Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-03 16:40:01    
Mabadiliko ya mavazi ya waislamu nchini China

cri

Mavazi ni kama kumbukumbu ya aina moja na historia inayovaliwa, na mabadiliko ya mavazi yanaonesha mabadiliko ya jamii. Katika maelezo hayo, mwandishi wetu wa habari aliwahoji waislamu wa China wanaotoka makabila tofauti, wakielezea jinsi mavazi ya watu wa China yalivyoendelezwa katika miaka 30 iliyopita.

Naibu mkurugenzi wa Shirika la dini ya Kiislamu la mji wa Lanzhou, mkoani Gansu, China Bw. Su Guanglin alikumbusha hali ya miaka 30 iliyopita, alisema "Miaka 30 iliyopita suti moja ya nguo haikuwa na gharama ya zaidi ya Yuan 10, na kutumika kwa muda wa miaka mitatu na minne, tena nguo zilikuwa zinawekwa viraka. Zamani baraghashia iliuzwa kwa centi kumi na kitu, na iliachwa kutumiwa wakati iliposhindwa kuwekwa kiraka. Nakumbuka siku nyingine baraghashia yangu ilichafuka sana, lakini sikuwa na pesa za kununua sabuni, ilinibidi niazime sabuni kutoka kwa mwanafunzi mwenzangu ili niweze kufua baraghashia yangu."

Bw. Su Guanglin mwenye umri wa miaka karibu 70 ni mbunge wa bunge la umma la China. Yeye ameshuhudia mabadiliko ya China katika miaka 30 iliyopita tangu China ianze kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango. Alikumbusha kuwa, kabla ya sera hiyo kuanza kutekelezwa, China ilikuwa na hali mbaya ya umaskini kiasi kwamba, katika baadhi ya mikoa, watu kadhaa wa familia moja walikuwa wanatumia suruali moja tu, hali hii ilionekana mara kwa mara. Na wakati ule, wanawake kwa wanaume, wazee kwa watoto walikuwa wanavaa nguo za rangi nne tu za kibuluu, nyeupe, nyeusi au kijani, na mitindo ya nguo ilikuwa michache sana, ambapo nguo zilikuwa na kazi pekee tu ya kuhifadhi joto mwilini.

Kuwepo kwa mitindo mbalimbali ya nguo kulianza mwaka 1978 China ilipoanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, ambapo vijana walianza kuvaa kwa kufuata mitindo ya kisasa, kwa mfano suruali pana, makoti yenye mikono mipana na sketi. Wachina walianza kushuhudia mabadiliko ya nguo katika rangi na mitindo. Bi. Halida kutoka kabila la Wauygur alisema "Nakumbuka nilipokuwa mwanafunzi kwenye shule ya sekondari, rafiki mmoja aliniletea kitambaa kimoja cha telerini cha rangi ya pinki kutoka Shanghai, mama yangu alinishonea shati. Niliivaa shati hilo shuleni na kuwavutia watu wengi macho, wakiniambia 'unapendeza kweli'. Wakati huo nilijivuna sana."

Katika kipindi hicho kitambaa hicho cha kemikali telerini kilipendwa sana na wachina kutokana na sifa zake mbalimbali, kama vile kitambaa chepesi, ambacho kina uwezo mkubwa wa kupitisha hewa na ni rahisi kusafisha. Hadi kufikia miaka ya 90 ya karne iliyopita, maendeleo ya sekta ya nguo ya China yalikuwa yameweza kwenda sambamba na maendeleo ya sekta hiyo duniani, ambapo vitambaa vya asili kama vile vya pamba na hariri vilianza kuwavutia wachina zaidi kuliko vile vya kemikali.

Asghar Turson wa kabila la Wauygur alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, wakati ambapo yeye alikuwa miongoni mwa kundi la watu waliokuwa wanapenda mitindo ya kisasa ya nguo. Alisema "Nilipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu kulitokea mabadiliko makubwa katika maisha ya kila siku. Uchumi ulikuwa unaendelezwa, na mtizamo wa watu pia ulikuwa unabadilika, mimi pia nilianza kuwa na nguo kadhaa rasmi. Nilivaa shati, nakumbuka shati moja ya rangi mbalimbali, lilikuwa na mtindo na rangi za kisasa na kitambaa chenyewe kilikuwa cha kuhifadhi mazingira. Sikuwahi kutarajia kuvaa nguo ya namna hii."

Bibi Harida anatoka mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur, uliopo kwenye mpaka wa magharibi mwa China, alieleza kuwa tokea miaka ya 90, mavazi ya watu wa Xinjiang pia yamekuwa na mabadiliko mbalimbali sambamba na kuzidi kutekelezwa kwa sera ya mageuzi na kufungua mlango. Alisema  "Mavazi mbalimbali yanayopendeza na ya mtindo wa kisasa yaliingia kwenye soko la Xinjiang kutoka miji mikubwa ya Beijing, Shanghai na Guangzhou, na hata nchi za nje. Watu wa Xinjiang wanatumia pesa nyingi katika kununua mavazi, kwani wakazi wengi wa mkoa huo wanatoka makabila madogomadogo ambao wana tabia ya kupenda zaidi kujipamba, na wanapenda kugharimia nguo nzuri na mapambo mbalimbali. Hali hii inalingana na wasichana wa sehemu nyingi za China."

Hivi sasa imeingia karne ya 21, wachina wanaona mavazi si kama tu yanafanya kazi ya kuhifadhi joto mwilini, bali pia kuonesha mvuto na umaalumu wa mtu binafsi.

Bw. Bai Shangcheng kutoka kabila la Wahui alisema"Hivi sasa nguo zina mitindo na rangi mbalimbali, kila mtu ana umaalumu wake, anaweza kuvaa kama anavyopenda. Bila shaka sharti la kwanza ni maendeleo ya uchumi na kuinuka kwa kiwango cha maisha, ndipo watu wanapokuwa na uwezo wa kununua nguo wanazopenda."

Bibi Jin Lanying kutoka mkoa wa Shandong aliwahi kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 1988, na mwaka huu kwa mara nyingine tena alichaguliwa kuwa mbunge. Alitoa maoni yake kuhusu mabadiliko ya mavazi ya watu wa China, alisema "Nilichaguliwa kuwa mbunge wa bunge la awamu ya 7. Ninalinganisha picha yangu ya wakati ule, naona mavazi ya wakati ule yamepitwa na wakati, na hivi sasa ninaonekana kijana zaidi kutokana na kuvaa kwa mtindo wa kisasa zaidi. Zamani mimi na dada zangu tulichangia suruali moja tu, na hivi sasa tuna uwezo wa kutumia Yuan elfu moja, mbili kununua nguo."

Idhaa ya kiswahili 2008-04-03