|
Mazungumzo ya duru jipya ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa yalianza tena tarehe 31 mjini Bangkok. Hayo ni mazungumzo ya kwanza kufanyika baada ya "Ramani ya Bali" iliyopitishwa mwezi Desemba kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa. Mkutano huo unaofanyika sasa mjini Bangkok utajadili namna ya kutekeleza "Ramani ya Bali" na kuweka mpango halisi kuhusu mazungumzo yatakayofanyika baadaye. Licha ya hayo, mkutano huo utahimiza nchi zilizoendelea zitekeleze ahadi zao.
Wajumbe kutoka kundi la nchi 77 zinazoendelea na mjumbe wa China walitaka nchi zilizoendelea zipunguze uchafuzi kwa mujibu wa kanuni ya "jukumu kwa wote lakini litekelezwe kwa namna tofauti", kanuni ambayo imewekwa kwenye "Makubaliano ya Kimsingi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa". Mkuu wa Ofisi ya Uongozi wa Kupambana na Mabadiliko ya Hali ya Hewa nchini China Bw. Su Wei kwenye mkutano huo alisema nchi zilizoendelea zina jukumu na pia zina uwezo wa kupunguza uchafuzi. Alisema,
"Kwa mujibu wa ripoti ya nne iliyotolewa na kamati ya kimataifa ya kiserikali kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, IPCC, katika mwaka 2004 wastani wa kutoa hewa ya carbon dioxide kwa mtu moja kwenye nchi zilizoendelea ni tani 16.1, nchi zilizoendelea zina jukumu na uwezo wa kupunguza uchafuzi kwa mujibu wa "Mkataba wa Kyoto". China inaunga mkono ripoti ya nne ya IPCC kwamba nchi zilizoendelea zipunguze kwa 25 hadi 40% ya uchafuzi wa mwaka 1990 baada ya mwaka 2012."
Bw. Su Wei alisema nchi zilizoendelea zinatakiwa zipunguze uchafuzi kwa kuchukua hatua ndani ya nchi, ni kwa kufanya hivyo tu ndipo nchi hizo zinaweza kuwa mfano wa kuigwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa. Kwenye mkutano na waandishi wa habari Bw. Su Wei alisema, kwa kuzingatia historia, nchi zilizoendelea zinawajibika zaidi kupunguza uchafuzi, na kwa kuzingatia hali ya sasa uchafuzi unaotolewa na nchi zinazoendelea pia ni mwingi. Kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa ndani ya "Makubaliano ya Kimsingi kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa" nchi zilizoendelea zinatakiwa kutangulia kupunguza uchafuzi na nchi zinazoendelea pia zinatakiwa kupunguza uchafuzi kwa msingi wa kuhakikisha maendeleo endelevu, na pamoja na hayo nchi zilizoendelea zinatakiwa kuzisaidia nchi zinazoendelea kwa teknolojia.
Kutokana na kuwa nchi fulani zilizoendelea zilitoa asilimia ya kupunguza uchafuzi kwa mujibu wa uzito wa uchafuzi uliotolewa mwaka 2005 badala ya mwaka 1990, Bw. Yvo de Boer alieleza kuwa mkutano huo unajadili zaidi kiasi cha kupunguzwa. Alisema,
"Naona kujadili suala hili ni kama mbio za marathon, kwamba kuna mwanzo wake lakini mwisho wake haujulikani, mkutano huu utajadili tu kila nchi itapunguza kiasi gani cha uchafuzi, kama nchi fulani haikubali kupunguza asilimia ya uchafuzi kwa mujibu wa uzito uliotolewa mwaka 1990 basi inatakiwa kubadilisha mwanzo wa safari ya marathon."
Kutokana na kuwa kipindi cha kwanza cha utekelezaji wa "Mkataba wa Kyoto" kinamalizika mwaka 2012, kwa mujibu wa mkataba huo nchi zilizosaini mkataba huo zinapaswa kuzungumzia namna ya kutimiza ahadi za kipindi cha pili. Hivi sasa kikundi cha kuandaa mazungumzo hayo kimeanza maandalizi hayo. Mjumbe wa jumuyia isiyo ya serikali CAN kwenye mkutano alizitaka nchi zote zichukue hatua mara moja kupunguza uchafuzi na kupunguza kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa. Alisema,
"Tusisubiri mpaka kesho, leo tu tuanze. Kukumbukeni ongezeko la joto kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa litafikia kileleni baada ya miaka kumi, hakuna sababu yoyote ya kuchelewesha, chukueni hatua mara moja."
Idhaa ya kiswahili 2008-04-01
|