Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-01 20:27:19    
Barua 0401

cri

Kwanza tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa, kutokana na mpango mpya wa vipindi vyetu vya Idhaa ya Kiswahili, kuanzia wiki iliyopita, kipindi cha Sanduku la barua kinatangazwa kila Jumanne badala ya kila jumapili. Karibuni muendelee kuwa nasi. Sasa tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Mchana J. Mchana wa sanduku la posta 1878 Morogoro Tanzania hivi karibuni ametuletea barua pepe akisema, kwanza anapenda kutoa pongezi kwa watu wote wa China kwa juhudi zao kubwa wanazofanya za kila siku ya kujiletea maendeleo. Pili anatoa pongezi kwa viongozi wa ngazi zote kwa kuhakikisha kero zinazowapata wapiga kura wao wanazishughulikia kwa muda muafaka. Tatu hapendi kuwasahau vinara wa habari, kwani bila wao masuala mengi yanayofahamika leo yasingefahamika, hao ni watangazaji na waandishi wa habari wa Radio China Kimataifa. Nne anatoa pongezi pia kwa rais wa China ambaye pia ni katibu mkuu wa kamati kuu ya Chama cha kikomunisti cha China Hu Jintao na waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao kwa ushirikiano mzuri na wajumbe wa mikoa inayojiendesha, anadhani maazimio yaliyofikiwa yatatekelezwa kwa muda muafaka. Kwani sehemu muhimu zilizozungumizwa ni kama vile, moja ni Utekelezaji wa sera ya serikali, sehemu hii ni muhimu kwani majukumu mazima ni usimamizi wa utekelezaji wa sera viongozi ni muhimu wafahamu wajibu wao. Mbili ni kushughulikia mambo ya makabila na dini, kwa maoni yake anawaomba viongozi wote duniani wahubiri kwa nguvu zao zote na washirikiane ili kuutokomeza kabisa ukabila na udini, kwani ni ugonjwa hatari kama ukoma, jambo hili lisipokemewa dunia itanuka damu, kwa hiyo anashukuru viongozi wa mikutano mikubwa ya China wameliona hili. Na tatu linahusu China bara na Taiwan, wito wake kwa viongozi wa pande mbili hizi ni kuongeza zaidi mshikamano na utekelezaji wa ahadi na kutatua tofauti pale zinapojitokeza. Penye upendo amani hutawala. Mwisho anawatakia kila la heri wajumbe walioshiriki kwenye kuyafanyia kazi maamuzi yaliyoamuliwa na vikao hivi viwili.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mchana J. Mchana kwa barua yake ya kupongeza mikutano miwili ya mwaka ya Bunge la umma la China na Baraza la mashauriano ya kisiasa ya China iliyofanyika hivi karibuni, usikivu wake wa makini unatutia moyo na kutuhimiza kuchapa kazi zaidi ili kuwafurahisha wasikilizaji.

Msikilizaji wetu Nazael Piniel wa sanduku la posta 30 Mto wa mbu Arusha Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, salamu nyingi na pongezi zitufikie waandaaji wote pamoja na watangazaji wote wa Radio China Kimataifa kwa kuandaa kipindi kizuri cha kujifunza Kichina, ni matumaini yake sisi sote hatujambo, na ameandika kwa kichina nimenhao?hamjambo, hatujambo asante sana.

Anasema anapenda kusema kwamba anafuraha ya kwamba masomo ambayo tumemtumia amekwisha kuyasoma yote na anaweza kuyatamka vizuri kabisa, Ingawa siyo yote ambayo si wazi kuyatamka ni machache . Na pia anawafundisha wenzake ili wapate uzoefu wa kuongea zaidi. Anasema yeye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Enaboishu iliyopo Arusha Tanzania. Yeye yupo shule ya bweni, hivyo si muda wote anaweza kusikiliza radio mpaka wakati wa likizo. Anaomba kama kuna uwezekano tumtumie masomo mengine pamoja na picha zinazoonesha mandhari ya China pamoja na kanda ya nyimbo za kichina.

Tunamshukuru msikilizaji wetu Nazael Piniel kwa barua yake ya kueleza maoni yake kuhusu kipindi chetu cha jifunze Kichina. Kutokana na sababu mbalimbali, mwezi huu mpango wa vipindi vyetu kuna mabadiliko fulanifulani, kipindi hiki cha jifunze Kichina kinatangaza zaidi kwenye matangazo yetu ya FM 91.9 Naierobi Kenya, na kuanzia mwezi Mei mwaka huu, tutarekebisha vizuri mpango wetu, na kipindi cha jifunze Kichina kitatangazwa kwenye matangazo yetu ya kila saa, tunaomba wasikilizaji wetu msikose kutusikiliza.

