Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-11 16:17:26    
Wazimbabwe wengi zaidi wataelewa utamaduni wa China

cri

Mkurugenzi wa chuo cha Confucius cha chuo kikuu cha Zimbabwe ambaye pia ni mkurugenzi wa chuo cha fasihi cha chuo kikuu hicho Bw. Pedzisai Mashiri, hivi karibuni alipohojiwa na mwandishi wa habari wa shirika la habari la China, Xinhua alisema, ana matumaini kuwa wazimbabwe wengi zaidi wanaweza kukifahamu chuo cha Confucius, na wanaweza kujifunza lugha ya Kichina, na wazimbabwe wengi zaidi pia wanaweza kuelewa utamaduni wa China. Bw. Mashiri alisema mkurugenzi wa chuo kikuu cha umma cha China Bw. Ji Baocheng atafanya ziara kwenye chuo cha Confucius wakati wa kuadhimisha mwaka mmoja tangu chuo cha Confucius cha chuo kikuu cha Zimbabwe kianzishwe, na chuo hicho cha Confucius kitatumia fursa hiyo kuwaoneshea wazimbabwe utamaduni wa China. Chuo hicho cha Confucius kitaandaa semina za mfululizo kuhusu historia, sera za kidiplomasia, dini, vyakula na matibabu ya jadi ya China. Vilevile chuo hicho kitaandaa mashindano ya utoaji wa hotuba kwa lugha ya Kichina.

Tarehe 16 mwezi Machi ni siku ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu chuo cha Confucius nchini Zimbabwe kianzishwe. Tarehe 14 mwezi Aprili mkurugenzi wa chuo kikuu cha umma cha China Bw. Ji Baocheng ataongoza ujumbe na kukagua kazi ya chuo cha Confucius cha Zimbabwe, pia atatoa hotuba kuhusu njia ya maendeleo ya uchumi wa China. Kutokana na kukabidhiwa kazi na ofisi ya uongozi ya uenezaji wa lugha ya Kichina ya China, chuo kikuu cha umma cha China kinashughulikia ujenzi wa chuo cha Confucius katika chuo kikuu cha Zimbabwe.

Bw. Mashiri alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa sera ya serikali ya Zimbabwe kuhusu kuiga uzoefu kutoka kwa China imehimiza uhusiano na mawasiliano kati ya China na Zimbabwe. Kutokana na kuhimizwa na sera hiyo, mashirika, kampuni na watu wengi zaidi wanataka kujifunza lugha ya Kichina na utamaduni wa China. Aidha, katika miaka ya hivi karibuni uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Zimbabwe umekuwa ukiendelezwa kwa kasi, na safari mbili za moja kwa moja kati ya China na Zimbabwe kila wiki zilizoanzishwa na Shirika la ndege la Zimbabwe pia zimeleta urahisi kwa mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Bw. Mashiri alisema ingawa chuo cha Confucius cha Zimbabwe kimekuwepo kwa mwaka mmoja tu, lakini kimepata mafanikio makubwa. Alijulisha kuwa mwaka jana, watu 241 walishiriki kwenye masomo ya lugha ya Kichina ya chuo hicho, wakiwemo mke wa rais Robert Mugabe na watoto wao wawili. Mwezi Julai mwaka jana, wanafunzi 19 wa chuo hicho walikuja nchini China kushiriki kwenye shughuli za wiki moja za mawasiliano ya utamaduni, hii iliwahimiza kupenda zaidi kujifunza na kuelewa utamaduni wa China. Mwezi Septemba mwaka jana wanafunzi wa chuo hicho waliokamilisha masomo ya lugha ya Kichina na utamaduni wa China walipata shahada ya kwanza ya chuo kikuu cha Zimbabwe. Hivi sasa wanafunzi wengi walioshiriki kwenye masomo ya lugha ya Kichina ya chuo cha Confucius ni wafanyabiashara na waandishi wa habari. Bw. Mashiri alisema yeye na watu anaoshirikiana nao wameweka mpango wa muda mrefu na muda mfupi wa kuendesha chuo hicho cha Confucius. Kuanzia mwezi Agosti hadi mwezi Septemba mwaka huu, chuo hicho cha Confucius kitatumia muda wa mapumziko ya shule nchini Zimbabwe kuandaa masomo ya lugha ya Kichina kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Licha ya Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, kwenye sehemu nyingine za nchi hiyo, hasa kwenye miji mikubwa na sehemu za utalii, pia kuna watu wengi wanaotaka kujifunza lugha ya Kichina. Lakini hivi sasa chuo cha Confucius kiko mjini Harare, watu wa sehemu nyingine hawana mazingira ya kujifunza lugha ya Kichina. Bw. Mashiri alisema kutokana na hali hiyo, anazingatia kutuma walimu wa chuo cha Confucius kwenye sehemu nyingine, na kuandaa masomo ya lugha ya kichina ya muda mfupi. Bw. Mashiri alisisitiza kuwa lengo la chuo cha Confucius ni kufundisha lugha ya Kichina kwenye vyuo vikuu vya walimu nchini Zimbabwe, na kuandaa wazimbabwe wenye ujuzi wa kufundisha lugha ya Kichina, hivyo masomo ya lugha ya Kichina yanaweza kuingia kwenye masomo ya shule za msingi, na wazimbabwe wanaweza kujifunza lugha ya Kichina wakiwa watoto.

Habari nyingine zinasema, kongamano lilliloendeshwa na benki ya maendeleo ya kusini mwa Afrika na kituo cha utafiti wa China nchini Afrika Kusini kuhusu China na suala la utandawazi wa uchumi wa kanda ya Afrika, lilifanyika mjini Johannesburg kuanzia tarehe 21 mwezi Machi hadi tarehe 1 mwezi Aprili. Maofisa, wataalamu, wasomi na wanaviwanda zaidi ya 150 walihudhuria kongamano hilo.

Mkuu wa benki ya maendeleo ya kusini mwa Afrika alisema tangu China ilipoanza kufanya mageuzi na kufungua mlango, ilipata mafanikio makubwa katika maendeleo ya uchumi. Bara la Afrika linataka kujifunza uzoefu wa China, linakaribisha China kushiriki kwenye ujenzi wa utandawazi wa uchumi wa kanda ya Afrika, na kuwasaidia waafrika milioni 900 kuondokana na umaskini. Mtaalamu wa uchumi wa benki ya maendeleo ya Afrika alisema, ushirikiano kati ya China na Afrika ni wa kirafiki, na China inahimiza maendeleo ya Afrika pamoja na urafiki. Ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika unafanyika kwa pande zote kwa kufuata kanuni za kimataifa, pia unafuata kanuni za uchumi wa soko huria. Na mtafiti mwandamizi wa chuo kikuu cha Stellenbosch aliona kuwa China inaonesha umuhimu mkubwa zaidi katika mchakato wa utandawazi wa uchumi wa kanda ya Afrika. Ikilinganishwa na nchi nyingine za magharibi, China inafanya ushirikiano wa kiuchumi na Afrika na kutoa misaada kwa Afrika bila masharti. Aliona kuwa ushirikiano na China unanufaisha moja kwa moja maendeleo ya kasi ya nchi mbalimbali.

Profesa wa chuo kikuu cha Witwatersrand cha Afrika Kusini alisema, ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika unalenga mahitaji ya Afrika, China inawekeza katika sekta zinazohitaji maendeleo barani Afrika, na nchi mbalimbali barani Afrika zinaona kihalisi faida ilizoleta China.

Idhaa ya kiswahili 2008-04-11