Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-01 18:42:18    
China yahimiza ushirikiano wa eneo dogo la mto mkubwa Mekong

cri

Kutokana na mwaliko wa waziri mkuu wa Laos Bw. Bouasone Bouphavanh, waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alifanya ziara nchini Laos na kuhudhuria mkutano wa 3 wa viongozi wa ushirikiano wa eneo dogo la mto mkubwa Mekong(GMS) uliofanyika mjini Vientiane kuanzia tarehe 29 hadi tarehe 31 mwezi Machi. Katika siku hizo mbili, waziri mkuu Wen Jiabao alishiriki kwenye shughuli zaidi ya 20. Alisema serikali ya China inaendelea kutekeleza sera za kidiplomasia za urafiki na nchi jirani, inashiriki na kuhimiza ushirikiano kwenye eneo hilo, na inapenda kushirikiana na nchi zote za eneo hilo kujenga eneo hilo kuwa na masikilizano na ustawi zaidi.

  

Katika ziara hiyo waziri mkuu Wen Jiabao alikuwa na mazungumzo kwa nyakati tofauti na waziri mkuu Bw. Bouasone Bouphavanh na rais Choummaly Saygnasone wa Laos. Bw. Wen Jiabao alitoa mapendekezo ya kuimarisha uaminifu wa kisiasa, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, pamoja na maingiliano ya watu ili kuimarisha uhusiano kati ya China na Laos. Waziri mkuu wa Laos Bw Bouasone Bouphavanh alikaribisha mapendekezo hayo, na kutarajia kuwa nchi hizi mbili zitapata maendeleo makubwa zaidi katika kuhimiza urafiki na ushirikaino wa nchi mbili. Alisema,

"Tunapongeza sana ziara hiyo ya waziri mkuu Wen Jiabao nchini Laos, tunawashukuru waziri mkuu na ujumbe wa China kushiriki kwenye mkutano huo wa GMS. Ninapenda kuungana na wewe kuhimiza uhusiano wa urafiki wa jadi wa nchi hizi mbili."

Kwenye mkutano huo wa GMS, Bw. Wen Jiabao alitoa hotuba akieleza mtizamo wa China kuhusu ushirikiano na mustakabali wa GMS, na kutoa mapendekezo na hatua kuhusu maendeleo ya ujenzi wa miundo-mbinu, biashara, usafirishaji wa bidhaa, mambo ya afya na raslimali ya nguvu-kazi. Alisema mkutano huo umefuata wazo la "kuimarisha uhusiano na nguvu za ushindani", kushikilia mambo muhimu ya ushirikiano wa GMS na kuonesha matarajio ya pamoja ya nchi mbalimbali. Alisema ni kwa kushikilia mtizamo wa ushirikiano wa kunufaishana na kuimarisha maingiliano ya ngazi mbalimbali na kwenye maeneo mbalimbali tu, ndipo nchi za eneo hilo zitaweza kuhimiza ushirikiano wa GMS hadi kufikia kiwango kipya na kunufaisha zaidi watu wa eneo hilo. Katika ziara yake Bw. Wen Jiabao alishiriki kwenye mazungumzo kati ya viongozi na vijana pamoja na wawakilishi wa sekta za viwanda na biashara, pamoja na sherehe ya uzinduzi wa ujenzi wa kipindi cha kwanza wa mawasiliano ya habari ya GMS. Alipokuwa na mazungumzo na wawakilishi wa vijana Bw. Wen Jiabao alisema, serikali ya China itafanya mambo mawili kwa ajili ya vijana wa nchi zote za eneo hilo.

 

"La kwanza ni kuwa, kuanzia mwaka 2008 tutaongeza nafasi 200 za kusoma katika vyuo vikuu vya mikoa mitatu ya China kwa vijana wa nchi za eneo la GMS; Pili, umoja wa vijana wa China utawashirikisha vijana kushiriki kwenye shughuli za maingiliano kwenye sehemu ya mtiririko wa mto Mekong. Wanaweza kutalii kwa kutumia meli, kufahamu hali ya maumbile ya eneo hilo na kuimarisha urafiki, maelewano na uaminifu kati yao."

Waziri mkuu Wen Jiabao alipokuwa na mazungumzo na wawakilishi wa sekta za viwanda na biashara alisema, katika miaka mitatu ijayo, China itaongeza maradufu idadi ya watu wanaoshiriki kwenye mafunzo yanayotolewa chini ya mpango wa ushirikiano wa uchumi wa GMS, na itabuni miradi mingine mingi na mizuri zaidi ya mafunzo. Kuhusu ujenzi wa miundo-mbinu ya eneo hilo, Bw. Wen Jiabao alisema serikali ya China itaendelea kutoa mchango kwa ujenzi wa miundo mbinu yakiwemo mawasiliano ya habari kwa eneo hilo,alisema,

"Kuharakisha ujenzi wa miundo-mbinu ya mawasiliano wa habari na kuimarisha ushirikiano wa sekta ya upashanaji habari kwenye eneo la GMS ni mahitaji na matarajio ya nchi zote za eneo hilo. China itashirikiana na nchi zote pamoja na benki ya Asia kuweka mpango wa kuanzisha ujenzi wa kipindi cha pili."