Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-07 16:50:19    
Putin na Bush wafanya mazungumzo ya kuagana

cri

Rais Vladimir Putin wa Russia na rais George W. Bush wa Marekani ambaye yuko ziarani nchini Russia, tarehe 6 walifanya mazungumzo huko Sochi, mji wa kusini mwa Russia. Kutokana na kuwa rais Putin atamaliza muda wake wa urais mwezi Mei mwaka huu, vyombo vya habari vinayaita mazungumzo hayo kama ni mazungumzo ya kuagana kati ya wakuu hao wawili. Baada ya mazungumzo hayo, nchi hizo mbili zilitoa taarifa kuhusu uhusiano wa kimkakati kati ya Russia na Marekani.

Imefahamika kuwa mazungumzo hayo yalihusu uhusiano kati ya Russia na Marekani, upanuzi wa Jumuiya ya NATO, mfumo wa kinga dhidi ya makombora, hali ya Mashariki ya Kati na suala la Kosovo. Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo inasema, vita baridi vimemalizika, Russia na Marekani zinapaswa kushirikiana na nchi nyingine duniani katika juhudi za kukabiliana na masuala magumu na changamoto zinazoikabili dunia nzima katika karne ya 21, na kugeuza uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuwa maswahibu wa kimkakati kutoka mahasimu wa kimkakati. Rais Putin wa Russia alisema, taarifa hiyo inalenga siku za mbele na kutoa tathmini sahihi kwa uhusiano kati ya Russia na Marekani kwa hivi sasa. Na rais Bush wa Marekani pia alisema, vita baridi vimemalizika, hakuna haja ya kushikilia mambo ya zamani. Aidha alisema Marekani inaunga mkono Russia ijiunge mapema na Shirika la biashara duniani WTO. Msaidizi wa rais wa Russia Bw. Sergei Prihodko alipogusia taarifa hiyo alisema, taarifa hiyo imejumuisha historia ya ushirikiano kati ya Russia na Marekani, kuamua mwelekezo wa ushirikiano huo katika siku zijazo, kwa hiyo inafaa kwa taarifa hiyo ichukuliwe kuwa ni mpango wa uhusiano kati ya Russia na Marekani katika kipindi hiki na siku za mbele.

Lakini taarifa hiyo haikuepusha kutaja maoni ambayo Russia na Marekani zinapingana kuhusu suala la mfumo wa kinga dhidi ya makombora barani Ulaya. Kwenye taarifa hiyo Russia inasisitiza kuwa, Russia haikubali hatua ya Marekani ya kuweka mfumo huo nchini Poland na Czech, hata hivyo Russia inafurahia mapendekezo yaliyotolewa na Marekani kuhusu suala hilo. Pande hizo mbili zilikubaliana kuendelea na mazungumzo juu ya suala hilo katika siku zijazo, na kuanzisha utaratibu wa kazi utakaoshirikisha pande tatu za Russia, Marekani na Ulaya ili kukabiliana na tishio la makombora. Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mazungumzo hayo, rais Putin alisema njia mwafaka ya kuondoa wasiwasi wa Russia kuhusu suala la mfumo wa kinga dhidi ya makombora ni kutafiti na kuanzisha mfumo wa kinga dhidi ya makombora duniani, na kuusimamia mfumo huo kwa njia za usawa na kidemokrasia, kwani huu utakuwa ni mfumo mwafaka wa kuhakikisha usalama wa nchi zote.

Ni dhahiri kuwa hivi sasa suala la kuweka mfumo wa kinga dhidi ya makombora ni hitilafu kubwa kuliko nyingine katika uhusiano kati ya Russia na Marekani, rais Putin na rais Bush wamekuwa wakibadilishana maoni mara kwa mara kuhusu suala hilo tangu walipoingia madarakani. Na suala hilo litaendelea kuwasumbua warithi wao.

Wachambuzi wametoa maoni tofauti kuhusu mazungumzo hayo ya kuagana kati ya marais wa Russia na Marekani. Baadhi yao wanasema mazungumzo hayo yanasaidia kuhimiza uhusiano kati ya nchi hizo mbili, na wengine wanasema baada ya Marekani kugusa mara kwa mara kanuni za kimkakati za Russia, safari hii Bush anajaribu kutumia fursa ya rais mpya wa Russia kuingia madarakani ili kuufanya uhusiano kati ya Marekani na Russia urudi na kuendelezwa kwa kufuata njia ya kawaida.

Idhaa ya kiswahili 2008-04-08