Msikilizaji wetu Aliyce Mpemba wa sanduku la posta 222 Sengerema Mwanza Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, dhumuni la barua hii ni kutaka kutujulisha kuwa hata yeye amefurahishwa na vipindi vyetu vya Radio China Kimataifa, kwa sababu amefurahishwa na vipindi vyetu na anaahidi kuwa atafuatilia vipindi vyetu vyote vya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Pia anatoa pongezi kwa vipindi vyetu vya salamu hapa studio, kwani ni vizuri hata na yeye amefurahishwa. Pia anatoa pongeza kwa watangazaji wote wa hapo kwani wanajitahidi kutangaza vipindi vyao. Pia atakuwa mwanachama wa kudumu wa Radio China Kimataifa, na pia atawahamasisha marafiki zake wawe wanasikiliza Radio China Kimataifa kwani ina vipindi vizuri. Na ametanguliza shukrani zake za dhati kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, anasema Mungu awabariki watangazaji wote wa Radio China Kimataifa.

Tunamshukuru msikilizaji wetu Aliyce Mpemba kwa barua yake ya kueleza kufurahishwa na vipindi vyetu, hapa tunamkaribisha kwa mikono mwili kuwa msikizaji wetu wa kudumu, ni matumaini yetu kuwa utasikiliza matangazo yetu kwa makini na kutoa maoni na mapendekezo ili kutusaidia kuboresha vipindi ili tuwahudumie vizuri zaidi wasikilizaji wtu.

Msikilizaji wetu Aliy Abdurahm Aliy wa sanduku la posta 2477 Zanzibar Tanzania ametuletea barua akisema, ni matumaini yake kuwa hatujambo na anatupa salamu za mwaka mpya wa 2008. Kwanza anatushukuru sana kwa kadi ya salamu na makala ya chemsha bongo tuliyomtumia ambayo tayari amekwisha jibu maswali yake na kuyatuma kwetu, anatarajia kuwa Allah atamfanya kuwa mmoja wa washindi maalum, ili aje China kuwaona wachina katika nchi yao na mazingira yao.

Pili ni maoni yake kuhusu michezo ya Olimpiki kama kauli mbiu ya safari hii isemayo, "dunia moja na ndoto moja", hivyo anatarajia kuwa michezo ya Olimpiki itakuwa ni ya usawa kwa wote bila ubaguzi. Kila mshindani atakuwa na fursa na bahati sawa ya kushinda medali ingawa anaamini kuwa China itakuwa ni mshindi wa jumla wa michezo hiyo na anategemea kuwa historia itakayowekwa na China katika mashindano haya itachukua miongo kadhaa kufikiwa tena. Vilevile anapendekeza kuwa idhaa ya Kiswahili iandae chemsha bongo nyingine ambayo itawapa washindi fursa ya kuyashuhudia baadhi ya mashindano hayo makubwa ulimwenguni, anamaliza kwa kusema Mungu ibariki China na wabariki wasikilizaji wake.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Aliy Abdurahm Aliy kwa barua yake ya kuitakia China mafanikio mazuri kwenye Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu hapa mjini Beijing. Kama alivyosema, kwa kufuata kauli mbiu ya "dunia moja na ndoto moja" ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, tuna imani kuwa, wachezaji wa nchi mbalimbali kote duniani wanajitahdii kujipatia mafanikio kwenye michezo ya Olimpiki, kwani michezo hiyo itakuwa ni ya usawa kwa wote bila ubaguzi. Siku hizi maandalizi ya kipindi cha mwisho ya michezo hiyo yanafanyika kwa pilikapilika mjini Beijing, hata sisi tumeanza kutangaza kila siku kipindi kipya kuhusu Mbio wa kukimbiza na kupokezana mwenge wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing, na kipindi kipya kuhusu wakimbiza mwenge mbalimbali. Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu watatusikiliza na kutoa maoni na mapendekezo, ili tuandae vipindi vizuri zaidi kuhusu Michezo ya Olimpiki. Tunataka kutoa habari kwa wakati kuhusu Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008, hakika siku hizi mpango wa vipindi vyetu utabadilikabadilika, nia yetu ni kuwafurahisha wasikilizaji wetu. Asanteni.