Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-09 19:52:47    
Bibi Betts Rivet kutoka Marekani anayefundisha Kiingereza huko Fuzhou

cri

Bi. Betts Rivet mwenye umri wa miaka 80 alipata shahada ya udaktari wa saikolojia, na alifanya kazi ya ualimu kwa miaka 5 hadi 6. Kabla ya kuja China, alitembelea zaidi ya nchi 70. Siku moja miaka 15 iliyopita, muda mfupi baada ya kustaafu Bi. Betts alisoma habari moja kuhusu chuo cha wanawake cha Fuzhou cha China. Bi. Betts alisema:

"nilisoma habari kuhusu chuo cha wanawake cha Fuzhou katika gazeti la Marekani. Habari hiyo iliandikwa na Dk. Liu aliyehitimu na aliwahi kufundisha katika chuo hicho. Niliposoma habari hiyo, nilikuwa nimestaafu, kwa hivyo nilijiuliza kama naweza kwenda kufundisha huko?"

Mwanzoni Bi. Betts alikuwa na wasiwasi kwa kuwa hakuwahi kwenda China, na alikuwa hajui hata kidogo kuhusu chuo hicho nchini China. Kwa hivyo alimwandikia barua Dk. Liu aliyeandika habari ile na aliwapigia simu walimu watano kutoka nchi za nje waliokuwa wanafundisha katika chuo hicho, ili kupata habari kuhusu chuo hicho. Bi. Betts alipata jibu zuri kutoka kwao kuwa chuo cha wanawake cha Fuzhou ni chuo kizuri, chenye watu wema na mazingira mazuri. Baada ya uchunguzi Bi. Betts aliamua kufundisha katika chuo hicho lakini kwa muda tu. Bi. Betts alisema:

"nilijiambia mwenyewe kuwa ninapaswa kujaribu mambo mapya na tofauti. Utamaduni wa China na Ulaya ni tofauti sana. Kwa hivyo niliamua kwenda kujaribu kufundisha katika chuo hicho, lakini kwa mwaka mmoja tu."

Mwezi Agosti mwaka 1992 ambapo Bi. Betts alikuwa na umri wa miaka 64 alifika Fuzhou akiwa peke yake. Njiani alikuwa anafikiri sehemu hiyo ambayo ataishi kwa mwaka mmoja ni ya namna gani, kama ataweza kuelewana na watu wa huko, na kama ataweza kuwasiliana na watoto bila matatizo. Lakini wakati alipokanyaga uwanja wa ndege wa Fuzhou, wasiwasi wote ulitoweka. Bi. Betts alisema:

"Nilikuja China peke yangu, sikujua ni mambo gani yatatokea. Nilipokwenda nje ya uwanja huo, niliona watu watano wenye tabasamu usoni wakishika ubao uliokuwa umeandikwa "karibu kwenye chuo cha wanawake cha Fuzhou". Nilifikiri, tayari nimefika."

Chuo cha ufundi kwa wanawake cha kusini mwa China alichofundisha Bi. Betts ni chuo cha elimu ya juu cha kiserikali chenye historia ya miaka 100. Chuo hicho kilichoko kwenye vitongoji vya mji wa Fuzhou kilijengwa kwenye kando ya milima na kutoka kwenye chuo hicho, eneo zima la mji wa Fuhzou linaonekana vizuri. Bi. Betts anapenda sana chuo hicho na alizoea kwa haraka maisha ya huko. Bi. Betts alisema:

"wiki mbili baada ya kuja chuo hicho, niliamua kuishi hapa."

Katika chuo hicho, Bi. Betts alikuwa mwalimu wa kitivo cha lugha ya Kiingereza na kitivo cha elimu kwa watoto. Bado anakumbuka hali ya mara ya kwanza alipokuwa anafundisha darasani. Alipoingia darasani wanafunzi wote walikuwa wamekaa vizuri na kumwangalia mwalimu huyo mpya kwa macho ya udadisi. Bi. Betts alisema:

"mara ya kwanza nilipowaona wanafunzi wangu, nilikuwa naona wao wote wanafanana, sikuweza kutambua nani ni nani. Wote walikuwa na nywele nyeusi na walikuwa wanavaa nguo zinazofanana. Kwa hiyo jambo la kwanza nililofanya ni kuwaambia wachagua wenyewe majina ya Kiingereza, kwa kuwa chuo hicho ni chuo cha lugha za kigeni. Halafu nikaandika majina yao kwenye kadi na kuweka kwenye meza zao. Kwa hivyo hatimaye niliweza kutambua wanafunzi wote. Hadi sasa bado ninafanya hivyo, inanisaidia kukumbuka majina yao haraka."

Mwanafunzi wake Bi. Chen Qiong alisema, hadi leo bado anakumbuka vizuri njia maalum ambayo Bi. Betts anafundisha. Bi. Chen Qiong alisema:

"katika shule ya sekondari ya juu darasani wanafunzi wanaandika kama walivyofundishwa na mwalimu. Lakini katika darasa la Bi. Betts, tunaona ni rahisi sana. Bi. Betts anafundisha kwa njia maalum, anaona kuwa matamshi ni muhimu, kama ukiweza kutamka maneno, basi utaweza kuyaandika. Tunaweza kujifunza mambo mengi kutoka kwa Bi. Betts wakati tukifanya michezo pamoja naye."

Mbali na kazi ya ufundishaji, Bi. Betts pia anashiriki kwa shauku kubwa kwenye kazi za usimamizi wa chuo hicho, kutoka mageuzi ya ufundishaji hadi matengenezo ya madirisha ya darasa. Mkuu wa chuo hicho Bw. Lin Benchun alisema, Bi. Betts ni mtu muhimu ambaye hakubadilishwa na chuo hicho. Bw. Lin Benchun alisema:

"Bi. Betts anapenda sehemu hiyo, anatoa mchango mkubwa kwa shughuli za elimu kwa wanafunzi wa kile. Walimu wengi waliokuja kufundisha katika chuo chetu walivutiwa naye. Alianzisha tovuti moja kusajili walimu; pia alishiriki yeye mwenyewe katika kazi ya kutangaza na kufahamisha kuhusu chuo chetu. Ana moyo wa kujizatiti katika shughuli za elimu, na wanafunzi wote wanampenda."

Mwaka 2006 Bi. Betts alipewa tuzo ya urafiki ya taifa inayotolewa na serikali ya China, ili kusifu mchango aliotoa kwa ajili ya maendeleo ya elimu ya China. Alipokumbuka jambo hilo, alisema:

"nilipewa tuzo hiyo mwaka jana na ina maana kubwa sana. Mara kwa mara najiuliza kwamba kama ninastahili kupewa tuzo hiyo, au kama wangetoa tuzo hiyo kwa watu wengine? Lakini ninafurahi sana kupewa tuzo hiyo. Hii ni heshima ya kweli. Tuzo hiyo iliyotengenezwa kwa dhahabu tupu ina thamani kubwa. Si kama tu kwa sababu ya dhahabu bali zaidi ni maana yake."

Bi. Betts alisema kama hatakuwa na matatizo ya kiafya, ataendelea kuishi nchini China na kuendelea kufundisha katika chuo hicho. China ni maskani yake ya pili, hapa kuna jamaa na marafiki yake.