Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-01 16:39:18    
Hadithi ya kubadilisha maafa ya upepo kuwa nishati ya upepo katika wilaya ya Tongyu mkoani Jilin(A)

cri

Msichana aliyeimba wimbo huo anaitwa Baixue, na mwaka huu ana umri wa miaka 12. Ingawa anaimba wimbo uitwao watoto wanaoishi kwenye sehemu yenye mito mingi, yeye hajawahi kuona mto wala maua, anajua kuwa maji ni kitu kinachotakiwa kuthaminiwa tangu alipokuwa mtoto mdogo. Familia ya msichana huyo inaaishi magharibi mwa wilaya ya Tongyu, karibu na mbuga ya Kerqin ambayo inabadilika kuwa jangwa. Katika sehemu hiyo mvua inanyesha mara chache sana, na upepo wenye nishati ya ngazi ya 6 unavuma kwa muda mrefu ukipeperusha mchanga kila mwaka. Wenyeji wa huko wanasema upepo unavuma mwaka mzima kuanzia majira ya mchipuko hadi majira ya baridi.

Mchanga ukipeperushwa na upepo unakaribia kwenye sehemu ya magharibi ya kijiji anachoishi Baixue siku hadi siku. Mashamba yaliyojengwa katika miaka ya 60 karne iliyopita yamefunikwa na mchanga. Na baada ya miaka 40, nyumba za familia zaidi ya 40 zinafunikwa na mchanga hatua kwa hatua. Inazibidi familia hizo zihamie kwenye sehemu ya mashariki ya kijiji hicho. Wilaya ya Tongyu ni wilaya iliyo nyuma zaidi kiuchumi nchini China. Mazingira mabaya ya kimaumbile yamewasababishia wakulima wasipate mavuno, na wastani wa mapato kwa mtu ni mdogo kuliko mstari uliowekwa na serikali. Katika miaka ya 90 karne iliyopita, maofisa wa shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa waliona kuwa wilaya hiyo ni moja ya sehemu ambazo hazifai kuishi kwa binadamu duniani.

Mababu za Baixue wote waliishi kijijini humo. Mchanga ukifunika mashamba tena, wao walipanda mazao tena. Watu wa huko wanapambana na mazingira mabaya kizazi baada ya kizazi. Katika miaka mingi iliyopita, upepo mkubwa mwenye mchanga unawasumbua watu wa Tongyu. Kila mwaka serikali ya wilaya ilitenga fedha kwa ajili ya kupanda miti ya kuzuia upepo, lakini upepo unapeperusha mchanga haraka zaidi kuliko ukuaji wa miti, tena kupanda miti mingi ni kazi ngumu kwa wilaya ambayo iko nyuma kiuchumi. Mazingira mabaya na maisha magumu yaliwafanya watu wa huko wasikitishwe na mustakabali wao, lakini hawakati tamaa kuhusu watoto wao na maisha mazuri katika siku za usoni.

Mhandisi mkuu wa idara ya utoaji wa umeme kwa kilimo ya wilaya ya Tongyu Bw. Gu Tiezheng alizaliwa na kukua wilayani humo. Alipokuwa mtoto alijifunza kwa bidii, baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu alirudi kwenye maskani yake. Tofauti kubwa kati ya miji mingine na kijiji hicho ilimfanya aone kuwa ni jukumu lake kufanya mambo fulani kwa wanakijiji wa kijiji hicho. Mwaka 1992 Bw. Gu aliona kwenye gazeti moja kuwa nchi za nje zimetengeneza mitambo midogo ya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo. Alijua kuwa mitambo mikubwa ya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo itatengenezwa katika muda usio mrefu. Kutokana na upepo mkubwa wilayani Tongyu, alianza kufikiria kama kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo kinaweza kujengwa huko.

Pendekezo lake liliungwa mkono na idara za hali ya hewa na idara ya umeme za wilaya hiyo. Waliomba wataalamu wa idara ya umeme ya China kuchunguza nishati ya upepo ya huko. Mwaka 1997 takwimu zilitolewa, ambazo zinaonesha kuwa kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo kinafaa kujengwa huko. Bw. Gu alisema,

"Tulipopata matokeo hayo, tulifurahi sana, kwa sababu matumaini ya watu wa Tongyu ni kujengwa kwa kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo."

Mwaka 1997, serikali ya mji wa Baicheng iliamua kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo kwenye wilaya ya Tongyu ambayo ardhi ya huko ni yenye rutuba hafifu zaidi. Lakini ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme unahitaji uwekezaji mkubwa, na fedha zilizotolewa na serikali kuu hazikutosha. Bi. Tian Xiuhua na Bw. Yu Bin wanaoshughulikia mradi huo walitafuta uungaji mkono wa kifedha wa makampuni mbalimbali ya umeme, lakini kutokana na uwekezaji mkubwa wa kituo cha kuzalisha umeme na hali ya wilaya ya Tongyu, makampuni mengi ya umeme hayakuthubutu kuwekeza kwenye mradi huo. Bi. Tian Xiuhua alisema?

"Tulitafuta makampuni mbalimbali na kuyaomba yawekeza hapa, hapa kuna nishati nyingi ya upepo."

Bw. Yu Bin alisema,

"Lakini walisema mradi huo ni mgumu sana, ambao utawabidi watekeleze wajibu mkubwa, na ni vigumu kufanya kazi hiyo."

Mwaka 1998 kutokana na juhudi zao, kampuni ya umeme ya mkoa wa Jilin iliunda kampuni maalum ya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo wilayani Tongyu, na kupanga kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo chenye uwezo wa kuzalisha umeme kilowati elfu 30. Ili kuhimiza maendeleo ya nishati zisizochafua mazingira, nchi zilizoendelea zinatoa mikopo kati ya serikali yenye riba nafuu kwa nchi zinazoendelea. Mradi huo ulipata mikopo ya dola za kimarekani milioni 5 kutoka serikali ya Hispania. Baada ya kupata fedha hizo, mradi wa kipindi cha kwanza ulianzishwa kwa mafanikio. Lakini inakadiriwa kuwa mradi wa vipindi vilivyofuata bado ulihitaji fedha nyingi, je wangepata wapi fedha hizo?

Ili kuhakikisha mradi huo unamalizika, kampuni ya umeme ya mkoa wa Jilin iliamua kukusanya fedha kwa kuwauzia hisa wafanyakazi wa makampuni ya umeme mkoani humo. Wafanyakazi wa kampuni ya umeme wa wilaya ya Tongyu wana matumaini makubwa kuhusu mstakabali wa mradi huo walipoona ujenzi wa mradi wa kipindi cha kwanza, lakini walikuwa na mashaka kuhusu kununua hisa za mradi huo, kwa sababu hawajawahi kutumia fedha zao kuwekeza kwenye miradi, tena mradi huo ni mkubwa sana kwa wilaya ya Tongyu ambayo iko nyuma kiuchumi. Hivyo watu wote waliangalia msimamo wa Bw. Gu TieZheng.

Katika kipindi cha wiki ijayo, tutaendelea kuwaelezea hadithi ya kubadilisha maafa ya upepo kuwa nishati ya upepo katika wilaya ya Tongyu mkoani Jilin, ili tujue kama Bw. Gu TieZheng alifaulu kuwashawishi wafanyakazi wenzake kununua hisa kwa hiari, na kama kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo kitaweza kujengwa kwa mafanikio?