wushu.
Kwa niaba ya wananchi wa China tunawashukuru sana, na ni matumaini yetu kuwa mtafanya kazi kwa bidii hapa, na kutoa mchango kwa ajili ya urafiki kati ya China na Tunisia.
Baada ya kutembelea vyumba mbalimbali kwenye kituo hicho, Bw. Li Changchun alisema:
"Nimefurahi sana baada ya kutembelea kituo hicho, kwani nimeona watoto wengi wanafanya shughuli zao kwa furaha hapa, kituo hicho kimekuwa mnara mkubwa wa kuonesha urafiki kati ya China na Tunisia, naona sisi wananchi wa China tumefanya jambo lenye umuhimu mkubwa kwa ajili ya wananchi wa Tunisia. Kwa kufuata hatua nane alizotangaza rais Hu Jintao kwenye Mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka 2006, tutaongeza nguvu ya kufanya kazi kama hiyo".
Bw. Li Changchun alisema, ndani ya miaka mitano, China itatuma watu 300 wanaojitolea kwa nchi mbalimbali za Afrika, kazi za watu hao wanaojitolea zitahimiza kuendeleza urafiki wa jadi kati ya China na Afrika kizazi hadi kizazi. Waziri wa vijana na michezo wa Tunisia aliyeambatana na Bw. Li Changchun katika matembezi hayo Bw. Kaabi Abdallah, pia alisema kwa kupitia kituo hicho, mawasiliano kati ya vijana wa China na Tunisia yatakuwa barabara zaidi. Alisema:
"Katika miaka mingi iliyopita, serikali ya China na wananchi wake wametoa msaada kwa kituo hicho, vijana na chipukizi wa Tunisia wanakuja mara kwa mara kufanya shughuli zao, na kufahamishwa mambo kuhusu China na kuelewa ustaarabu wa China. Kwa kupitia njia hiyo, uhusiano kati ya wananchi wa China na Tunisia, hasa kati ya vijana wa nchi hizo mbili yatakuwa karibu zaidi".
Kwenye daftari la kumbukumbu la kituo hicho, Bw. Li Changchun aliandika maneno yasemayo: "Urafiki kati ya China na Tunisia uendelee kizazi baada ya kizazi".
|