Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-04-10 16:32:52    
Bei ya nafaka inayopanda kwa kasi duniani inaleta hali mbaya

cri

Mkuu wa Benki ya Dunia Bw. Robert Zoellick hivi karibuni ameonya kwamba bei ya nafaka inayopanda kwa kasi imesababisha baadhi ya nchi kukabiliwa na tishio la njaa, na kuzifanya baadhi ya nchi zinazoendelea zipoteze mafanikio yao yaliyoptikana katika juhudi za miaka kadhaa katika mapambano yao dhidi ya umaskini. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon pia amekuwa na wasiwasi kuhusu kupanda huko kwa bei.

Hivi karibuni bei ya nafaka imekuwa inapanda kwa kasi katika sehemu mbalimbali duniani, bei ya ngano na mahindi imekuwa juu kabisa ambayo haijawahi kutokea katika miaka yote kumi iliyopita, na bei ya mchele imepanda kwa zaidi ya 30%. Bei ya mchele kutoka Thailand inayozalisha mchele kwa wingi duniani imepanda na kuwa kubwa kuliko miaka 20 iliyopita, kupanda huko kwa bei kumesababisha mfumuko wa bei ambao haujawahi kutokea nchini humo katika miaka miwili iliyopita. Ili kukabiliana na hali hiyo, baadhi ya nchi zimechukua hatua za kuzuia nafaka kuuzwa nchi za nje ili kukidhi mahitaji ya nchini. Vietnam na Misri zimechukua hatua za kuzuia mchele kuuzwa nchi za nje kwa kupandisha ushuru wa forodha. Lakini hatua hizo za nchi zinazozalisha mchele kwa wingi zimechangia kupanda bei na kuzifanya nchi zinazonunua mchele zikumbwe na matatizo makubwa zaidi.

Kupanda kwa bei ya nafaka licha ya kuwa kumeathiri moja kwa moja maisha ya kimsingi ya wananchi wa kawaida, na kusababisha kupanda kwa bei ya bidhaa nyingi katika nchi nyingi zinazoendelea, na familia nyingi zinakabiliwa na matatizo ya chakula. Kutokana na malalamiko ya kupanda kwa bei, hivi karibuni maandamano makubwa na mgomo wa kazi yametokea nchini Misri, na mgomo huo ulisababisha vurugu. Hali kadhalika, kupanda kwa bei ya mahindi na mikate pia kumesababisha maandamano makubwa nchini Mexico. Nchini Yemen watoto walifanya maandamano wakidai watatuliwe shida la njaa. Nchini Philippines mwezi uliopita ilitokea hali ya watu kulimbikiza mchele bila kuuza, na serikali ilipaswa kuchukua hatua.

Wataalamu wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa wamefafanua kuwa, kupanda kwa bei ya nafaka kunatokana na sababu kubwa kadhaa. Kwanza maafa ya kimaumbile yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yalitokea mara kwa mara na kusababisha uzalishaji wa nafaka kupungua. Katika miaka ya hivi karibuni ukame ambao haujawahi kutokea katika miaka mia moja iliyopita, ulitokea katika sehemu za uzalishaji wa nafaka nchini Australia. Hali mbaya ya hewa pia imesababisha uzalishaji wa ngano kupungua katika sehemu za uzalishaji barani Ulaya. Sambamba na hayo mahitaji ya nafaka yanaongezeka. Pili, kutokana na mabadiliko ya mazoea ya matumizi ya chakula, mahitaji ya mafuta ya mimea na protini ya nyama ya mifugo yanaongezeka kwa kasi, nafaka kwa ajili ya chakula cha mifugo zinatumika zaidi, na baadhi ya nchi zinaendeleza nishati safi kwa kutumia chakula. Kutokana na hayo "akiba ya chakula" imekuwa hatarini. Zaidi ya hayo sababu nyingine ni kupungua kwa thamani ya dola za Marekani na kusababisha mfumuko wa bei duniani.

Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Bw. Robert Zoellick alionya kuwa kupanda kwa bei ya nafaka kunazifanya baadhi ya nchi zikabiliwe na tishio la njaa na juhudi zao za kupambana na umaskini zimepotea bure. Alitaka "Makubaliano Mapya kuhusu Sera za Chakula" yapatikane haraka, ili kutatua tatizo la chakula kwa watu maskini, na amezitaka nchi zilizoendelea zitoe misaada ya haraka kwa nchi zinazoendelea.

Ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa hivi karibuni inaonesha kuwa kupanda kwa bei ya nafaka sio kwa muda tu, bali kutaendelea katika kipindi kirefu kijacho. Ripoti inasema kama misaada ya chakula haitaweza kuongezeka, basi kuna haja kutoa misaada kwa kiasi maalumu kwa nchi maskini. Hivi sasa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa limekuwa likifanya mazungumzo kuhusu msukosuko wa chakula ili kujadili misaada hiyo ya chakula. Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao hivi karibuni alisema, akiba ya chakula nchini China ni ya kutosha, na serikali ya China imetunga sera nyingi za kuhamasisha uzalishaji wa chakula, China ina uwezo wa kujikimu.