Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-02 17:14:21    
Mkoa wa Fujian wajitahidi kukamilisha utaratibu wa bima ya matibabu ya kimsingi kwa wakazi wa mijini

cri

Katika miaka ya hivi karibuni, China imeanzisha na kueneza hatua kwa hatua utaratibu wa bima ya matibabu ya kimsingi kwa wafanyakazi mijini na utaratibu wa aina mpya wa ushirikiano wa matibabu vijijini, na hatua hizo zimetoa uhakikisho kwa wafanyakazi mijini na wakazi wa vijijini katika suala la matibabu. Lakini kwa wakazi wa mijini wasio na pato, hasa wazee, watu wenye pato la chini, walemavu na watoto, je ni vipi wataweza kuhakikisha watu hao pia wanapata matibabu kama ipasavyo?

Bi. Chen Xiang anayeishi mjini Xiamen mkoani Fujian ana umri wa miaka zaidi ya 80. Mwanzoni mwa mwaka huu, aligunduliwa kupatwa saratani ya sehemu ya mwisho ya utumbo mkubwa (rectum). Hali hiyo ilikuwa ni pigo kubwa kwa familia hiyo ambayo hali yake ya kiuchumi si nzuri. Mke wa mtoto wa mzee huyo Bi. Zheng Zhenzhen aliyemwangalia na kumtunza alipokumbuka hali ya wakati huo alisema:

"kuwa na mzee mgonjwa kwa familia yetu ni mzigo mkubwa, mimi na mume wangu sote tulipunguzwa kazini. Gharama za matibabu ya hivi sasa ni kubwa sana, hata sisi hatuwezi kumudu gharama zake za matibabu hospitalini."

Wakati familia hiyo ilipoingiwa na wasiwasi mkubwa, utaratibu wa bima ya matibabu kwa wakazi wa mjini ulikuwa umewaletea matumaini. Imefahamika kuwa kuanzia mwaka 2001 mkoa wa Fujian ulianzisha utaratibu wa bima ya matibabu kwa wafanyakazi mijini na utaratibu wa aina mpya wa ushirikiano wa matibabu vijijini kwenye sehemu mbalimbali mkoani humo, na hatua hizo zimetatua kimsingi tatizo la gharama za matibabu kwa wafanyakazi mijini na wakazi wa vijijini. Ili kuweza kuwanufaisha wakazi wote kutokana na utaratibu wa bima ya matibabu ya jamii, kuanzia mwaka jana, mkoa huo ulianza kutekeleza kwa majaribio utaratibu wa bima ya matibabu kwa wakazi wa mijini kwenye miji mitatu ya Fuzhou, Xiamen na Nanping. Naibu mkurugenzi wa idara ya kazi na huduma za jamii ya mkoa wa Fujian Bw. Lai Shiqing alisema:

"utaratibu huo unakusanya fedha kutoka kwa serikali na watu binafsi, unatilia maanani katika kutatua suala la matibabu kama wanachama wakilazwa, au kupatwa magonjwa makubwa. Utaratibu huo una umaalumu kadhaa ufuatao, kwanza utaratibu huo unawafikia watu wa makundi mbalimbali, wakiwemo wakazi wote wasio na ajira; pili, utaratibu huo una njia nyingi za kukusanya fedha, kwa kawaida utakusanya fedha kutoka kwa serikali na kwa watu binafsi, na pia unaweza kuchangisha fedha katika jamii."

Bw. Lai Shiqing alisema, kabla utaratibu huo haujaanzishwa, gharama za matibabu kwa wakazi wa miji wasio na ajira kama vile watoto na wazee zilikuwa zinalipiwa na familia zao. Kama wakipatwa na magonjwa makubwa, familia zao zitakuwa na shinikizo kubwa la kiuchumi. Bw. Lai Shiqing alisema, kuanzishwa kwa utaratibu wa bima ya matibabu kwa wakazi wa mijini kumetatua kimsingi suala la uhakikisho wa matibabu kwa watu hao wakipata magonjwa makubwa.

Kwa mujibu wa takwimu husika, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, watu wapatao laki saba wa miji ya Fuzhou, Xiamen na Nanping walijiunga na utaratibu huo, na mzee Chen Xiang pia ni mmoja wao. Mkurugenzi wa kituo cha usimamizi wa bima ya jamii ya mji wa Xiamen Bw. Jiang Gengsheng alisema, asilimia 40 hadi 60 ya gharama za matibabu ya wanachama wa utaratibu huo zinalipwa na serikali ya huko, na kiwango hicho pia kitainuka zaidi katika siku za baadaye. Bw. Jiang Gengsheng alisema:

"wanachama wa utaratibu huo wananufaika kidhahiri katika upunguzaji wa gharama za matibabu. Kwa mujibu wa takwimu zetu, kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini, gharama za matibabu zitapunguzwa kwa asilimia 47 kwa wakazi wazee, na asilimia 55 kwa watoto. Hayo ni manufaa halisi hasa kwa wakazi hasa katika kuwapunguzia mzigo wa matibabu."

Kwa upande mwingine, watu wanatakiwa kulipa pesa kidogo tu ili kujiunga na utaratibu huo. Kwa mfano, mjini Xiamen kila mwanachama anatakiwa kulipa Yuan 178 tu kwa mwaka, kwa vijana walio chini ya miaka 18 wanatakiwa kulipa Yuan 80 tu kwa mwaka. Mbali na hayo, makundi maalum ya watu kama vile watu wenye pato la chini na walemavu, wanasemehewa au kupunguziwa zaidi malipo yao. Mwuguzi mkuu wa hospitali moja ya mjini humo Bi. Li Sumin alisema, kuanzishwa kwa utaratibu wa bima ya matibabu kwa wakazi wa mijini kunawanufaisha watu wasio na uhakikisho wowote wa matibabu. Bi. Li Sumin alisema:

"bila utaratibu huo, watu wengi watakuwa hawamudu gharama za matibabu hospitalini. Sasa utaratibu huo unatekelezwa mjini Xiamen, umezipunguzia mzigo mkubwa wa kiuchumi familia zenye matatizo ya kiuchumi na watu waliopatwa na magonjwa makubwa."

Naibu mkurugenzi wa idara ya kazi na huduma za jamii ya mkoa wa Fujian Bw. Lai Shiqing alisema, kuanzia mwezi Aprili mwaka huu, utaratibu wa bima ya matibabu kwa wakazi wa miji utatekelezwa kote mkoani humo. Kwa hivyo mkoa wa Fujian umetimiza lengo la kunufaisha kila mtu kwenye kila sehemu kwa bima ya matibabu mkoani humo. Miji mitatu ya Fuzhou, Xiamen na Nanping ya mkoa wa Fujian ni mfano tu kuhusu China kusukuma mbele utaratibu wa bima ya matibabu mijini. Hivi sasa utaratibu huo umeanzishwa kwenye miji 79 kote nchini China. Kwa mujibu wa mpango wa serikali, ifikapo mwaka 2010 utaratibu huo utaenezwa kote nchini China.

Idhaa ya kiswahili 2008-04-02